Monday, December 10, 2012

Wabeba mizigo Kilimanjaro kutetewa bungeni

By Daniel Mjema, Moshi

MAKAMU Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, Abdulkarim Shah, ameahidi kulivalia njuga tatizo la malipo kiduchu wanayolipwa wabeba mizigo ya watalii na waongoza watalii katika Mlima Kilimanjaro.


Tovuti ya Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa), imetamka bayana waongoza watalii katika mlima huo wanapaswa kulipwa si chini ya Dola 20 za Marekani kwa siku sawa na Sh33,000 na mbeba mizigo Dola 10 za Marekani kwa siku sawa na Sh16,000.
Lakini mbali na kuwapo kwa sharti hilo la Kinapa, lakini baadhi ya waongoza watalii wamejikuta wakilipwa Sh10,000 kwa siku huku Wabeba mizigo wakilipwa hadi Sh5,000 na wakati mwingine wakibebeshwa mizigo mizito kinyume cha utaratibu uliowekwa.


Ni kutokana na kunyonywa huko na baadhi ya kampuni za utalii, kundi hilo lilimtafuta kwa siri Shah wakati akipanda mlima huo wiki iliyopita na kumuomba atumie mamlaka ya Bunge kuhakikisha wenye kampuni wanabanwa ili wawalipe inavyostahili.


Shah alilazimika kuzungumza na makundi hayo kila alipowakuta katika lango hilo kabla hajaanza safari ya kupanda mlima huo na kuwahakikishia kuwa amesikia kilio chao na atapeleka kilio hicho bungeni.


ili Bunge litumie mamlaka yake kuisimamia Serikali.
“Matatizo yenu yote tumeelezwa namna mnavyonyonywa na kulipwa ujira kidogo na baadhi yenu kubebeshwa mizigo mizito na nataka niwahakikishie kuwa tumewasikia na hatutawaangusha na tutalifanyia kazi kwa uzito unaostahili,”alisema Shah.


Shah ambaye alipanda mlima huo pamoja na wabunge wenzake sita, aliishia Kituo cha mwisho cha Kibo Hut kilichopo urefu wa meta 4,700 kutoka usawa wa bahari, akiwa amebakiza 1,195 kufika kilele cha Uhuru.


Wakati huohuo, Chama cha waongoza watalii Mkoa Kilimanjaro (KGA), kimepata viongozi wapya ambapo Mtanzani pekee aliyeweka rekodi ya kupanda mlima Everest ambao ni mrefu duniani, Wilfred Moshi alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti.


Katika uchaguzi huo uliofanyika mwishoni mwa wiki, Respicius Baitwa alichaguliwa kuwa mwenyekiti huku James Mong’ateko akichaguliwa kuwa Katibu na Gerald Mwaimu akichukua nafasi ya Mweka Hazina katika chama hicho ambacho kinafufuliwa upya.

-->