Afungua kesi kupinga adhabu ya kunyongwa

Muktasari:

Wakili wa kujitegemea Jebra Kambole amefungua kesi hiyo Mahakama Kuu akipinga adhabu ya kunyongwa akitaka watu waliotiwa hatiani kwa makosa ya mauaji waitwe tena kwa ajili ya kuadhibiwa upya.

Dar es Salaam. Wakili wa kujitegemea, Jebra Kambole amefungua kesi ya kikatiba Mahakama Kuu Masjala Kuu, akipinga adhabu ya kunyongwa hadi kufa, ambayo imekuwa ikitolewa na Mahakama Kuu kwa watu wanapatikana na hatia kwa baadhi ya makosa makubwa kama mauaji na uhaini.

Katika kesi hiyo, Kambole anayewakilishwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), anaiomba mahakama itamke kwamba kifungu cha 197 cha Kanuni za Adhabu (Penal Code- PC), Sura 16, marekebisho ya mwaka 2002, kinakinzana na Katiba hivyo, iamuru kifungu hicho kiondolewe katika sheria za nchi.

Pia, anaiomba mahakama iamuru watu ambao tayari wameshatiwa hatiani kwa makosa ya mauaji waitwe tena kwa ajili ya kuadhibiwa upya.

Katika hati ya madai aliyoiwasilisha mahakamani wiki iliyopita na hati ya kiapo kinachounga mkono madai yake, Kambole anadai kuwa masharti ya lazima ya adhabu ya kifo yanakinzana na Katiba kwa sababu yanaondoa usawa katika mashtaka.

Anadai kuwa masharti ya Kanuni za Adhabu Sura 16 (Marekebisho ya 2002, yanatoa sharti la lazima la adhabu ya kifo kwa watu wanaotiwa hatiani kwa makosa ya mauaji.

Amedai mahakama yenye mamlaka ya kusikiliza kesi hizo ina mamlaka ya uchaguzi wa kutoa adhabu kulingana na mazingira ya kesi na kwamba mtu aliyetiwa hatiani ana haki kujitetea ili apewe adhabu ndogo, kwamba mazingira yanayosababisha makosa ya mauaji hutofautiana.

Anadai kuwa ibara za Katiba ya Nchi ambazo adhabu hiyo ya kifo inakiuka ni ya 14, 13 (6) (a) (e), 13(6)(d) na 12(2).