Ajali Mbeya zamshusha cheo kigogo wa polisi akiwa eneo la ajali

waziri mpya wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola.

Muktasari:

Uamuzi wa Fungu kushushwa cheo ulitolewa jana na waziri mpya wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola jijini Dar es Salaam ikiwa ni saa chache baada ya ajali nyingine iliyoua watu watano.

Mbeya/Dar. Mfululizo wa ajali za barabarani mkoani Mbeya umemshusha cheo mkuu wa Usalama Barabarani mkoani humo, Leopold Fungu.

Uamuzi wa Fungu kushushwa cheo ulitolewa jana na waziri mpya wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola jijini Dar es Salaam ikiwa ni saa chache baada ya ajali nyingine iliyoua watu watano.

Lugola alimuagiza katibu mkuu wa wizara hiyo, Meja Jenerali Jacob Kingu kumshusha cheo Fungu ambaye alikuwa mrakibu wa polisi hadi kubaki na nyota tatu ikiwa na maana anakuwa mrakibu msaidizi wa polisi.

Pamoja na uamuzi huo, Lugola pia aliagiza kushushwa cheo kwa kamanda wa Kikosi cha Zimamoto mkoani Kagera, George Mrutu.

Hata hivyo, alisema alipanga kuwafukuza kazi Mrutu na Fungu, lakini hakufanya hivyo kwa kuwa jana ilikuwa siku yake ya kuzaliwa.

“Niliamua kuagiza wafukuzwe kazi, lakini kwa bahati mbaya na nzuri kwao mimi nilizaliwa siku ya Ijumaa na leo ni siku ya Ijumaa,” alisema Lugola.

“Siku ambayo nimezaliwa kuna kitu kinaitwa happy birthday (heri ya kuzaliwa). Sasa wakati naimbiwa happy birthday napaswa kufurahi kufurahi.Halafu huku unasema fukuzeni hao basi hata hako kafuraha sitokapata kwa uhalisia, hii ndio bahati kwao.”

Alisema pengine angefanya hivyo siku tofauti, askari hao watakiona cha moto kwa kuwa sheria ziko wazi, hivyo ametuma salamu kwa Polisi na Zimamoto kuwasimamia vizuri askari na kuwabadilisha kimtazamo

“Nyakati hizi siyo zile za mwaka ‘47, Serikali ya John Magufuli inataka vyombo vyake kuwa kielelezo na kioo,” alisema.

Lugola aliyekuwa katika kikao cha kimkakati cha viongozi wa taasisi za wizara hiyo pia alimfukuza kikaoni kamishna mkuu wa Magereza, Dk Juma Malewa kwa kuchelewa kikaoni.

Waziri huyo aliagiza mlango wa chumba walimokuwa wakifanyia kikao ufungwe itakapotimu saa 5:00 asubuhi na Dk Malewa aliingia kikaoni saa 5:01 na akaamriwa kuondoka.

Licha ya kuomba msamaha, Lugola alikataa kumruhusu kuingia kikaoni.

Ajali Mbeya

Wakati Lugola akiagiza Fungu ashushwe cheo, usiku wa kuamkia jana kulitokea ajali iliyosababisha vifo vya watu watano na mmoja kujeruhiwa eneo la mlima wa Igawilo iliyohusisha gari dogo aina ya Noah na lori.

Katika ajali hiyo, lori lililokuwa na mizigo lilifeli breki likiwa mlimani na kuigonga Noah, kisha kuilalia.

Fungu aliyekuwepo eneo la tukio hadi wakati taarifa za kushushwa kwake cheo zinatolewa na Waziri Lugola, alisema shughuli za uokoaji zilikuwa ngumu kutokana na lori hilo kuwa na mizigo mingi mizito.

Ajali ya jana ni mfululizo wa ajali zilizotokea mkoani humo ambapo Julai 2, lori liliangukia mabasi madogo matatu na kusababisha vifo vya watu 20.

Juni 14 watu 13 walifariki dunia, wakiwamo vijana 11 waliokuwa mafunzoni wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), katika ajali iliyotokea kwenye mteremko wa Igodima.

Julai Mosi, Rais John Magufuli alifanya mabadiliko madogo ya baraza la mawaziri na kumuondoa Mwigulu Nchemba katika uwaziri wa Mambo ya Ndani na Lugola kuteuliwa kushika nafasi hiyo.

Kadhalika, Rais aliagiza kuchukuliwa hatua kwa makamanda wa polisi wanaosuasua katika utekelezaji wa majukumu yao ikiwamo kukabiliana na matukio ya ajali za barabarani.

“Nimechoka kutuma salamu za rambirambi, kila siku inatoka ajali hii, inakuja hii. Kwa bahati mbaya ni mimi ninayetuma rambirambi, waziri wa Mambo ya Ndani hahangaiki...” alisema Rais wakati akimwaapisha Lugola na viongozi wengine aliowateua hivi karibuni.