Alichokisema Zitto baada ya kuachiwa kwa dhamana

Muktasari:

  • Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe, Baada ya kushikiliwa kwa siku mbili na Jeshi la Polisi, na jana kufikishwa mahakamani na kuachiwa kwa dhamana mbunge huyo amewataka Watanzania kujenga mshikamano ili kuisimamia Serikali.

Dar es Salaam. Baada ya kushikiliwa kwa siku mbili na Jeshi la Polisi, na jana kufikishwa mahakamani na kuachiwa kwa dhamana, Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe amewataka Watanzania kujenga mshikamano ili kuisimamia Serikali.

Zitto alitoa kauli hiyo nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kutakiwa kuzungumza na wanahabari, huku akisikitishwa kwa kutoshiriki kongamano la uchumi na siasa lililofanyika juzi katika Chuo Kikuu Dar es Salaam.

Katika kongamano hilo, Rais John Magufuli alikuwa miongoni mwa washiriki ambapo alizungumzia masuala mbalimbali ukiwemo mchakato wa Katiba Mpya akieleza kuwa kwa sasa si kipaumbele cha Serikali yake.

Hata hivyo, Zitto akizungumza jana alisema ni lazima Watanzania wajenge mshikamano na ushirikiano ili kuleta mabadiliko kwa kuisimamia Serikali ipasavyo.

“Hatuwezi kuona viongozi wakubwa wa kisiasa wakishtakiwa kila siku, ni kushindwa kuisimamia Serikali,” alisema.

“Kila mtu ameumizwa wakiwemo wafanyabiashara kubambikiwa kodi, wakulima na wafugaji na wanasiasa kushindwa kufanya majukumu yao.”

Kuhusu mdahalo huo, alisema atakaa na kufanya tathmini ya kilichozungumzwa.

Asomewa mashtaka matatu

Zitto alifikishwa mahakamani hapo saa 7:22 mchana baada ya kushikiliwa na polisi tangu Oktoba 31, ambapo alisomewa mashtaka matatu ya uchochezi.

Wakili wa Serikali mwandamizi, Tumaini Kweka alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kuwa, mshtakiwa huyo alitenda makosa hayo Oktoba 28 katika mkutano na wanahabari uliofanyika makao makuu ya ACT - Wazalendo.

Katika shtaka la kwanza kwenye kesi hiyo ya jinai namba 327, Kweka alidai kwa nia ya kuleta chuki kwa wananchi dhidi ya Jeshi la Polisi, Zitto alitoa maneno ya uchochezi.

Alidai katika mkutano huo, Zitto alisema majeruhi wanne katika mapambano kati ya wananchi na polisi waliokwenda Kituo cha Afya cha Nguruka kutibiwa walifuatwa na polisi na kuwaua.

Kweka alidai maneno hayo yalikuwa ni ya uchochezi yenye kuleta hisia ya hofu na chuki.

Katika shtaka la pili, alidai, “Katika mkutano huo, Zitto alisema ‘lakini tumefuatilia kwa kina jambo hili, taarifa ambazo tumezipata kutoka kijijini Mpeta Nguruka, Uvinza ni mbaya, ni taarifa ambazo zinaonyesha wananchi wengi sana wameuwa.”

Alidai, Zitto aliongeza kuwa, “Na Jeshi la Polisi pamoja na kwamba Afande Sirro (Simon, Inspekta Jenerali wa Polisi) wamekwenda kule halijatoa taarifa yoyote kuhusu wananchi...kama hawa Wanyantuzu walivamia eneo la ranchi, kuna taratibu za kisheria za kuchukua na siyo kuwaua wananchi wengine.”

Katika shtaka la tatu, Kweka alidai kwamba siku hiyo Zitto alitoa waraka kwa umma ukiwa na maneno ya uchochezi kwa nia ya kuleta chuki kwa Watanzania dhidi ya polisi.

Akinukuu waraka huo, alisema, “Tumekuwa tukifuatilia kwa kina yanayojiri yote huko Uvinza ...tunasikitika kusema kuwa taarifa tunazozipata kutoka Uvinza zinaogofya mno kwani tunaambiwa kuwa wananchi zaidi ya 100 wa kabila la Wanyantuzu wamepoteza maisha kwa kupingwa risasi na polisi, wengine wakisemwa kuuawa hata wakiwa kwenye matibabu hospitali baada ya kujeruhiwa kwenye purukushani na Jeshi la Polisi...”

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Zitto alikana na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi bado haujakamilika.

Hata hivyo, Wakili Kweka aliiomba mahakama isitoe dhamana kwa Zitto na kuwasilisha hati ya kiapo iliyoapwa na Mkuu wa Upelelezi wa Polisi Mkoa wa Kinondoni (SSP), John Malulu.

Katika hati hiyo waliiomba mahakama isitoe dhamana kwa sababu za kiusalama, na pili upelelezi wa kesi bado haujakamilika, ukiwa unaendelea katika eneo la tukio linalodaiwa kutokea mauaji hayo.

Pia, upande wa mashtaka ulidai kuwa ikiwa mshtakiwa huyo ataachiwa kwa dhamana anaweza kuingilia upelelezi.

Wakili wa utetezi, Peter Kibatala aliiomba mahakama impatie dhamana mshtakiwa huyo na kwamba, hati ya kiapo iliyowasilishwa na upande wa mashtaka ina upungufu wa kisheria ikiwamo kutopaswa kutajwa vifungu vya kisheria.

Hakimu Shaidi baada ya kusikiliza hoja hizo alisema katika hati ya kiapo lazima kuwepo na sababu za kutosha na za msingi kupinga dhamana na kwamba iliyowasilishwa na upande wa mashtaka haina sababu za kutosha zaidi ya usalama.

Alisema ni jukumu la polisi kulinda raia na mali zao na kushangazwa na jeshi hilo kuhofia usalama wa Zitto wakati ni jukumu lao kuhakikisha kila raia anakuwa salama.

Hakimu alimtaka Zitto kuwa na mdhamini mmoja mwenye kitambulisho atakayesaini bondi ya Sh10 milioni, ambapo alitimiza masharti na kuachiwa, huku kesi hiyo ikiahirishwa hadi Novemba 26.