‘Ambulance’ ilivyochukua roho za wanafunzi, wafanyakazi UDSM

Muktasari:

Ajali hiyo ilihusisha gari la kubeba wagonjwa (ambulance) walilokuwa wamepanda wanafunzi hao na lori

Dar es Salaam. Mwanamuziki wa bendi kongwe nchini ya Sikinde, Shaaban Dede aliwahi kuimba wimbo usemao, “Nani kauona mwaka.” Ndani ya wimbo huo miongoni mwa maneno yaliyomo, “ni majaliwa ya Mungu kuuona mwaka...”

Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) waliokuwa na ndoto nyingi maishani mwao, lakini zilizimika ghafla juzi usiku baada ya kupoteza maisha kwa ajali ya gari.

Ajali hiyo ilihusisha gari la kubeba wagonjwa (ambulance) walilokuwa wamepanda wanafunzi hao na lori lililokuwa likitokea Ubungo kwenda Buguruni katika barabara ya Mandela.

Naibu waziri wa afya na kefteria wa Serikali ya Wanafunzi wa UDSM (Daruso), John Kodi alisema mmoja wa wanafunzi hao alikuwa anakimbizwa hospitali kutokana na tatizo la kifafa na mwingine alikuwa na malaria kali.

Wengine waliofariki dunia katika ajali hiyo ni muuguzi, dereva wa gari na mhudumu wa wanafunzi wa chuo hicho.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa na Daruso iliwataja waliofariki kuwa ni Maria Gordian ambaye alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza na Steven Sango wa mwaka wa pili.

Taarifa hiyo pia ilisema mwanafunzi mwingine aliyekuwa katika gari hilo, Abishai Nkiko hali yake ni mbaya na mpaka jana jioni alikuwa anapata matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Mwananchi lilifika nyumbani kwa wazazi wa marehemu Maria na kuzungumza na baba mzazi, Gordian Soko aliyesema mtoto wake amefariki ikiwa ni siku mbili baada ya kusherehekea siku yake ya kuzaliwa. Alisema Maria alizaliwa Juni 9.

“Jumamosi ndiyo ilikuwa siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa alikuja hapa nyumbani kwa kuwa mimi na yeye tunaishi kama marafiki, nikamuuliza anataka zawadi gani akaniambia anataka hela akanunue keki ale na wenzake na atarudi nyumbani kesho yake kutuletea keki,” alisema mzazi huyo.

“Kesho yake kweli alikuja na nikaonana naye jioni, nikaondoka nikamwacha akijiandaa kurudi chuo. Kwa kawaida anatoa taarifa akifika chuo, lakini siku nyingine hujisahau na hakutoa taarifa.”

Alisema taarifa za tukio la ajali alizipata juzi kupitia mtandao wa Facebook licha ya kuwa zilimshtua, lakini kwa wakati huo hakujua kama zilimhusisha mtoto wake. “Hadi nilipopata taarifa kwa wanafunzi wanaosoma naye,” alisema Soko.

Kuhusu ratiba ya mazishi, mzazi huyo alisema wanaendelea kuwasiliana na uongozi wa chuo, lakini mazishi yanatarajiwa kufanyika Ijumaa katika makaburi ya Kondo Ununio jijini hapa.

Akizungumzia chanzo cha ajali hiyo, kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema ilisababishwa na uzembe wa dereva wa gari la wagonjwa.

Alisema ‘ambulance’ ilitoka upande mmoja na kuingia upande wa pili ilipo Hoteli ya Land Mark katika eneo lisilopaswa kupita magari yanayoelekea Ubungo na kuligonga lori lililokuwa limeegeshwa.

“Ni uzembe wa dereva wa gari la wagonjwa la UDSM, aliingia upande wa pili kizembe bila kuangalia na akiwa katika mwendo mkali na kusababisha ajali iliyoleta vifo na majonzi kwa jamii,” alisema.

Wanafunzi wazungumza

Akizungumzia tukio hilo, mwanafunzi aliyekuwa akisoma na Maria, Rashid Sungura (25) alisema yeye na wenzake wawili walitaka kuwasindikiza wenzao kwa kutumia gari hilo, lakini dereva aliwazuia kwa kuwa lilikuwa limejaa.

“Alikuwa na tatizo lililokuwa linasababisha apoteze fahamu, lilipompata tatizo hilo tukampelekea zahanati ya hosteli, lakini watoa huduma wakafanya mawasiliano ili aje kuchukuliwa na gari la kubebea wagonjwa ambalo ndilo hilo alipata nalo ajali,” alisema.

Sungura ambaye ni kiongozi wa darasa, alisema kwa kuwa walikuwa wanne wote wanaume walimpendekeza msichana aongozane na Maria. “Dereva alimwambia yule msichana atangulie barabarani atamkuta baada ya kumchukua mgonjwa mwingine, kama baada ya dakika 10 nilisikia taarifa ya ajali ya gari hilo. Nikampigia simu yule dada aliyetakiwa kumsindikiza akaniambia yupo chumbani amelala, dereva alipomkuta barabarani alimwambia arudi tu gari limejaa,” alisema Sungura.

“Tulipofika Muhimbili saa sita usiku ndipo tuliporuhusiwa kwenda mochwari kutambua miili, nafika pale nikauona kwanza mwili wa mwanafunzi mwingine kisha Maria. Wakati huo mpaka sasa nilikuwa natafakari ile ajali na kutafakari endapo ningekuwa ndani ya gari hilo,” alisema Sungura.