Apandishwa kizimbani kwa tuhuma ya kumbaka mtoto

Muktasari:

  • Wengine wawili matatani kwa tuhuma ya kutishia kuua kwa panga

Dar es Salaam. Mkazi wa Kinondoni B jijini Dar es Salaam, Rajabu Ally (18) amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni kujibu shtaka la kumbaka mtoto wa kike wa miaka 15.

Mtuhumiwa huyo alisomewa hati ya shtaka leo mbele ya Hakimu Karorine Kiliwa, ambapo wakili wa Serikali, Neema Moshi alidai kosa hilo alilitenda Agosti 2017 na Mei tarehe tofauti maeneo ya Kinondoni Mahakamani.

Alidai mshtakiwa alifanya kosa hilo huku akitambua ni kinyume cha sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Wakili wa Serikali huyo baada ya kusoma hati ya mashtaka mtuhumiwa alikana kutenda kosa hilo na Hakimu Kiliwa alileza kwa mujibu wa sheria shtaka hilo linadhaminika.

Mshtakiwa alirudishwa rumande baada ya kutotimiza masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili kutoka taasisi inayotambulika hadi kesi hiyo itakapotajwa tena Septemba 26.

Wakati huo huo, mkazi wa Kunduchi, Patrick Robison (40) na mkazi wa Kawe, Bushir Theophil (42) wamepandishwa kizimbani katika mahakama hiyo wakikabiliwa na shtaka la kumtishia kimuua kwa panga Karim Azizi.

Akisoma hati ya mashtaka leo, Wakili wa Serikali, Ramadhan Mkimbu mbele ya Hakimu Joyce Mushi alidai watuhumiwa hao walitenda kosa hilo Mei 22 maeneo ya Nyakanekwa.

Baada ya kusomewa mashtaka yao, watuhumiwa walikana kosa hilo na Hakimu Mushi alisema shtaka hilo linadhaminika na masharti yake ni kuwa na wadhamini wawili kutoka taasisi inayotambulika wenye vitambulisho watakaosaini bondi ya Sh1milioni kwa kila mmoja.

Washtakiwa walirudishwa rumande baada ya kutotimiza masharti ya dhamana na kesi hiyo itatatajwa tena Septemba 26.