Asilimia 90 ya dawa nchini zinanunuliwa nje ya nchi

Muktasari:

Serikali mewahamasisha wazalishaji wa dawa kutoka nje kuwekeza Tanzania kwa kuanzisha viwanda kwa sababu soko lipo

Dar es Salaam. Zaidi ya asilimia 90 ya dawa zinazotumika nchini zinanunuliwa nje ya nchi wakati asilimia sita pekee zikinunuliwa katika viwanda vitano vilivyopo nchini.

Hayo yamebainishwa leo Julai 16, 2018 jijini Dar es Salaam katika mkutano kati ya Bohari Kuu ya Dawa (MSD) na wazalishaji na wasambazaji 160 wa dawa kutoka nchi mbalimbali duniani.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Mpoki Ulisubisya amesema lengo la mkutano huo ni kuwashirikisha wazalishaji na

wasambazaji kujua uwezo wa MSD na kutambua fursa zilizopo nchini.

“Lengo la mkutano huu ni kuitikia wito wa Rais John Magufuli aliyetutaka kununua dawa kutoka kwa wazalishaji wenyewe badala ya kuwatumia middlemen (madalali),” amesema Dk Ulisubisya na kusisitiza kwamba bajeti ya dawa imeongezeka na kufikia Sh269 bilioni.

Dk Ulisubisya amewahamasisha wazalishaji wa dawa kutoka nje kuwekeza Tanzania kwa kuanzisha viwanda kwa sababu soko lipo.

Amebainisha kuwa mwaka jana pekee, MSD ilitumia Dola za Marekani 700 milioni kwa ajili ya kununulia dawa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurian Bwanakunu amesema upatikanaji wa dawa muhimu 135 umefikia asilimia 93 na wamekuwa wakitoa kipaumbele kwa wazalishaji wa ndani.