VIDEO: Azam TV ilivyopanga kuboresha ladha, ukaribu na washiriki

Mkurugenzi mtendaji wa kituo cha televisheni cha Azam, Tido Mhando

Muktasari:

  • Azam TV ni miongoni mwa wadhamini wa mashindano ya kampuni 10 bora za kati (Top 100) ambaye amekuwapo kwa miaka minne sasa. Mashidano ya mwaka huu, mkurugenzi wake mmtendaji, Tido Mhando ameahidi kuongeza ladha kwa ajili ya washiriki wote kwa kuwapa jukwaa la kukutana na kubadilishana mawazo na uzoefu.

Mkurugenzi mtendaji wa kituo cha televisheni cha Azam, Tido Mhando amesema wamejipanga kuongeza ladha kwa watazamaji wao katika shindano la Top 100 litakalofanyika mwishoni mwa mwezi huu.

Top 100 ni shindano la kila mwaka linalozishindanisha kampuni za kati zenye mapato kati ya Sh1 bilioni na Sh20 bilioni na kuzitunuku zinazofanya vizuri. Miongoni mwa vigezo vinavyozingatiwa ni uzingatiaji wa sheria za biashara, rekodi za mauzo na matumizi pamoja na kukagua hesabu hizo za biashara.

Azam TV imekuwa ikirusha matangazo mubashara ya fainali hizo kwa miaka minne mfululizo, lakini mwaka huu, Mhando anasema kutakuwa na kitu cha ziada kwa watazamaji wao pamoja na washiriki. Anasema wamejipanga kuwashirikisha wahusika ambao watajieleza ili kuleta sura nyingine ya kipindi na si kama ilivyokuwa miaka ya nyuma yalipokuwa yanarushwa matangazo ya tukio pekee.

“Tutazungumza haraka sana baada ya tukio la kutangazwa kwa washindi ili watueleze zaidi kuhusu kampuni zao zinafanya nini. Mtu anayetazama pengine anaweza kuvutiwa na kuhamasishwa kutokana na historia,” anasema Mhando.

Pia, anasema wakati huo shughuli itakuwa na vionjo tofauti vyenye mvuto na msisimko wa kuwekwa katika televisheni kwani kwa miaka minne iliyopita ushiriki ulikuwa si wa viwango vilivyotarajiwa. “Miaka minne ambayo Azam TV imehusika, ushirika wake haukuwa mkubwa. Sasa tumeanza kufanya mabadiliko kwa kuongeza ubunifu.”

Anasema kuwa miaka hiyo Azam TV ilikuwa inaonyesha fainali za shindano hilo kwa kulirusha mubashara kupitia televisheni yao, lakini mwaka jana walianza kubadilika na kuongeza ubunifu zaidi kwenye maudhui.

Mwaka jana, anasema, baada ya fainali Azam TV iliwakaribisha chakula cha usiku washiriki wote waliofika hatua ya mwisho na waliitumia fursa hiyo kufanya mazungumzo ya kufahamiana zaidi na kubadilishana mawasiliano, hivyo kukuza biashara kati yao.

“Ubunifu ule ulileta matokeo makubwa kiasi lakini sasa watu watarajie makubwa zaidi,” anasisitiza mkurugenzi huyo.

Anasema Azam TV inawatengenezea washiriki vipindi maridadi na makala za kampuni zao ili kuwa karibu nao kuliko kawaida.

Hiyo, pamoja na makala zinazochapishwa na kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL inayochapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti, itasaidia kuwatambulisha kwa wananchi wengi zaidi hivyo kuwaongezea wateja.

“Mwaka jana baada ya kumaliza shindano tuliketi tukaona hatujitendei haki kwa sababu hata sisi tunataka kuwa karibu na wafanyabiashara na lile ni kundi kubwa sana ambalo ukiwa karibu nalo huna haja ya kuwafuata maeneo mengine.”

Kwenye hafla hiyo ya chakula cha usiku iliyofanyika mwaka jana, anasema waligundua, tofauti na siku ya fainali, wafanyabiashara hawana mahali ambako wanaweza wakakaa na kujadili mambo yao na kushauriana zaidi, hivyo wakati wa hafla hiyo muda mwingi waliutumia kubadilishana mawazo.

Kuhusu mapokeo ya watazamaji, Mhando anasema mara nyingi baada ya tukio kurushwa hupokea maoni mengi jambo linaloonyesha kuwa matangazo ya Top 100 yanafuatiliwa na wadau wengi wa uchumi na biashara nchini.

“Baada ya pale, utasikia watu wanawazungumzia washindi au tukio zima kwa ujumla, ndiyo maana kwetu ni mradi muhimu sana ambao lazima tuufanye,” anasema.

“Katika tathmini zetu za wiki wakati wa Top 100 tumegundua kuwa tumetazamwa zaidi kuliko siku nyingine za kawaida ukiachilia mbali vipindi vya mpira ambavyo vina watazamaji wengi kutokana na umaarufu wa mchezo huo.”

Ingawa kurusha matangazo mubashara ni gharama kubwa, anasema ukiona yanafanyika ujue kuna uhakika wa watu kutazama na mara zote watazamaji huangalia kitu chenye faida kwao siyo kile kitakachowapotezea muda.

Maboresho wanayokusudiwa kufanywa kwenye vipindi vya matangazo ya mashindano ya Top 100, anasema Mhando kuwa ni ya kawaida kama ilivyo kwa kila kitu duniani kwa kuwa kibinadamu watu wanachoka kuangalia vitu ambavyo havibadiliki.

“Lazima viingizwe vitu vingine vya kuongeza chachu ili kila mwaka washiriki waone kitu kipya badala ya kuona ya kawaida tena yanayojirudia. Changamoto yangu kwa waandaaji wasibaki kuwa ni watu wanaotekeleza ratiba ya kila mwaka, bali kuwe na ubunifu mpya kila mwaka,” anasema.

Anaongeza kuwa shindano hilo limedumu kutokana na umakini wa waandaaji na washiriki, pengine ni kutokana na kiu ya mafanikio kwa kampuni ndogo.

Anasema shindano la Top 100 ni kipimo kizuri cha kampuni za kati kwa kuzingatia kuwa ndizo zilizopo katika changamoto nyingi na jambo la faraja ni kwamba halina kashfa ya upendeleo.

Kwa miaka minane sasa MCL kwa kushirikiana na kampuni ya kimataifa ya ukaguzi wa hesabu za fedha na ushauri wa kibiashara na uwekezaji ya KPMG wanaandaa shindano hilo linalolenga kutambua mchango wa kampuni za kati kwenye maisha ya wananchi na pato la Taifa.

Inaelezwa kuwa endapo kundi hilo litawezeshwa ndilo lenye uwezo wa kuchangia kiasi kikubwa cha mafanikio katika utekelezaji wa sera ya uchumi wa viwanda unaopigiwa chapuo na Serikali kutokana na uzoefu lililonalo kwenye sekta tofauti za uchumi.

Kadri siku zinavyokwenda, idadi ya wajasiriamali wanaotaka kuendesha biashara zao kisasa zaidi ili kuzitumia fursa zilizopo kwenye soko la ndani hata kimataifa inazidi kuongezeka.