Baba mbaroni kwa kumtia mimba binti yake

Meneja wa Utetezi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa) Zanzibar, Hawra Shamte.

Muktasari:

  • Hata hivyo, kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Thobias Sedeyoka alisema jana kuwa kwa sasa yupo likizo, lakini amesikia uwepo wa taarifa za binti aliyetiwa mimba na baba yake.

Zanzibar. Polisi katika Mkoa wa Mjini Magharibi wanamshikilia Muhammed Juma Muhammed kwa tuhuma za kumtia mimba binti yake wa kambo mwenye umri wa chini ya miaka 18.

Hata hivyo, kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Thobias Sedeyoka alisema jana kuwa kwa sasa yupo likizo, lakini amesikia uwepo wa taarifa za binti aliyetiwa mimba na baba yake.

“Hivi sasa naongea na wewe nipo kijijini, lakini bila shaka taarifa hiyo wakati imefika Kituo cha Polisi Bububu naamini maofisa wangu wataifanyika kazi,” alisema.

Taarifa za kitendo kilichofanywa na mtuhumiwa huyo zilijulikana baada ya polisi kupatiwa taarifa na sheha wa Shehia ya Kijichi, Simba Ally Makame ambaye alipewa taarifa hizo na vijana wanaoshiriki ulinzi shirikishi. Binti huyo kwa sasa ameshajifungua.

Baba amtaja ibilisi

Baada ya kukamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi katika Kituo cha Polisi Bububu, baba huyo alikiri kufanya kitendo hicho huku akidai kuwa “shetani alimpitia”.

Muhammed alisema licha ya kuwa alifanya kitendo hicho, hakuwa akifanya peke yake.

“Ni ibilisi tu aliniingia na kuanza kufanya kitendo hiki ambacho leo naelezwa kuwa nimempa mimba mtoto wa mke wangu huku akiwa tayari ameshajifungua,” alisema baba huyo akiwa mikononi mwa polisi.

Sheha, Tamwa wazungumza

Sheha wa Shehia ya Kijichi, Makame alisema awali alipokea taarifa kutoka kwa askari wa ulinzi shirikishi na kuripoti tukio hilo polisi. Alisema ili kujiridhisha, alikwenda hadi kwa mama wa binti ambaye aligoma kulizungumzia akidai ni suala la aibu, lakini akakiri mumewe kuwa na uhusiano na binti yake.

“Awali, hata mama mzazi wa mtoto tuliwahi kuzungumza naye lakini hakuwa tayari kutoa ushirikiano kwa madai ya kuogopa ndoa yake kuvunjika. Kuanzia hapo ndipo tukaona kuna haja ya kulivalia njuga suala hili,” alisema.

Meneja wa Utetezi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa) Zanzibar, Hawra Shamte alisema matukio ya aina hiyo hayapaswi kufumbiwa macho wala kuonewa aibu na kuitaka jamii kuyafichua.

Alisema ikiwa wananchi watajenga utamaduni wa kufichua matukio hayo vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto vitakoma.

Hawra alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha vinatenda haki yanapotokea matukio ya aina hiyo.

Awali, Kamanda Sedoyeka alisema ni vyema jamii ikajifunza na kufuata mila na desturi za Kitanzania kuliko kuendeleza matendo yanayokiuka maadili.