Bobi Wine kurejea Uganda leo, kupambana na polisi

Mbunge  wa Kyadondo, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine.

Muktasari:

  • Wakati polisi nchini Uganda wakionya mikusanyiko kwa ajili ya mapokezi ya mbunge wa Kyadondo, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, mwanasiasa huyo leo mchana Alhamisi Septemba 20, 2018 anatarajia kuwasili nchini huko akitokea Marekani

Kampala. Wakati polisi nchini Uganda wakionya mikusanyiko kwa ajili ya mapokezi ya mbunge  wa Kyadondo, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, mwanasiasa huyo leo mchana Alhamisi Septemba 20, 2018 anatarajia kuwasili nchini huko akitokea Marekani.

Bobi Wine, mwanamuziki aliyegeuka mwanasiasa ameapa kukaidi amri hizo, akieleza kuwa yeye ni raia huru wa Uganda mwenye haki zote za kutembea kokote hivyo asipangiwe nani ampokee na aende wapi.

Bobi Wine aliyekwenda Marekani kwa ajili ya matibabu baada ya kudai kupigwa na kuteswa wakati akiwa mikononi mwa polisi,  amesema kurejea kwake Uganda hakuwahusu polisi, hawapaswi kuhoji nani atampokea.

"Nimekuwa najiuliza kwa nini hawa maofisa wa polisi wanakubali kujidhalilisha kiasi hicho. Wanataka kuamua nani aje kunipokea na wapi nielekee baada ya kuwasili?” Amehoji.

“Basi kwa taarifa yenu, hakuna hata mwana familia mmoja ambaye atanipokea uwanja wa ndege, nitakutana nao nyumbani kwa sababu najua namna ya kufika nyumbani!.”

Amesema, “nitapokelewa na marafiki, viongozi wenzangu na wasanii wengine. Baada ya hapo nitakwenda na kumuona bibi yangu ambaye ni mgonjwa kwa muda mchache kitongoji cha Najjanankumbi na baada ya hapo nitaelekea Kamwokya kupata chakula cha mchana na wanafamilia (kaka na dada zangu) kabla ya kuelekea nyumbani kijijini Magere.”

Bobi Wine alitoa kauli hiyo kupitia katika tamko alilotuma katika mitandao ya kijamii kabla ya kuanza safari ya kurejea nyumbani.

Vyombo vya habari nchini Uganda vimemnukuu msemaji wa polisi, Emilian Kayima aliyewaambia waandishi wa habari kuwa atakapowasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Entebbe baadaye leo, mbunge huyo atapokelewa na familia yake na atapatiwa ulinzi kutoka uwanja wa ndege mpaka nyumbani.

“Polisi itaendelea kuhakikisha watu wanaotumia barabara wako salama. Hakutaruhusiwa mikutano, maandamano na mikusanyiko kinyume cha sheria. Harakati zozote ambazo zitahusisha mikusanyiko lazima zifuate sheria,” amesema Kamanda Kayima.

Baada ya kauli hiyo ya polisi  Bobi Wine  amesema, “mimi  ni mwananchi wa Uganda huru ambaye nina uhuru wa kuzunguka nchini kwangu.”

“Polisi si jukumu lao kunipangia mimi nani anipokee na nani hawezi kunipokea au wapi naruhusiwa kwenda na wapi siruhusiwi. Vizuizi hivi lazima vikome mara moja. Nitakutana nanyi marafiki zangu.”