‘Bunge live’ ndiyo kilio cha wananchi

Muktasari:

Maoni hayo ni matokeo ya utafiti uliofanywa na Taasisi ya Twaweza uliotolewa jana ambao pia, asilimia 65 ya wananchi wana hofu kuwa, kupitishwa Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari kutazuia utoaji taarifa za maovu yanayofanywa na Serikali.

Dar es Salaam. Asilimia 92 ya wananchi wanataka vipindi vya Bunge vionyeshwe moja kwa moja, huku asilimia 79 wamepinga uamuzi wa Serikali kuzuia matangazo hayo.

Maoni hayo ni matokeo ya utafiti uliofanywa na Taasisi ya Twaweza uliotolewa jana ambao pia, asilimia 65 ya wananchi wana hofu kuwa, kupitishwa Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari kutazuia utoaji taarifa za maovu yanayofanywa na Serikali.

Matokeo ya utafiti huo yametolewa wiki mbili baada ya Rais John Magufuli kutia saini muswada wa sheria hiyo unaoelezwa kukandamiza vyombo vya habari.

Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze alisema 2016 umegubikwa na changamoto kwa raia kupata taarifa na kutoa maoni yao kwa uhuru. Alisema kusitishwa kwa matangazo ya moja kwa moja ya Bunge kupitia runinga na redio ni moja ya changamoto hizo.

“Watanzania kadhaa wamechukuliwa hatua kali chini ya sheria ya uhalifu wa mitandao kwa kosa la kutoa maoni yao, vilevile mwaka huu ndipo sheria kandamizi ya huduma za habari imepitishwa na Bunge na kutiwa saini na Rais,” alisema.

Eyakuze alisema asilimia 88 wanasema Bunge lirushwe moja kwa moja bila kujali gharama, huku asilimia 12 wakisema lisionekane kwa sababu ya kubana matumizi.

Kuhusu uhuru wa kutangaza habari, asilimia 53 wanasema vyombo vya habari viwe huru kutangaza habari yoyote, huku asilimia 44 wakisema Serikali iwe na mamlaka ya kufungia magazeti.

Vilevile, asilimia 65 wanasema vyombo vya habari havijawahi kutumia vibaya uhuru wake kwa kutangaza vitu ambavyo si vya kweli na asilimia 95 ya wahojiwa waliunga mkono wananchi kuwa na uhuru wa kuikosoa Serikali pale wanapoona imekosea na kusisitiza uwapo wa demokrasia.

Akizungumzia utafiti huo mwanasheria Profesa Abdallah Safari alisema ni wakati wa Serikali kujitathmini na kuwapatia wananchi kitu wanachotaka.

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Dk Hellen Kijo-Bisimba na Profesa Damian Gabagambi walisema sheria ya huduma ya vyombo vya habari itakuwa kikwazo katika utoaji wa taarifa.

Gabagambi alisema kutokana na sheria hiyo, uhuru wa kujieleza umedhibitiwa.