Chadema ‘yaingia mafichoni’ kujipanga

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana alipokuwa akionyesha baadhi na nakara za matokeo ya uchaguzi mdogo wa Ubunge wa Jimbo la Ukonga, uliofanyika Septemba 16, mwaka huu. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe amezitaja sababu hizo kuwa ni pamoja na kutoandikishwa kwa wapigakura wapya tangu 2015, hujuma, kutumika kwa nguvu ya vyombo vya dola na kutishiwa wapigakura.

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetaja sababu tatu za kutoendelea kushiriki chaguzi ndogo zote zilizotangazwa na Tume ya Uchaguzi (NEC) kwa sasa, huku kikiamua ‘kuingia mafichoni’ kusuka mikakati yake.

Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe amezitaja sababu hizo kuwa ni pamoja na kutoandikishwa kwa wapigakura wapya tangu 2015, hujuma, kutumika kwa nguvu ya vyombo vya dola na kutishiwa wapigakura.

Mbele ya wanahabari jana, Mbowe alisema uamuzi huo ulichukuliwa juzi baada ya kamati ndogo ya Kamati Kuu kuketi na kutafakari uchaguzi mdogo uliofanyika Septemba 16 katika majimbo ya Ukonga, Dar es Salaam na Monduli, Arusha pamoja na kata 23 nchini.

Alidai kuwa katika chaguzi hizo kulikuwa na matumizi makubwa ya majeshi kutoka mikoa mbalimbali hali iliyowatisha wananchi kujitokeza kupiga kura.

Wakati Mbowe akitoa tamko hilo, tayari Tume ya Uchaguzi (NEC) imeshatangaza kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa Jimbo la Liwale mkoani Lindi na kata 37 utakaofanyika Oktoba 13.

Mwenyekiti wa NEC

Hata hivyo, akijibu malalamiko ya Chadema, mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Semistocles Kaijage alisema kila chama kina hiari ya kushiriki na tume haiwezi kukilazimisha.

“Tume inaendelea kufanya tathmini ya uchaguzi baada ya kukamilisha itatoa taarifa,” alisema.

Jaji Kaijage alisema, “kama uchaguzi ulifanyika kinyume cha sheria, wahusika walipaswa kufuata sheria kwa kwenda kutoa malalamiko yao kwenye vyombo husika badala ya kupeleka kwenye vyombo vya habari. Na hili la kutoshiriki uchaguzi, hatuwezi kulazimisha chama kigombee.”

Akizungumza huku akiangaliakaratasi zinazodaiwa kuwa ni za matokeo ya baadhi ya vituo, Mbowe alisema uchaguzi umegeuka kuwa kama vita kwa watu kupigwa na kuwekwa ndani, jambo linalowafanya kutokwenda kupiga kura. “Imani ya Watanzania sasa kuhusu ushiriki wao kwenye uchaguzi imefifia, watu hawaoni kama sanduku la kura siyo tena mwamuzi wa nani awe kiongozi, bali ni kauli ya viongozi,” alisema.

Alidai, “Rais aliwahi kusema anampa mtu gari, anampa mshahara na kazi, halafu amtangaze mpinzani, kauli hii imegeuzwa sheria na watendaji wote wa Serikali kuanzia wakuu wa wilaya, wa mikoa na wasimamizi wa uchaguzi katika kata zetu.”

“Sasa madhara makubwa yanayosaidia kubaka demokrasia ya Taifa yanaonekana dhahiri.”

Alisema wanawataka viongozi wa Serikali kutambua kuwa nchi inaongozwa kwa Katiba na sheria.

Mbowe alidai kuna mawakala wao walikamatwa, wakapigwa na kuwekwa mahabusu ya Kituo cha Polisi Sitakishari kilichopo Ukonga na sasa wamehamishiwa Kituo Kikuu cha Polisi.

Alisema walikamatwa wakiwa katika eneo la utetezi wa chama chao wakihakikisha haki na taratibu za uchaguzi zinafuatwa.

“Wameshakaa (ndani) zaidi ya saa 48, hivyo tunalitaka Jeshi la Polisi liwaachie haraka viongozi na mawakala wetu ambao walishikwa wakitekeleza wajibu wao,” alisema Mbowe.

Hata hivyo kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema hawashikilii wakala wala kiongozi wa Chadema. Alisema wakikamatwa watu kwa makosa mengine wao (Chadema) wanakimbilia kusema ni makosa ya uchaguzi.

Barua za utambulisho

Kuhusu barua za utambulisho, Mbowe alisema limekuwa kama donda sugu na hali hiyo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara.

Alitolea mfano wa uchaguzi mdogo wa Kinondoni uliofanyika Februari 17 ambao pia mawakala wao walinyimwa barua hizo, hali iliyosababisha kuzuka kwa vurugu. “Tulilazimika kuandamana ili kudai haki hii, lakini tulikamatwa, watu walipigwa risasi na tukafunguliwa kesi.”

Alisema wasimamizi wa uchaguzi hawatambulishwi mapema kwa sababu wana kazi maalumu ya kuhakikisha CCM inashinda.

Mbowe alisema jambo lingine ni kutoandikishwa kwa wapigakura wapya tangu ilipofanyika hivyo Agosti, 2015.

Alisema kuna Watanzania wengi walitimiza miaka 18 kuanzia Novemba, 2015 ambao wamekosa haki yao ya kupiga kura. “Inafanyika hivi makusudi kwa sababu wengi wao ni vijana ambao kwa kawaida ndiyo wapenda mabadiliko, kitendo hicho pia ni kinyume cha Katiba inayoongoza nchi,” alisema.

Kujitoa kushiriki uchaguzi

Alisema wanajitoa kwenye chaguzi zilizotangazwa, lakini wataendelea kufungua kesi mbalimbali za kikatiba Mahakama Kuu na Mahakama ya Afrika Mashariki, huku wakitumia muda huo kukihuisha chama chao.

Mbowe alisema, “tunaanza operesheni maalumu ya kujenga chama, huku katika kipindi hicho tukizindua dira ya chama ambayo kila mwanachama ataona huu ndiyo msimamo wa chama kuliko kushiriki uchaguzi ambao matokeo yameshapangwa.”

“Hatuwezi kushiriki hizo chaguzi kwa sababu kuna watu tayari wamechukua fomu Liwale wakidai wao ni Chadema, wakienda walioteuliwa na chama hawatapewa fomu.”

Alisema uamuzi huo wameuchukua kwa umakini mkubwa na si kwamba chama kimejitoa kabisa kwenye chaguzi zote za siku za usoni, bali wanajiondoa kwenye chaguzi ndogo zilizotangazwa.

Hoja ya kujiuzulu

kuhusu kujiondoa kwenye nafasi hiyo kutokana na kulaumiwa na wanaohamia CCM, Mbowe alisema huku akicheka kuwa, “walioniweka kwenye nafasi hii ni wanachama, wakisema niondoke nitafanya hivyo hata kesho na nitafurahi sana, lakini siwezi kuondoka kwa kelele za CCM.”

“Kila mtu akitoka lazima atafute mnyonge wake na mnyonge wa sasa ni Mbowe, wanafikiri labda Mbowe ningekuwa dhaifu.”

Alisema, “(nikiondoka) CCM watashangilia zaidi ili waendelee kushinda, hivi kweli kuna siku CCM wanaiombea Chadema Mbowe awe imara na Chadema iwe imara ili Chadema iweze kushinda, mimi bado hawajanipata kwenye kona ambayo nitawapigia magoti.”

Alisema kazi ya kuwa kiongozi wa chama si nyepesi, ni ya ujasiri na utume wenye misalaba ambayo siyo kila mtu anaweza kuibeba na kelele za wanaohama haziwaondoi kwenye reli.

“Kumbuka kila anapotoka diwani mmoja Chadema maelfu wanaingia, wapo wengi na tutawaibua utakapofika uchaguzi mkuu.” Chadema ilianzishwa Mei 28, 1992 na katika uchaguzi mkuu wa 1995 ilishinda majimbo manne ya uchaguzi kati ya 269 na madiwani 42 nchi nzima.