Mkutano mkuu wa chama tawala China kuanza kesho

Muktasari:

  • Mkutano huo unatarajiwa kuibuka na maazimio yatakayoleta  mabadiliko yenye mwelekeo wa maendeleo ya kisoshalisti.

Mkutano Mkuu wa 19 wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) unaanza kesho Jumatano Oktoba 18, 2017 pamoja na mambo mengine, ukitarajiwa kuchagua viongozi wapya watakaokuwa na jukumu la kusimamia mabadiliko ya katiba ya chama hicho.

Msemaji wa mkutano huo, Tuo Zhen amewaambia waandishi wa habari leo Jumanne kuwa, mkutano huo unatarajiwa kuibuka na maazimio yatakayoleta  mabadiliko yenye mwelekeo wa maendeleo ya kisoshalisti, ambayo amesema yameingia katika hatua muhimu ya kujenga jamii iliyo na mafanikio katika kila nyanja.

Amesema katika mkutano huo utakaofanyika katika Ukumbi Mkuu wa Mikutano wa Watu wa Beijing (Great Hall of the People in Beijing), wajumbe 2,200 watajadili utendaji wa chama wa miaka mitano iliyopita na hatua ambazo Kamati Kuu chini ya Katibu Mkuu, Xi Jinping imefanya katika kukiunganisha chama hicho na Wachina wote na kusimamia maendeleo ya kisoshalisti tangu mkutano wa 18.

Zhen amesema mkutano huo pia utajadili kwa kina mazingira ya sasa ya kitaifa na kimataifa ili kuwa na uelewa mpana wa matarajio ya wananchi na mahitaji mapya ya chama na nchi kwa jumla.

“Mkutano wa maandalizi umefanyika mchana huu na kupitisha ajenda. Jambo kubwa katika ajenda ni kupokea na kupitisha maazimio ya Kamati Kuu ya 18 ya Chama, ripoti ya utendaji ya Kamati Kuu ya 18 ya Chama ya Nidhamu na Ukaguzi, kujadili na kupitisha maazimio ya mabadiliko ya Katiba ya Chama cha Kikomunisti cha Watu wa China, kuchagua Kamati Kuu ya 19 ya Chama na kuchagua Kamati Kuu ya 19 ya Chama ya Nidhamu na Ukaguzi,” amesema.

Akizungumzia maandalizi ya ripoti ya kisiasa ya chama kwa ajili ya mkutano huo, Zhen amesema Kamati Kuu ilichukulia suala hilo kwa uzito na kuiundia kamati maalumu iliyoongozwa na Jinping na ‘makomredi’ waandamizi katika chama na maeneo mengine wakiwamo wataalamu na wanazuoni.

Amesema kamati hiyo ilifanya kazi chini ya usimamizi wa Kamati Kuu ya Siasa na Kamati ya Usimamizi (Standing Committee) ambazo kwa pamoja zilifanya mikutano kadhaa kupitia rasimu ya ripoti hiyo ambayo itawasilishwa katika mkutano huo.

Ili kufanikisha kazi hiyo, Zhen amesema maandalizi yalitegemea zaidi utafiti. Amesema Kamati Kuu ya CPC iliteua taasisi 59 kufanya utafiti katika maeneo makuu 21 ambayo yalizaa ripoti 80.