‘Changamkieni fursa zilizopo Dodoma’

Muktasari:

Wito huo ulitolewa juzi na Meya wa Manispaa ya Dodoma, Jafari Mwanyemba wakati akifungua semina ya wajasiriamali iliyoandaliwa na Mbunge wa Dodoma, Antony Mavunde kwa kushirikiana na Kampuni ya Hi-tech International ya jijini Dar es Salaam.

Dodoma. Wafanyabiashara wakubwa na wadogo mkoani hapa wametakiwa kuchangamkia fursa zinazopatikana kwa kujiongezea kipato kutokana na wingi wa watu wanaohamia.

Wito huo ulitolewa juzi na Meya wa Manispaa ya Dodoma, Jafari Mwanyemba wakati akifungua semina ya wajasiriamali iliyoandaliwa na Mbunge wa Dodoma, Antony Mavunde kwa kushirikiana na Kampuni ya Hi-tech International ya jijini Dar es Salaam.

Mwanyemba alisema mara nyingi watu hushindwa kuzitumia vyema fursa wazipatazo na huishia kuilaumu Serikali.

Mbunge Mavunde alisema kutokana na azma ya Rais, John Magufuli kuifanya Tanzania kuwa ya viwanda, angependa kuona Dodoma ikishamirishwa na viwanda.

Aliahidi kuendelea kuwasaidia wajasiriamali hao kwa kuwatafutia fursa mbalimbali zilizopo nchini ili wafikie malengo waliyojiwekea.

Mkurugenzi wa Hi-Tech International, Paul Mashauri aliwataka wajasiriamali kuwa na hamu ya mafanikio kwa kuthubutu kuwekeza katika biashara na kujenga tabia ya kujiamini.