DC aeleza sababu kuzuia mkutano wa Chadema

Mwenyekiti Chadema, Freeman Mbowe akizungumza na viongozi wa chama hicho wakati wa mkutano wa baraza la uongoza kanda ya Ziwa Victoria jijini Mwanza jana.Picha na Mpiga picha Maalum

Muktasari:

  • Mkutano wa Chadema uliopangwa kufanyika jana Jumapili Oktoba 20, 2018 wilayani Bariadi mkoani Simiyu umeshindwa kufanyika baada ya kuzuiwa na mkuu wa wilaya hiyo, Festo Kiswaga.

Dar es Salaam. Mkuu wa Wilaya Bariadi, Festo Kiswaga amesema walikubaliana na viongozi wa Chadema kusogeza mbele mkutano wao kwa kuwa kulikuwa na maandalizi ya ziara ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na kwamba hiyo ndiyo sababu ya kuwazuia kukutana.

“Tulikubaliana na viongozi wao kwamba wakati huu hatuwezi kuwa na matukio mawili kwa wakati mmoja hasa ukizingatia tumeanza wiki ya Sido kwa ajili ya viwanda vidogovidogo na wageni mbalimbali wanatarajia kuja. Tuliwaeleza wasogeze shughuli yao mbele,” alisema Kiswaga.

Wakati Kiswaga akieleza hayo, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema mkutano huo ulikuwa ufanyike katika ukumbi wa KKKT lakini katika hali ya kushangaza ulipigwa marufuku bila maelezo ya kina.

Alisema lengo la mkutano huo lilikuwa kupanga mikakati ya kufanikisha chaguzi zinazotarajiwa kufanyika hivi karibuni na ulikuwa mahsusi kwa ajili ya Kanda ya Serengeti inayohusisha mikoa ya Mara, Shinyanga na Simiyu.

“Tumeambiwa mkuu wa wilaya ndiye aliyetoa amri mkutano wetu usifanyike. Kama hiyo haitoshi gesti ambazo zilikuwa zimechukuliwa kwa ajili ya kuwahifadhi wageni wetu nazo pia zimezuiliwa,” alidai Mrema.

“Tunashangazwa namna viongozi wanavyotumia vibaya madaraka maana huu ni mkutano wa ndani na unafanyika kama katiba inavyoelekeza. Tumepata hasara kwa maana hiyo tunakusudia kumchukulia hatua za kisheria huyu mkuu wa wilaya kama yeye binafsi.”

Alisema kutokana na zuia hilo, chama hicho kililazimika kuhamishia mkutano huo wilayani Shinyanga ambako ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali.

Katika ufafanuzi wake, Kiswaga alidai Chadema hawakutoa taarifa kama wangekuwa na mkutano mkubwa wilayani humo ili kusaidia namna ya kuweka mazingira mazuri.

“Wao wana mwakilishi wao hapa na hakutuleza kama watakuwa na mkutano huo. Wangetueleza mapema nasi tungewaeleza siku hiyo kutakuwa na jambo fulani na wangepanga upya, isitoshe wao walitarajia kuwa na mawaziri wakuu wastaafu sasa lazima mambo yawekwe sawa hatuwezi kusimamia matukio mawili kwa wakati mmoja,” alisema.

Mbali ya utata huo, Mrema alisema leo, viongozi wakuu wa chama hicho wanaanza kuzunguka katika majimbo mbalimbali kwa ajili ya kujiimarisha na kujiandaa na uchaguzi wa chama hicho.

Kuhusu viongozi wakuu kufanya ziara, Mrema alisema, “Mwakani tunatarajia kufanya uchaguzi mkuu ndani ya chama, kabla ya uchaguzi huo, tunaanza na chaguzi za chini kwa maana ngazi za mashina, wilaya mpaka kanda.

“Viongozi wetu wamegawanywa katika kanda mbalimbali kwa mfano mwenyekiti wetu, Freeman Mbowe yeye ataanza Kanda ya Ziwa na baadaye kwenda maeneo mengine.”