Demokrasia ya vyama vingi ilivyogubikwa na fedha chafu

Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania, John Cheyo akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari alipokuwa akitoa tamko kuhusu mchakato wa Katiba na uchaguzi mkuu wa 2015, mjini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Miongoni mwa mabadiliko hayo ni kuyoyoma kwa sera ya ujamaa na kujitegemea iliyoasisiwa na Mwalimu Nyerere na kuibuka kwa mfumo wa soko huria. Kwa upande wa siasa, mfumo wa chama kimoja ulibadilishwa kwa kurejeshwa mfumo wa vyama vingi uliokuwa umefutwa miaka ya 1960.

Baada ya Mwalimu Julius Nyerere kung’atuka madarakani mwaka 1985, mabadiliko makubwa ya kisiasa na kiuchumi yalifanyika kupitia tawala zilizofuata baada ya yake.

Miongoni mwa mabadiliko hayo ni kuyoyoma kwa sera ya ujamaa na kujitegemea iliyoasisiwa na Mwalimu Nyerere na kuibuka kwa mfumo wa soko huria. Kwa upande wa siasa, mfumo wa chama kimoja ulibadilishwa kwa kurejeshwa mfumo wa vyama vingi uliokuwa umefutwa miaka ya 1960.

Mfumo wa soko huria ulioanza kutekelezwa chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi, ulifuatiwa na mfumo wa vyama vingi ulioanza kutekelezwa mwaka 1992 na uchaguzi mkuu wa kwanza ulioshirikisha vyama hivyo ukafanyika mwaka 1995.

Hapo ndipo kila chama cha siasa kilipoanza kupambana kutafuta wanachama wa kukiunga mkono na rasilimali fedha ili kichaguliwe.

Wakati wa Rais awamu ya tatu chini Rais Benjamin Mkapa kukawa na sera ya ubinafsishaji wa mashirika ya umma, huku pia nchini kukiwa na uwekezaji wa kampuni za kigeni.

Tangu wakati huo hadi awamu ya nne chini ya Jakaya Kikwete, kulikuwa na mwingiliano mwingi kibiashara kutokana na mfumo wa soko huria, huku baadhi ya viongozi wakionekana kujilimbikizia mali na hapo ndipo zilipoanza kuibuka kashfa za ufisadi zilizohusisha wizi wa mali na fedha za umma.

Kwa upande mwingine, janga la dawa za kulevya liliongezeka, huku ikielezwa kuwa wafanyabiashara haramu walijipenyeza katika siasa au kwa wanasiasa na kuchangia kampeni za vyama ya siasa.

Ripoti ya utafiti uliofanywa na taasisi ya Kuwezesha Afrika kupambana na uhalifu (Enact) iliyozinduliwa hivi karibuni jijini Dar es Salaam, inaoyesha kuwa biashara ya dawa za kulevya inahusika kuendesha siasa kwa baadhi ya nchi za Afrika, ikiwemo Tanzania.

Hata hivyo, utafiti huo uliofanywa kwa miezi minne kwa kuwahoji watu 240 katika nchi za Tanzania, Kenya, Msumbiji na Afrika Kusini, umeonyesha kuwa biashara ya dawa za kulevya imedhibitiwa hapa nchini, hasa baada ya hatua zilizochukuliwa na Serikali ya awamu ya tano.

Tanzania inavyopambana

Akifafanua kuhusu utafiti huo, mtafiti Peter Gastrow anasema biashara hiyo ilijipenyeza kwenye mifumo ya siasa kutokana na mfumo wa soko huria uliokuwapo.

Anasema kati ya mwaka 1990 na 2015, Tanzania ilipata maendeleo makubwa kiuchumi, lakini kipindi hicho pia kiligubikwa na kashfa za rushwa na ufisadi ndani ya Serikali huku fedha zikielekezwa kwa matajiri wachache.

“Licha ya kuongezeka kwa kashfa za ufisadi na umasikini, CCM imeendelea kuchaguliwa, huku vyama vya upinzani vikiongozwa na Chadema ikiendelea kuimarika kila uchaguzi,” anasema.

Akifafanua hali huyo, Simone Haysom aliyehusika katika utafiti huo, anasema tangu mwaka 1995 hadi 2015 ufadhili wa vyama vya siasa katika uchaguzi haukuwa na mikakati imara kiasi cha kuruhusu fedha chafu kutumika kwenye siasa.

Kwa mfano, anasema wakati wa Rais Mkapa, Serikali ilipitisha sheria ya takrima iliyowaruhusu wanasiasa kuwakirimu wapiga kura wao kwenye majimbo, jambo lililolalamikiwa na vyama vya upinzani kwa kuwapendelea wanasiasa wenye utajiri,” alisema.

Anasema kutoakana na ushindani wa madaraka na kutokuwepo kwa sheria madhubuti, kuliibuka mtindo wa wanasiasa kuwa wafanyabiashara, huku pia baadhi wakihusishwa na fedha chafu zinazotokana na biashara ya dawa za kulevya.

“Japo Chadema wanadai ukuaji wake unatokana na kuchukua tabaka la wasomi, wahojiwa wetu wanasema fedha chafu kwa CCM na upinzani ni chanzo muhimu cha fedha kampeni za pande zote mbili,” anasema.

Mtafiti huyo anaongeza: “Ilikuwa rahisi kujua mbunge anayechukua fedha kwa wafanyabiashara wa dawa za kulevya kwa kuwa walifanya kazi pamoja, ikiwezekana hata kugawa vyama ili kuwazuia wabunge wasitunge sheria na sera mbaya kwa biashara zao.”

Ripoti hiyo pia inazungumzia ufadhili wa vyama vya siasa katika kampeni ikitoa mifano ya matumizi ya helkopta yaliyoanzishwa na Chadema na kukifanya chama hicho kuwa maarufu kwa muda mfupi. Baada muda hata CCM ilianza kutumia aina hiyo ya usafiri katika kampeni zake.

“Kuongezeka kwa matumizi ya helkopta ni dalili ya kampeni za siasa zinazotegemea wafadhili kuliko nguvu ya matawi ya chama yanayotegemea nguvu ya wanachama kupata wapiga kura wapya. Aina hii ya ufadhili katika siasa unaibua maswali ya jinsi wagombea wanakopata fedha hizo.”

Ripoti hiyo inaendelea kubainisha kuwa hakukuwa na hatua kali dhidi ya biashara hizo: “Kwanza mikakati ya kupambana na dawa za kulevya haikuwa na nguvu ikiwa pamoja na kushindwa kuwakamata wahalifu wakiwa baharini.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watu waliokamatwa kwa makosa yanayohusu dawa za kulevya, walikuwa ni mawakala wa mitaani lakini wafanyabiashara wakubwa hawakuwekwa wazi. Kiasi kikubwa kilichokamatwa na mawakala hao wakati huo kilikuwa ni gramu 700.

Hatua mpya

Kuhusu utawala wa Rais Magufuli, ripoti hiyo inaeleza kuwa umegeuza mwelekeo wa CCM iliyokuwa ikilalamikiwa na wapinzani kuwa imeshindwa kupambana na watendaji wenye tuhuma za ufisadi.

“Tanzania kwa sasa inapitia mfululizo wa mabadiliko chini ya Rais Magufuli ambayo yanabadilisha uhusiano wa siasa na uhalifu katika nchi, huku kukiwa na dalili za kuwaondoa wahalifu katika baadhi ya maeneo,” anasema Gastrow.

“Tanzania inaweza kutajwa kama soko lililovurugika la uhalifu,” aliongeza.

Gastrow ametaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kuwataja hadharani watu maarufu waliohusishwa na dawa za kulevya wakiwamo wanasiasa, viongozi wa dini na wasanii.

Anataja pia hatua ya Rais Magufuli kufanya ziara za kushtukiza katika Bandari ya Dar es Salaam na kuibua usafirishaji wa mchanga wa madini na hivyo kuweka madai mapya ya kodi kwa mchanga huo.

“Kwa hali hiyo wafanyabiashara wengi wa dawa za kulevya na nyara za Taifa wameanza kuiogopa bandari ya Dar es Salaam, kwa kuwa Rais Magufuli na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wamekuwa wakiitembelea mara kwa mara kama mkakati wa kupambana na ufisadi,” inasema ripoti.

Taarifa za serikali

Akizungumzia ripoti hiyo, Kamishna wa Operesheni wa Mamlaka ya Kuzuia na kupambana na dawa za kulevya, Felix Milanzi anasema kwa kipindi cha mwaka mmoja tangu mamlaka hiyo imeundwa imeweza kudhibiti mianya yote iliyokuwa ikitumiwa awali kuingiza dawa za kulevya.

“Nakubaliana na wewe kwamba dawa bado zipo, lakini siyo kwa kiwango kile cha zamani,” alisema Milanzi.

Aliongeza; “Tumedhibiti kila mianya, ukienda uwanja wa ndege au baharini, kwa sasa tuko kule saa 24. Huwezi kuingiza dau lako baharini tusilikamate, maana zamani zilikuwa zikipaki meli kule baharini wanapaleka majahazi, siku hizi hakuna.”

Hata hivyo, alisema bado vita ni ngumu kwa sababu wafanyabiashara wana nguvu ya fedha kiasi cha kurubuni mifumo ya Serikali.

Jicho la pili

Kwa upande mwingine, utafiti huo pia umebainisha maoni tofauti ya wahojiwa wakisema juhudi hizo za Rais Magufuli zinawalenga pia wapinzani wake ndani na nje ya CCM, wakigusia baadhi ya watuhumiwa wa ufisadi ndani ya chama hicho kutoguswa.

“Kwa hali hii, hatua za Rais Magufuli na sera zake za kiuchumi zinalenga kujiimarisha zaidi kwa kudhibiti upatikanaji wa fedha kwa kambi rasmi ya upinzani na wakosoaji waliomo ndani ya CCM,” inasema ripoti.

Wahojiwa wengine wameonyesha wasiwasi kama hatua zinazochukuliwa na utawala wa sasa zinaweza zisiwe endelevu baada ya Rais Magufuli kumaliza muda wake, huku wakigusia usimamishwaji kazi kwa watendaji wa Serikali usiotabirika na kuwafanya kutokuwa na maamuzi.

Ripoti hiyo pia inagusia kudhoofika kwa uhuru wa habari, ikisema tangu Serikali ya awamu ya tano iingie madarakani, kuna magazeti matano yameshafungiwa.

Sheria ya gharama za uchaguzi

Pamoja na mafanikio yanayoonekana bado suala fedha za uchaguzi ni donda ndugu na ndiyo maana mwaka 2010, Bunge lilipitisha Sheria ya gharama za uchaguzi Na.6 ya 2010 inayoainisha vitendo ambavyo vikifanywa na mgombea au mwananchi wakati wa uchaguzi au kampeni anakuwa ametenda makosa chini ya sheria hiyo.

Kwa mfano, kutoa fedha za kukopesha au kuahidi kitu chochote ili kupigiwa kura, kutoa au kusaidia ajira sehemu za kazi, kutoa zawadi, mikopo, msaada au kuingia makubaliano; kutoa au kuwezesha kupatikana kwa uteuzi kutokana na zawadi kinyume na kifungu cha 21 (1)(d).

Katika kipengele cha malipo haramu, kifungu cha 22 (a na b) kimetamka malipo ambayo hayaruhusiwi kufanyika katika mchakato wa uchaguzi, kabla na baada. Ni kosa mtu yeyote ambaye kwa njia ya rushwa kutoa, kuandaa, kulipa kwa ujumla au sehemu, gharama ya kutoa au kuandaa chakula, mahitaji ya mtu kwa madhumuni ya kumshawishi mpiga kura katika mchakato wa uchaguzi.

Kipengele kingine kusafirisha wapiga kura kifungu cha 23 (1) (a), (3) na kifungu cha 23 (4) ambacho kimekataza mgombea kuwasafirisha wapiga kura kwenda au kutoka kwenye kituo cha kupiga kura kwa kukodi gari, kutoa nauli ya treni au vinginevyo.

Kosa hilo linamhusu mtu anayemiliki vyombo vya usafiri kwani imezuiwa kuruhusu au kukitoa kwa kukikodisha, kukopesha vyombo hivyo hali anajua kwamba wanasafirisha wapiga kura.