Dk Tulia asema bunge lipo shwari

Naibu Spika, Dk Tulia Ackson

Muktasari:

Awali, katika Bunge la Bajeti lililofanyika, Juni mwaka huu mjini Dodoma, wabunge hao walisusa kuhudhuria vikao vilivyoongozwa na Dk Tulia kwa madai ya kutokubaliana na uendeshaji wake.

Dar es Salaam. Baada ya kukumbana na misukosuko ikiwamo ya kususiwa vikao vya bajeti na wabunge wa upinzani, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson amesema mwenendo wa vikao vya Bunge la 11 vilivyofanyika mwezi uliopita hali ilikuwa shwari.

Awali, katika Bunge la Bajeti lililofanyika, Juni mwaka huu mjini Dodoma, wabunge hao walisusa kuhudhuria vikao vilivyoongozwa na Dk Tulia kwa madai ya kutokubaliana na uendeshaji wake.

Alipohojiwa jana katika Kipindi cha Power Breakfast cha Clouds FM, Dk Tulia alisema Bunge la Septemba lilikuwa tofauti ikilinganishwa na yaliyopita.

“Kama utakuwa mfuatiliaji utagundua kitu tofauti katika Bunge la Septemba na yale yaliyopita. Hili matukio ya watu kuambiwa wafanye hivi au vile hayakuwa mengi.  Mtu akiambiwa kaa anakaa,” alisema Dk Tulia.

Alisema hali ya baadhi ya wabunge kutofuata kanuni za Bunge imekuwa ikijitokeza kwa sababu wengi ni wapya.

“Ukifanya hesabu ni kama asilimia 65 ya wabunge ni wageni na kuna mambo mengi ya kujifunza. Mtu anaweza akafanya jambo kwa kufuata mkumbo,” alisema.

Alifafanua kuwa yeyote anayekalia kiti cha Spika kazi yake ni kuhakikisha wabunge wanafuata kanuni na taratibu.

“Mambo ya kuamua huwa yanapangiwa utaratibu na lazima uufuate ili kuwe na haki sawa kwa wote,” alisema.

Alifafanua kuwa anaipenda kazi yake na kwamba katika Bunge hakuna mtu anayemmudu mwenzake, isipokuwa ni kufuata  taratibu zilizowekwa.