Fagio la NSSF waomba lisogee mikoani

Muktasari:

  • Wameishauri bodi hiyo kufanya ziara mikoani kuwabaini baadhi ya wasimamizi wa mfuko huo ambao wameshindwa kutimiza wajibu wao, kwa kuwabana waajiri kuwasilisha michango ya wafanyakazi kwa wakati.

Pwani. Wafanyakazi wa sekta binafsi mkoani Pwani, wamepongeza uamuzi wa Bodi ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kuwasimamisha kazi wakurugenzi sita na mameneja watano, kwa tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi wakitaka usiishie makao makuu.

Wameishauri bodi hiyo kufanya ziara mikoani kuwabaini baadhi ya wasimamizi wa mfuko huo ambao wameshindwa kutimiza wajibu wao, kwa kuwabana waajiri kuwasilisha michango ya wafanyakazi kwa wakati.

Wiki iliyopita, Bodi ya NSSF iliwasimamishwa kazi vigogo hao kwa tuhuma za ubadhirifu, matumizi mabaya ya ofisi na kutofuata kanuni, sheria na taratibu katika uwekezaji, usimamizi wa miradi, ununuzi wa ardhi na ajira.