Faru kufungwa vifaa vya usalama kuwalinda na majangili

Muktasari:

  • Mpango huo utagharimu Sh253, wanyamapori hao watafuatiliwa kila eneo watakalokuwa

Arusha. Ulinzi wa faru katika Hifadhi ya Serengeti na maeneo jirani unatarajiwa kuimarika zaidi baada ya kuanza kwa mradi wa wanyamapori hao kufungwa kifaa cha kisasa cha kujua walipo lengo likiwa ni kuwalinda na ujangili au kupotea.

Uamuzi huo unatokana na wanyama hao kuwa hatarini kutoweka kutokana na majangili kuwaua kwa ajili ya kupata pembe zao.

Akizungumza na MCL Digital leo Jumapili Juni 24, 2018 mwakilishi mkazi wa Shirika la Uhifadhi la Kimataifa la Frankfurt Zoological Society, Gerald Bigulube amesema mradi huo utatumia zaidi ya Sh253 milioni.

Amesema fedha hizo zimetolewa na Shirika la Uhifadhi la Friedkin Conservation Fund (FCF) na kuratibiwa na Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (Tawiri).

Bigulube amesema tayari utekelezaji wa mradi huo umeanza, kwamba mwaka 2017 faru 21 walifungwa vifaa maalum na mwaka 2018 wengine watafungwa vifaa vya kisasa zaidi kutumia mfumo wa LoRa.

“Lengo letu kama wahifadhi ni kuhakikisha faru waliopo nchini wanaongezeka zaidi sambamba na wanyama wengine ambao maisha yao yamekuwa hatarini wakiwepo tembo ambao nao tayari kuna miradi ya kuwafunga vifaa vya kisasa ili kuwafuatilia,” amesema.

Amesema katika kuhakikisha mradi huo unakuwa endelevu wameanza kuwapeleka kwenye mafunzo nchini Uholanzi wahifadhi ambao ndio watakuwa wakiratibu matumizi ya technolojia katika ulinzi na ufuatiliaji wa Faru.

"Hivi karibuni tutaanza kuwafunga vifaa Faru, zoezi ambalo litatumia teknolojia za hali ya juu, helkopta nna vifaa vingine vya kisasa kama ilivyokuwa mwaka jana,” amesema

Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, William Mwakilema amesema mpango huo unaoshirikisha Wizara ya Maliasili na Utalii na wadau wengine utasaidia ulinzi wa wanyamapori hao.

 

Mtafiti kiongozi wa Tawiri, Edward Kohi amesema ili kuimarishwa ulinzi wa faru, teknolojia mbalimbali zinatakiwa kutumika.

 

"Hii teknolojia ya kuwafunga vifaa maalum itawezesha kujulikana kila siku wapo wapi na hivyo ni rahisi kuwafuatilia na kuwapa ulinzi,” amesema.