Hakimu ajitoa kesi ya Lema, akidaiwa kuwa na urafiki na mkewe

Mbunge wa Jimbo la Arusha mjini, Godbless Lema

Muktasari:

  • Hakimu huyo ni wa pili kujitoa katika kesi hiyo, kwani Mei 29, Hakimu Mkazi wa Mkoa wa  Arusha, Desderi Kamugisha pia alijitoa kwa maelezo kuwa hawezi kusikiliza kesi zote nne zinazomkabili Lema  hivyo kuwaeleza mahakimu wengine watapangiwa kesi hiyo.
  • Leo (Alhamisi Julai 6) wakati kesi ikipangwa  kusomewa maelezo ya awali, Wakili wa Jamhuri katika kesi namba 441, Sabina Silayo aliwasilisha hoja katika mahakama hiyo kuwa Hakimu Kisinda ana urafiki na Neema.

Arusha. Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha, Patricia  Kisinda aliyekuwa anasikiliza  kesi ya uchochezi  inayomkabili Mbunge wa Jimbo la Arusha mjini, Godbless Lema dhidi ya Rais John Magufuli  amejitoa baada ya kuwekewa pingamizi na Jamhuri kuwa ana urafiki na mke wa Lema, Neema Lema.

Hakimu huyo ni wa pili kujitoa katika kesi hiyo, kwani Mei 29, Hakimu Mkazi wa Mkoa wa  Arusha, Desderi Kamugisha pia alijitoa kwa maelezo kuwa hawezi kusikiliza kesi zote nne zinazomkabili Lema  hivyo kuwaeleza mahakimu wengine watapangiwa kesi hiyo.

Leo (Alhamisi Julai 6) wakati kesi ikipangwa  kusomewa maelezo ya awali, Wakili wa Jamhuri katika kesi namba 441, Sabina Silayo aliwasilisha hoja katika mahakama hiyo kuwa Hakimu Kisinda ana urafiki na Neema.

Sabina alieleza mahakama kuwa ana ushahidi kuwa hakimu Kisinda ana urafiki wa karibu na mke wa Lema.

"Ombi la Jamhuri ni kuwa hatuna imani na wewe kuendelea na shauri hili na tunaomba ujiondoe kwa vile mke wa mshtakiwa ni rafiki wako wa karibu sana na ushahidi huo tunao na haina pingamizi," amesema Sabina.

Amesema Hakimu huyo kuendelea kusikiliza kesi hiyo kutaondoa imani kwa upande wa Jamhuri kwani huenda haki isitendeke na hivyo aliiomba mahakama ipange kesi hiyo kwa hakimu mwingine.

Baada ya hoja hiyo kuwasilishwa mbele ya wakili wa utetezi wa Lema, Sheck Mfinanga aliomba mahakama kutupa hoja hiyo kwani haina uzito kwa kuwa Watanzania wote ni ndugu na ni marafiki.

Wakili Mfinanga amesema kesi hiyo haina  urafiki hivyo kama mahakama iko kwa ajili ya kusimamaia sheria na haki iache hakimu huyo aendelee na kesi hiyo.

Hata hivyo, Wakili wa Serikali Sabina alijibu hoja hiyo kwa kuonyesha mashauri mbalimbali ambayo yalionyesha kuwa kuna kanuni na sheria za mahakama  kuwa endapo itabainika kuwa Jaji au Hakimu ana uhusiano wowote na mshtakiwa au mshtaka atatakiwa ajiondoe kusikiliza kesi hiyo.

Hata hivyo, kutokana na hoja hizo za pande mbili, Hakimu Patricia ametumia dakika 20 kufanya uamuzi mdogo juu ya hoja ya upande wa Jamhuri na amekubaliana ana hoja hiyo ya kujiondoa.

Hakimu Patricia amesema ameamua kujitoa ili kupisha haki itendeke lakini yeye si rafiki na mke wa Mbunge bali anamfahamu tu.

Hata hivyo, amesema rufaa juu ya uamuzi huo iko wazi na kwamba Agosti 2 mwaka huu  kesi hiyo itafikishwa mahakamani tena kwa ajili ya kupangiwa  hakimu mwingine kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali.

Kesi nyingine ya Lema

Kesi nyingine ya uchochezi  dhidi ya Magufuli, (namba 440)  inayomkabili Lema imeshindwa kuendelea kutokana na maombi ambayo hayakuwekwa wazi na wakili wa utetezi Sheck Mfinanga .

Akieleza mahakamani hapo, mbele ya Hakimu Mkazi, Devota Msofe, Mfinanga amesema ametumiwa ujumbe na mteja wake kuwa kesi hiyo haitaweza kuendelea mpaka pale mahakama kuu itakapojibu ombi la mteja wake.

Alisema ombi hilo limepelekwa mahakama kuu, hivyo wanasubiria majibu ya mahakama kuu ili kesi hiyo iweze kusomewa mashtaka ya awali.

Hata hivyo, jana Lema hakuwepo mahakamani na wakili wake, Mfinanga, aliomba udhuru  kwa ajili ya mbunge huyo kutoweza kufika mahakamani kutokana na kuugua.

Mfinaga aliwasilisha nakala za hati za matibabu ambako mbunge huyo anatibiwa na kueleza mbunge huyo wakati akiwa safarini kutoka Dodoma kuelekea Dar es Salaam alijisikia vibaya hali iliyosababisha ashindwe kufika mahakamani hapo.