IGP Sirro: Mchezo ndio kwanza umeanza

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Simon Sirro akionyesha bastola zilizokutwa kwenye gari iliyotumika kumteka Mohmed Dewji . Picha na Filbert Rweyemamu

Muktasari:

  • Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi ameonya kuwa hawatatulia kwa sasa na pia kuwataka wanasiasa kutoitumia mitandao kulichafua jeshi hilo.

Dar es Salaam. Mkuu wa Jeshi la Polisi, (IGP), Simoni Sirro ameeleza namna mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji alivyopatikana katika viwanja vya Gymkana usiku wa kuamkia jana huku akisema licha ya hatua hiyo, “Mchezo ndiyo kwanza umeanza.”

Aliwaambia waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika makao makuu ya Polisi jijini Dar es Salaam jana kuwa kazi iliyobaki ni kuwasaka ili kuwaonyesha kuwa Tanzania si mahali salama kwa wahalifu.

IGP Sirro alisema, “Unapoanza mbio lazima zifike mwisho, watakapokwenda na sisi tutakwenda, hatuwezi kuwaachia, tukiwaacha watajipanga upya.”

Kuhusu alivyopatikana, Kamanda Sirro alisema saa 7:30 usiku, gari lililombeba mfanyabiashara huyo bilionea, lilimshusha katika eneo hilo na wahusika walilitelekeza na kuondoka.

Hata hivyo, alisema kabla ya kuondoka, watekaji hao walijaribu kutaka kulichoma moto gari hilo.

“Kwa maelezo ya Mo, alimpata mlinzi mmoja akapiga simu kwa wazazi wake, baadaye polisi tukapata taarifa na kuwahi eneo la tukio.

“Kwenye lile la tukio tuliamua kuweka utepe na kuimarisha ulinzi ili watu wasiingie hadi asubuhi ya leo (jana) ili upekuzi ufanyike,” alisema.

Alisema upekuzi ulipofanywa na timu ya askari wanaohusika na matukio, walilibaini gari hilo Toyota Surf kuwa ndilo ile iliyotajwa na polisi juzi kuwa lilihusika siku alipochukuliwa ambako aliwataka wasamaria wema kutoa taarifa popote watakapoliona.

“Gari ni lilelile halina mashaka. Lakini ndani ya gari tumekuta silaha nne ambazo ni Ak47 moja yenye risasi 19 na bastola tatu zenye risasi 16,” alisema Sirro.

Alieleza kuwa baada ya Mo kuhojiwa, alisema watekaji walikuwa na wasiwasi na walichokuwa wakikihitaji kwake ni fedha na yeye alichukua jukumu la kuwapa namba ya simu ya baba yake.

“Aliwaambia namba hii mkimpigia baba mtazungumza naye. Watekaji hawa walikuwa na wasiwasi, hawakutaka kuzungumza na baba yake Mo Dewji (Gullam Hussein) na lugha waliyokuwa wakizungumza ni Kiingereza na Kiswahili cha kubahatisha,” alisema.

Hata hivyo, mapema asubuhi, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alikaririwa akisema “Kwa mujibu wa maelezo ya Mo Dewji, watekaji walisikika wakizungumza kwa lafudhi ya lugha moja ya Afrika Kusini.” Sirro alisema upelelezi uko vizuri na aliwashukuru wakazi wa Dar es Salaam kwa ushirikiano wanaouonyesha ili kuhakikisha wahusika wanapatikana.

“Nawaomba sana… waendelee kutupa taarifa kwa sababu mchezo ndiyo kwanza umeanza . Tunataka kuwaonyesha Tanzania si mahali salama kwa mtu anayetaka kufanya uhalifu.

“Nafikiri lile tangazo nililolitoa na picha ilivyoonekana wakawa na wasiwasi kuwa wangekamatwa na kweli wangekamatwa, maana hawakuwa na namna, maana gari linajulikana, dereva na mmliki wake pia, kilichobakia ni kuchunguza tu wapo wapi,” alisema Sirro.

Kikundi cha watu

Katika hatua nyingine, IGP Sirro alisema kuna kikundi cha watu kinapenda kuingilia vyombo vya ulinzi na usalama wakati vinapokuwa vinafanya upelelezi kuhusu jambo fulani.

“Wanaingilia sana tena kwa kufundisha majeshi yafanye vipi kazi . Inanitia mashaka sana, niwaomba wasilazimishe kujenga uadui na majeshi yetu na polisi.

“Narudia, wajitahidi sana kushirikiana na majeshi yao hasa polisi, wasilazimishe kujenga uadui na majeshi yetu, najiuliza unapojenga uadui na majeshi yako unatumwa na nani, ili iwe nini na kwa faida ya nani?” alihoji Sirro.

Alisema yeye si mwanasiasa, anatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa maadili na kwamba, hajawahi kuzungumzia masuala ya siasa hata mara moja.

Alidai kuwa watu hao, kwa maslahi yao, wanataka Tanzania isikalike na kusisitiza kuwa kamwe hawatafanikiwa kwa sababu nchi ipo imara.

“Hebu waandishi wa habari fikirieni siku tisa askari wanazunguka, hawalali wanaingia apartment moja hadi nyingine wanahangaika, lakini mtu mmoja amelala na mke wake kwenye kiyoyozi kwa kutumia mitandao ya kijamii, anachallenge kazi za polisi.

“Anafundisha kazi zote za polisi. Nasema ukiamua kujenga uadui na majeshi yetu, nikwambie ukweli hautakuwa salama, tutajua kuna mtu anakutuma.

“Wewe hauna thamani kama Taifa hili na wajue wanaweza kusema hayo kwa sababu babu zetu walilinda usalama wa nchi hii, ndiyo maana hadi leo tupo na usalama,” alisema Sirro.

Aliwataka kuacha kutumika na watu wa nje ili nchi isitawalike.