‘Kivuli’ cha Dk Tulia Mbeya kuondoka na madiwani watatu wa Chadema

Muktasari:

  • Uamuzi huo wa Chadema umekuja ikiwa imepita wiki moja tangu Dk Tulia kutangaza ‘kiaina’ kuwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 atagombea ubunge, licha ya kutoweka wazi jimbo atakalowania.

Dar/ mikoani. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoani Mbeya kimependekeza madiwani wake watatu kufukuzwa uanachama kwa utovu wa nidhamu na kukiuka taratibu za chama, wakidaiwa kuhudhuria sherehe iliyoandaliwa na naibu spika, Dk Tulia Ackson.

Uamuzi huo wa Chadema umekuja ikiwa imepita wiki moja tangu Dk Tulia kutangaza ‘kiaina’ kuwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 atagombea ubunge, licha ya kutoweka wazi jimbo atakalowania.

Siku za hivi karibuni, Dk Tulia ameonekana akishiriki shughuli mbalimbali za kijamii mkoani humo, ikiwamo kuandaa mashindano ya mbio ya Mbeya Tulia Marathon, huku akitajwa kuwa anajipanga kuwania ubunge katika moja ya majimbo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mbeya jana, mwenyekiti wa Chadema Mbeya Mjini, Obadia Mwaipalu aliwataja madiwani na kata zao katika mabano kuwa ni Geofrey Kajigili (Sisimba), Hamphrey Ngalawa (Iwambi) na Newton Mwatujobe (Manga).

Uongozi wa Chadema mkoani Mbeya uliketi katika kikao cha dharura juzi na kukubaliana kuandika barua ya mapendekezo kwa uongozi wa chama hicho Kanda ya Nyanda ya Nyasa kuwa wavuliwe uanachama jambo litakalowafanya kupoteza sifa za kuwa madiwani.

Katika ufafanuzi wake, Mwaipalu alisema chama hicho kimeamua kuwachukulia hatua za kinidhamu madiwani hao baada ya kuonyesha utovu wa nidhamu uliokithiri.

“Walikaidi amri ya chama ya kutokwenda Dodoma kuhudhuria shughuli ambayo Dk Tulia alitoa mwaliko. Ilikuwa Aprili, mwaka huu na walishiriki shughuli hiyo pamoja na Dk Tulia,” alisema.

“Tuliwaandikia barua Mei 25 na kuwafikia Mei 28, tukiwataka wazijibu ndani ya siku 14 kwa nini wasichukuliwe hatua za kinidhamu kwa kukaidi amri ya chama. Ila mpaka leo hawajajibu barua hizo, jambo linaloashiria kuwa wamekaidi maagizo ya chama. Huu ni utovu wa nidhamu.”

Alisema baada ya kukaa vikao wamependekeza kufukuzwa uanachama kwa kuwa uongozi wa Chadema mjini humo hauna uwezo wa kumfuta uanachama diwani yeyote.

“Tumepeleka mapendekezo yetu katika ofisi ya kanda ambayo ndio wenye mamlaka ya kuchukua hatua za kinidhamu zaidi. Hivyo tunaamini ofisi ya kanda ina watu makini na itayafanyia kazi mapendekezo yetu,” alisema Mwaipalu.

Alisema madiwani hao wamekuwa na tabia ya kukichafua chama hicho akimtolea mfano Kajigili kuwa amekuwa akishiriki shughuli mbalimbali za Dk Tulia mjini Mbeya na kuzungumza mambo yasiyoendana na msingi wa Chadema.

“Kajigili ameanza kumpigia kampeni Dk Tulia hadharani kabisa huku akitamka maneno ya kejeli, dharau na dhihaka kwa viongozi wake wa chama kitu ambacho hakihitaji uwe na shahada ya uzamivu kujua msingi wake ni nini,” alisema.

Mwananchi liliwatafuta madiwani hao kuzungumzia tuhuma hizo, lakini ni Kajigili pekee ndiye aliyetoa ushirikiano akieleza kuwa hawezi kujibu jambo lolote hadi atakapopata barua ya uamuzi utakaochukuliwa dhidi yake, huku akipangua tuhuma dhidi yake.

Akizungumzia mwaliko wa kwenda mjini Dodoma, alisema ulikuwa ni wa halmashauri ya jiji na madiwani, na kwamba hakupata taarifa zozote kutoka Chadema akizuiwa kushiriki.

“Kuhusu mwaliko wa hivi karibuni hapa Mbeya, sikwenda kwa mwaliko wa Dk Tulia nilikwenda kwa mwaliko wa diwani mwenzangu kwa kuwa ile kata diwani wake ni wa Chadema. Na sioni kama ni dhambi kumpongeza mtu yeyote pale anapofanya vizuri,” alisema Kajigili.

“Kusema nilitumia maneno ya kejeli, dharau na dhihaka kwa viongozi kama Mbilinyi (Joseph-mbunge wa Mbeya Mjini-Chadema) siwezi kuthibitisha kwani sina kipimo cha kupima kama maneno yale yalikuwa ni kejeli, dhihaka na dharau.”

Katibu wa Chadema Kanda ya Nyasa, Emmanuel Masonga, jana alilieleza Mwananchi kuwa amepokea mapendekezo ya viongozi wa chama hicho mjini Mbeya kuhusu madiwani hao na kusema kuwa suala hilo litajadiliwa.

“Kwa sasa nipo safarini ila jambo hili tutalifanyia kazi na tutazingatia hoja za pande zote mbili ili kuweza kutenda haki kwa wote kwa kuwa jambo hili ni la kisheria pia,” alisema Masonga.

NEC yateua madiwani

Wakati kampeni za ubunge Jimbo la Buyungu na udiwani katika kata 77 zikiendelea, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeteua madiwani wanane wa viti maalumu kujaza nafasi zilizoachwa wazi.

Kati ya madiwani hao, sita ni wa CCM na wawili wa Chadema.

Taarifa iliyotolewa na mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage ilieleza jana kuwa, uteuzi huo umefanyika katika kikao cha tume hiyo kilichofanyika Julai 19.

Alisema walioteuliwa ni Ajira Kalinga (CCM-Songea), Mary Mbilinyi (CCM-Makete) na Zainab Mabrouk (CCM-Kongwa).

Wengine ni Restuta Gardian (CCM-Muleba), Siglinda Ngwega (CCM-Morogoro), Zena Luzwilo (CCM-mji Kahama), Neema Massawe (Chadema-Monduli) na Teodola Kalungwana (Chadema-Iringa).

“Uteuzi huu umefanyika baada ya kupokea taarifa kutoka kwa waziri mwenye dhamana ya serikali za mitaa kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za mitaa,” alisema Jaji Kaijage.

Aliongeza kuwa nafasi hizo zimejazwa kutokana na waliokuwa madiwani wa viti maalumu kufariki dunia na kujiuzulu.