Kiwanda kinaweza kuzalisha kifaa kimoja cha bidhaa kubwa duniani

Mkurugenzi Mtendaji wa  Taasisi ya Utafiti Repoa, Dk Donald Mmari (kushoto) wakiwa na  Mkurugenzi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) Godfrey Simbeye wakiingia kwenye ukumbi wakati wa kongamano la Jukwaa la Fikra kuelekea uchumi wa Viwanda.Picha na Anthon Siame

Muktasari:

Mkurugenzi wa Repoa, Dk Donald Mmari anasema viwanda duniani vimejikita katika mnyororo wa thamani ambako bidhaa zenye thamani kubwa huzalishwa na kampuni zaidi ya moja na mfano ni ndege ya Dreamliner iliyotengenezwa na kampuni zaidi ya 19 kutoka nchi saba tofauti.

Wakati kila mdau wa uchumi nchini akiangalia namna ya kushiriki kwenye ujenzi wa uchumi wa viwanda, wadau wanasema vinavyohitajika ni vile vitakavyojikita kuongeza thamani.

Maoni hayo yanafafanuliwa zaidi na ukweli kwamba bidhaa nyingi duniani huzalishwa kutokana na mchango wa kampuni nyingi zilizoshiriki kuikamilisha kutokana na changamoto za kiwanda kimoja kukamilisha kila kitu.

Mkurugenzi mtendaji wa Repoa, Dk Donald Mmari anasema uzalishaji wa viwandani duniani kwa sasa umejielekeza kwenye mnyororo wa thamani kwani bidhaa zenye thamani kubwa huzalishwa na zaidi ya kampuni moja.

“Ndege aina ya Dreamliner imetengenezwa na kampuni zaidi ya 19 kutoka nchi saba. Kuna kampuni ya Switzerland imetengeneza mlango tu. Kwa hiyo tunaweza kuanza kujenga viwanda kwa kujiingiza katika minyororo ya thamani,” anasema Dk Mmari.

Anasema hakuna sababu ya kufikiria uwekezaji wa viwanda kwa utengenezaji wa bidhaa kuanzia hatua ya kwanza hadi kukamilika kwake kwa ajili ya matumizi ya mteja wa mwisho badala yake kunaweza kuwa na ushirikiano wa kibiashara utakaotekelezwa kwa mikataba makini.

Kinachohitajika, anasema ni kuangalia eneo muhimu katika mnyororo wa utengenezaji wa bidhaa zilizopo katika soko kubwa duniani na kulifanyia kazi kwa umakini utakaokidhi viwango.

“Yapo maeneo mengi. Kwa mfano, hizi simu tunazotumia, zinatengenezwa kwa madini ya cobalt. Madini hayo yanatumika kutengenezea simu za mkononi aina ya Apple,” anafafanua Dk Mmari.

Kufanikisha hilo, Dk Mmari anaishauri Serikali kujiandaa kwa matumizi bora ya rasilimali zilizopo nchini kuingia katika mnyororo wa utengenezaji wa vifaa vya simu au bidhaa nyingine zenye uhitaji mkubwa duniani kutokana na madini na malighafi nyingine zilizopo nchini badala ya kukaribisha wawekezaji wanaozivuna na kwenda kuziongezea thamani nje ya nchi.

“Wakija wawekezaji tuwaeleze tunahitaji kutengeneza bidhaa si kusafirisha malighafi. Hii itasaidia kuingia kwenye mazingira ya uchumi wa dunia na watafiti tupo tayari kuendelea kufanya utafiti ili kuishauri Serikali na wadau wengine jinsi ya kufanikisha sera yetu,” anasema Dk Mmari.

Maoni ya Dk Mmari yanafanana na ya mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Haji Semboja anayesema ni jambo linalowezekana kutekelezwa nchini kutokana na upatikanaji wa rasilimali tofauti.

“Mnyororo wa thamani maana yake ni kwamba, katika kitu kimoja kilichomalizika, ni matokeo ya kazi nyingi zilizounganishwa kwa mpangilio kwa ushiriki wa watu wengi. Sasa, tukiamua tunaweza kukaa mwanzoni, katikati au mwishoni,” anasema.

Anatolea mfano gari aina ya Toyota lenye sehemu kati ya 275 na 325 tofauti zinazolifanya litembee kwa ufanisi unaotakiwa kwamba wajasiriamali nchini wanaweza kuchagua kutengeneza kifaa kimoja kati ya hivyo kuiruhusu kampuni hiyo kuendelea kutengeneza bidhaa zake.

Anasema kuna changamoto chache za kuweza kufanikisha hili kwani ni lazima uwe na soko la uhakika kwa sababu zipo kampuni au mataifa yanataka uendelee kuwa soko la bidhaa zao au kituo cha soko kwa majirani zako. Kenya kwa mfano, anasema wanautumia mfumo huu kwa muda mrefu sana.

“Ndiyo maana sera ya uchumi Kenya inakwenda kwa kasi kwa sababu wanalo soko. Kwa sasa wanaunganisha magari tofauti. Kampuni za China, Japan hata Ujerumani zina matawi yake Kenya,” anasema Profesa Semboja.

Baadhi ya kampuni, anasema huingia Kenya si kwa lengo la kufanya biashara na soko la nchi hiyo bali kuifanya kuwa kituo cha soko la Afika Mashariki.

Ili kufanikiwa katika hatua hiyo kama ilivyofanya Kenya, anasema yapo masharti yanayochagizwa na siasa ya nchi katika masuala ya viwanda na mtazamo wake kwa sheria, utaratibu na uwezo wa taasisi za fedha.

Anasema Kenya imefanikiwa kuimarisha mifumo yake na taasisi zinaunga mkono kuhakikisha shughuli za viwanda zinafanyika bila kuathiriwa na siasa za nchi.

“Hakuna mtu atakayekaa na kuanza kuropoka kuhusu viwanda vya Kenya, hakuna jukwaa hilo. Wanasiasa watagombana kwenye mambo yao tu, Wakenya wana taasisi zinazofanya kazi ya kusaidia utekelezaji wa sera zao,” anasema.

Mwenyekiti wa Shirikisho la wenye Viwanda Tanzania (CTI), Subhash Patel anasema licha ya changamoto ya kupata mtaji, nyingine ni mtazamo potofu dhidi ya wafanyabiashara.

Anasema baadhi ya viongozi wa Serikali hawana imani na wafanyabiashara na mara nyingi huwaona wanaopenda kujinufaisha kwa njia zisizo halali hasa kwa kuwanyonya wananchi masikini.

“Tabia ya kuona kila mtu ni tapeli, ni mtazamo unaopaswa kuondolewa ili kila mmoja awe na nafasi ya kushiriki kujenga uchumi bila kutiliwa mashaka,” anasema Patel.

Maoni ya wadau hawa yalitolewa kwenye mjadala uliofanyika Oktoba 4 katika uumbi wa Kisenga uliopo jengo la LAPF lililopo Makumbusho jijini Dar es Salaam.

Mjadala huo ulikuwa ni wa pili ukiandaliwa na jukwaa la fikra la Mwananchi linaloratibiwa na kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kwa kushirikiana na kituo cha runinga na ITV na Radio One.

Katika mjadala huo uliofanyika kuanzia saa 3:00 usiku mpaka 5:00 uliwahusisha watafiti, wafanyabiashara, watunga sera, taasisi za fedha na watendaji wa Srikali pamoja na wananchi wa kawaida wakiwamo wanafunzi wa vyuo vikuu kupata maoni yao juu ya utekelezaji wa sera hiyo.

Michango ya mjadala huo wa pili baada ya ule wa awali uliojadili magonjwa yasiyoambukiza, ilijikita kwenye utekelezaji wa sera ya uchumi wa viwanda.