Breaking News
Tuesday, September 11, 2018

Kukosekana kwa sheria, sera kunavyochangia ajali za bodaboda

 

By Herieth Makwetta, Mwananchi hmakweta@mwananchi.co.tz

Wakati taifa lilikiendelea kukumbuka na kuomboleza vifo vya watu 15 vilivyokana na ajali ambayo pia ilisababisha majeruhi 15 mkoani Mbeya, Ijumaa iliyopita, kila mmoja anapaswa kuongeza umakini katika matumizi ya barabara.

Ingawa umakini zaidi umekuwa ukiwekwa katika kudhibiti ajali zitokanazo na magari, lakini ni muhimu pia kuhakikisha vyombo vingine vya moto barabarani hususani pikipiki vinaendelea kutazamwa kwa jicho la karibu.

Kwa ajali niliyoishudia Tabata, Dar es Salaam ambayo ni moja kati ya nyingi zinazogharimu maisha ya watu, kusababisha ulemavu na kupunguza nguvu kazi, ipo haja ya kuongeza nguvu kukabiliana nazo.

Ilikuwa saa moja jioni nashuka kwenye daladala eneo la Tabata Mataa, Barabara ya Mandela, Dar es Salaam, ninapovuka kuelekea Tabata Hai, nashtushwa na kishindo nyuma yangu, ninapogeuka nakutana na ajali ya pikipiki maarufu bodaboda.

Dereva wa bodaboda anafanikiwa kukimbia, lakini abiria amelaliwa na chombo hicho, baada ya kuokolewa inagundulika ameumia kichwani, hakuvaa kofia ngumu ‘helmet’. Ajali hiyo imetokea mbele ya Askari wa Usalama Barabarani (Trafiki) aliyekuwa akiongoza magari, lakini mwendesha pikipiki alipuuza amri ya kumtaka asimame.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), ajali za barabarani zinaua watu milioni 1.23 kila mwaka duniani. Asilimia 90 zikitokea katika nchi zinazoendelea Tanzania ikiwa ni mojawapo.

Wasemavyo Bodaboda

Mwenyekiti wa Chama cha Waendesha Bajaji na Bodaboda Wilaya ya Kinondoni, Almano Mdede, anasema ongezeko la ajali za barabani linatokana na trafiki kutozingatia usalama wa waendesha bodaboda.

Anawataja askari kanzu kuwa chanzo cha kusababisha bodaboda kukosa utulivu wawapo barabarani.

Anawataja askari wasio na sare au wale wanaojulikana kwa jina la Tigo, kwamba huwatumia watu wasio na ujuzi ambao hawahusiki na si waaminifu kukamata pikipiki au bajaji kwenye kona mbalimbali jijini humo na kuchukua fedha.

Anayataja maeneo ambayo askari hao hupendelea kukaa ikiwemo kwenye taa za kuongozea magari za Ubungo, Mwenge, Bamaga na Morocco ambako anadai husababisha bodaboda kutozingatia suala la kusimama na kusubiri kuruhusiwa kwa utaratibu.

Mdede anahoji kwa nini askari hao wasitumie ukamataji sahihi usio hatarishi?.

Hata hivyo, anasema mfumo mpya wa kufunga vifaa vya kufuatilia mwenendo (GPS) ambacho kitafungwa kwenye pikipiki na kufuatiliwa kupitia mtandao utakuwa mwarobaini kwa madereva wasiofuata sheria.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Waendesha Pikipiki Wilaya ya Ilala, Omary Sudi Kombo, anasema kwa mtazamo uliopo wanachama wake wameshaelekezwa lazima wafuate utaratibu wa kuvuka taa hizo kwa ruhusa maalumu, lakini anadai walio wengi wanashindwa kutekeleza kutokana na askari kanzu.

“Hili linasababisha ajali nyingi…wanachama wetu wengi tumewazika na wengine wamekatwa miguu. Utakuta gari zimesimama wao wanapita bahati wakivuka salama, lakini wakati mwingine wanakutana uso kwa uso na magari,”anasema.

Anasema wanachokifanya wao (viongozi wa bodaboda), ni kutoa elimu ya kutosha.

Kombo anasisitiza kuwa tatizo kubwa kwa vijana wanaoendesha bodaboda ni mazingira ya polisi jamii kuwafanya wasijiamini kwa kuhofia kukamatwa na wakati wowote wanaweza kufanywa mtaji, hivyo inawalazimu kila wanapofika kwenye taa za kuongozea magari wavuke bila umakini.

Hatua zinazochukuliwa

Mwenyekiti wa Umoja wa Waendesha Pikipiki Wilaya ya Temeke, Said Kagomba anasema hadi sasa wameshatoa mafunzo kwa madereva 6,230 kuhusu usalama barabarani, kuzitambua sheria, kutochukua sheria mkononi.

Anasema katika mkoa wa kipolisi Temeke kwa mwaka 2015 hadi 2017 ajali zilikuwa chache kutokana na ushirikiano baina yao na RTO, lakini tangu walivyobadilishwa mwishoni mwa mwaka jana, hali kwao imekuwa mbaya.

“Dereva wa pikipiki ambaye hajapata mafunzo, hana leseni au kutojiamini kumkimbia trafiki ni jambo la kawaida na trafiki kumzingatia mtu wa pikipiki anashindwa kwa kuwa ukamataji wake si rahisi ni chombo kinachoweza kupenya tofauti na gari ambalo kwa kutumia namba wanalikamata,” anasema Kagomba na kuongeza:

“Tatizo kubwa ni kutoshirikishwa. Tunaliomba Jeshi la Polisi litushirikishe, baadhi ya polisi walitumia njia ya ulinzi shirikishi kukamata wavunja sharia. Miongoni mwa changamoto ni pale bodaboda anapokuwa sahihi kisheria lakini anakamatwa na pikipiki inawekwa chini ya kibanda chao kabla ya kubebwa kwenye lori na kupelekwa polisi”.

Anadai pindi wanapokamatwa polisi hao hawataki kuwakagua bali huwanyang’anya bodaboda na kuzipandisha kwenye lori bila kuzingatia usalama wake, mpaka zinapofika kituoni taa inaweza kuchomoka na hapo sasa hukutwa na makosa mawili mpaka matatu, “hatuendi sawa baina ya mwendesha pikipiki na polisi, napenda utaratibu wao, lakini askari wa chini wanafanya sivyo, ndiyo maana wakikutana bodaboda na askari wanakuwa maadui.”

Hata hivyo, Kagomba anasema viongozi wa juu wa Jeshi la Polisi, wamekuwa wakitoa ushirikiano mkubwa ikilinganishwa na walioko chini ambao si waadilifu kama maazimio ya wakubwa wao yanavyolenga.

Anasema lazima sheria ziwekwe sawa ili polisi na mwendesha pikipiki wawe marafiki.

“Ikumbukwe hii ni ajira kama angeibeba Rais Dk. John Magufuli kwenye pikipiki kuna fedha nyingi zinapotea, Temeke pikipiki 25,000 kila moja ikilipa Sh 22,000 unapata Sh 4.7 bilioni, hiyo fedha itaingia serikalini wanashindwa kutuita tukae pamoja kuyapanga haya,” anasema.

Ukubwa wa tatizo

Kwa mujibu wa Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (MOI), idadi ya majeruhi wanaofika kutibiwa katika kitengo cha dharura baada ya kupata ajali imeongezeka hadi kufikia wastani wa watu 30 kwa siku.

Daktari bingwa wa upasuaji wa Mifupa na Magonjwa ya Ajali Moi, Dk Kennedy Nchimbi anasema kwa siku chache zilizopita kumekuwapo na ongezeko kubwa.

“Ukiangalia kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita, Aprili tulipokea wagonjwa 650, Mei 435 na Juni tulipofunga mwaka wa fedha wa Serikali tuliwatibu 693. Ni ongezeko kubwa ukilinganisha na miezi iliyopita na ni wastani wa wagonjwa 17 mpaka 30 kwa siku,” anasema Dk Nchimbi.

Anasema idadi ya majeruhi kwa mwaka 2017/18 iliongezeka hadi kufikia 8,283 kutoka majeruhi 6,669 waliopokelewa mwaka 2016/17.

Dk Nchimbi anasema idadi ya majeruhi waliowapokea Julai mwaka huu iliongezeka hali iliyowalazimu kufunga meza za dharura.

“Kila siku tuna meza ya dharura, lakini wanapokuwa wengi tunaona tutachukua muda mrefu, kwa hiyo inabidi tuwabadilishe akishuka mtu, anapandishwa mwingine,” anasema.

“Kuna nyakati wagonjwa 12 wanakuwa katika mlango wa chumba cha upasuaji wa dharura na Moi tuna timu za madaktari kuanzia anayekuona, atakayekuandaa na atakayekwenda kukufanyia upasuaji. Inabidi hizi timu ziongezwe na meza zaidi zifunguliwe.”

Anasema wagonjwa wengi wanaumia maeneo mchanganyiko sehemu yoyote ambayo itagongwa kwa muda huo, kwa kuwa pikipiki ni chombo kilicho wazi hivyo ni rahisi kuumia mguu, kiuno, kifua na maeneo mengineyo ya mwili na wale wanaoumia zaidi kichwani hutokana na kutovaa kofia ngumu (helmet).

“Takwimu za helmet MOI tulizitoa…asilimia karibu 40 ya wagonjwa wanaofika hapa ripoti zinaonyesha hawakuwa wamevaa helmet, mwingine alilifunga nyuma au hana kabisa, wakati mwingine zinavaliwa lakini sio kwa usahihi, wapo wanaokwepa kuzivaa kutokana na staili za nywele,” anasema.

Anasema changamoto kubwa ni wengi kufika hospitalini hapo wakiwa hawana chochote, hivyo katika kuchangia matibabu inakuwa vigumu, anapofanyiwa matibabu akipona anasema hana ndugu. Walio na bima ya afya ni wachache.

Mwenyekiti wa Umoja wa Waendesha Bodaboda Tabata, (Chabowik) Rashid Mwanga anasema kikundi chao kina wanachama 80, pamoja na mambo mengine husaidiana katika matatizo mbalimbali. Wamekuwa wakichangia kiasi cha Sh500 kwa siku na malengo yao ni kujiunga katika mfuko wa bima ili kupata huduma za matibabu.

Ofisa Uhusiano wa Moi, Patrick Mvungi anasema licha ya ongezeko hilo, taasisi hiyo inaelemewa na gharama kubwa za kuwahudumia majeruhi hao kwa kuwa wengi wao hawana ndugu.

Anasema majeruhi wa bodaboda matibabu yao huchukua muda mrefu bila usaidizi wa ndugu, lakini baadhi yao hata marafiki ambao hujitokeza baadaye hupotea.

Kikosi cha usalama barabarani

Mwanasheria wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (ASP), Deus Sokoni anasema Sheria ya usalama barabarani iliyotungwa na Bunge mwaka 1973 inapaswa kufuatwa na kila mtumiaji barabara bila kujali ni dereva wa gari, bajaji, pikipiki, mwendesha guta au mtembea kwa miguu.

Anasema sheria inatambua kundi la kwanza ni waenda kwa miguu ambalo pia lina makundi mawili muhimu ambayo ni wazee na watoto.

Ni makundi yanayoangaliwa kwa namna ya pekee, kwani wapo kwenye hatari kubwa ya kugongwa wakajeruhiwa au hata kupoteza maisha. Hata hivyo wanapaswa kuijua sheria ya usalama barabarani ambayo ndiyo inayowatawala wanapotumia barabara.

“Pikipiki za matairi matatu na mawili, hawa wote ni madereva wa vyombo vya moto na wanapaswa kusoma udereva waelewe, watahiniwe, wafuzu ndipo wapewe leseni.

Takwimu

ASP Sokoni anasema kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu, ajali za pikipiki Januari hadi Desemba 2016 zilikuwa 2,653, vifo vikiwa 990 na majeruhi 1997.

Mwaka 2017 ajali zilikuwa 1,584 vifo 793 na majeruhi 1224, “Mwaka 2017 zilipungua kwa tofauti ya ajali 1,069 na vifo 227 sawa na asilimia 22.9. Huku kukiwa na upungufu wa majeruhi 773”.

Sera inasemaje?

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu, James Kajugusi anasema sera zipo, lakini pamoja na sheria zake zinasimamiwa na Wizara ya Mambo ya Ndani.

Anasema sera ya maendeleo kwa vijana Tanzania ya mwaka 2007, inasema Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi itaandaa mazingira mazuri ya kutengenezaji ajira kwa vijana.

-->