Kutekwa ‘Mo’ kwakwamisha Mambosasa kuhudhuria mafunzo ya kipolisi Dodoma

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa

Muktasari:

  • Taasisi ya Uongozi nchini imeendesha mafunzo ya uongozi kwa makamanda wa polisi nchini jijini Dodoma lakini makamanda wawili wa Kanda Maalumu ya Polisi ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa na Mkoa wa Kinondoni, Jumanne Murilo  wameshindwa kuhudhuria kutokana na kuwa na kazi maalumu.

Dodoma. Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa na wa mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Jumanne Murilo wameshindwa kuhudhuria mafunzo ya uongozi ya makamanda wa polisi nchini kwa kile kilichoelezwa wana kazi maalumu.

Jijini Dar es Saalam kuna mtikisiko  baada ya mfanyabiashara maarufu, Mohamed Dewji ‘Mo’ kutekwa alfajiri ya Alhamisi Oktoba 11, 2018 katika Hoteli ya Colosseum, iliyopo Oysterbay jijini humo.

Akizungumza katika mafunzo yaliyoandaliwa na Taasisi ya Uongozi Nchini leo Oktoba 15, 2018 jijini Dodoma, Kamishna wa Utawala na Menejimenti ya Raslimali Watu wa Jeshi la Polisi, Abert Nyamuhanga  amesema jeshi hilo liko tayari kwa mafunzo hayo kwa kiwango cha juu na kuhudhuria wakati wote.

“Ndugu makamanda huwa kuna mazoea kuwa tunapokuja katika mafunzo tunasema kwamba ni sehemu ya kupumzika, maelekezo ya makao makuu ya polisi si wakati wa kupumzika ni wakati wa kufanya kazi na kuzingatia kilichotuleta hapa na ndio maelekezo ya afande IGP (Simon Sirro),”amesema.

Amesema Sirro ameagiza makamanda wote wafike isipokuwa wale ambao wana kazi maalumu na kwamba  hata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi ametakiwa kuhudhuria mafunzo hayo baada ya kumalizika kwa uchaguzi.

“Na afande (Sirro) amesema aje uchaguzi umekwisha na hali ni shwari. Wale wa Dar es Salaam mnafahamu sababu iliyosababisha wasije, Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam na wa Kinondoni sote tunafahamu na ndiyo maana wamebaki pale,” amesema.

Mwisho