Laac yakataa taarifa ya mradi Dodoma

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge Hesabu za serikali za mitaa(Laac), Vedasto Ngombale amesema kilichobainika kwenye mradi huo umetekelezwa kinyume na mkataba unavyoainisha kutokana na wananchi kutotekeleza majukumu yao yaliyoanishwa kwenye mkataba.

Muktasari:

  • Mradi huo ambao umegharimu zaidi ya Sh 800 milioni, umeonyesha kuwa chini ya kiwango kulinganisha na thamani halisi ya fedha zilizotumika.
  • Kamati hiyo inafanya ziara ndani ya manispaa hiyo lengo likiwa kukagua miradi mbalimbali kutokana na hoja ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG).
  • Wabunge walishangazwa mradi huo kuchukua muda mrefu wakati ulitakiwa kukamilika ndani ya miezi nane lakini umechukua miaka sita bila kukamilika.

Dodoma. Kamati ya Bunge Hesabu za serikali za mitaa(Laac),  imekataa taarifa ya Manispaa ya Dodoma kuhusu mradi wa umwagiliaji kwa njia ya matone katika Kijiji cha Gawaye kwamba haulingani na thamani halisi ya mradi.

Mradi huo ambao umegharimu zaidi ya Sh 800 milioni, umeonyesha kuwa chini ya kiwango kulinganisha na thamani halisi ya fedha zilizotumika.

Kamati hiyo inafanya ziara ndani ya manispaa hiyo lengo likiwa kukagua miradi mbalimbali kutokana na hoja ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG).

Wabunge walishangazwa mradi huo kuchukua muda mrefu wakati ulitakiwa kukamilika ndani ya miezi nane lakini umechukua miaka sita bila kukamilika.

Hata hivyo, Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema),  alihoji zaidi ya Sh 190 milioni kutumika kununua mbolea ya samadi kwa ajili ya kupanda miche ya zabibu wakati mbolea hiyo inapatikana kwenye maeneo hayo.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Vedasto Ngombale alisema kilichobainika kwenye mradi huo umetekelezwa kinyume na mkataba unavyoainisha kutokana na wananchi kutotekeleza majukumu yao yaliyoanishwa kwenye mkataba.

Akijibu hoja za wajumbe, ofisa kilimo wa manispaa hiyo, George Mhina alisema walifikia maamuzi ya kukikopesha chama hicho fedha za kununulia mbolea na miche kwa kuwa bila kufanya hivyo wangemkwamisha mkandarasi kutekeleza mradi huo.

Mhina alisema uzalishaji kwa sasa unafanyika kwenye hekari 36 kati ya 100 za mradi huo.