‘Licha ya ushuru kupanda, bei ya sukari ni nafuu’

Muktasari:

Kauli hiyo imetolewa leo na mwenyekiti wa Mfuko wa Maendeleo ya Sukari

Morogoro. Mwenyekiti wa Mfuko wa Maendeleo ya Sukari nchini, Deo Lyatto amesema licha ya kupanda kwa ushuru wa sukari kutoka asilimia 25 hadi 35, bei ya bidhaa hiyo inaendelea kuwa nafuu ikilinganishwa na nchi jirani.

 

Lyato ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Juni 21, 2018 mjini Morogoro katika mkutano wa nane wa wadau wa sukari ulioandaliwa na mfuko huo kwa kushirikiana na Bodi ya Sukari.

 

Amewahakikishia wananchi kuhusu ubora wa sukari inayozalishwa nchini na kubainisha kuwa kuna mamlaka zinazoithibitisha ikiwemo Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA).

 

Naye mwenyekiti wa Muungano wa Vyama vya Wakulima wa Miwa (Tasga), Dk George Mlingwa amesema kama Serikali haitachukua hatua za kudhibiti uingizwaji wa sukari kutoka nje, soko la bidhaa hiyo nchini litakufa.

 

Amebainisha kuwa viwanda vya sukari vinavyoanzishwa hivi sasa vinaweza vikashindwa kukua na kujiendesha endapo sukari ya nje itaingizwa na kuuzwa kwa bei ya chini.