Lissu aaga TLS, Jaji Kiongozi atoa neno

Wajumbe wa mkutano Mkuu wa mwaka wa chama cha Wanasheria wa Tanganyika(TLS) wakifuatilia  mada zilizokuwa zikiwasilishwa wakati wa mkutano huo uliofanyika jijini Arusha jana. Picha na Filbert Rweyemamu

Muktasari:

  • Jaji Wambali akifungua mkutano mkuu wa TLS jana, alisema rushwa inawanyima haki wananchi. Aliwataka wanasheria kujitathmini kama malengo ya kuanzishwa taasisi hiyo yanaakisi shughuli zao sasa kulinganisha na idadi kubwa iliyopo ya wanasheria.

Arusha/Dar. Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Tundu Lissu anayemaliza muda wake amewaaga wanachama wa chama hicho huku Jaji Kiongozi, Ferdinand Wambali akieleza kuwa wanafanya kila linalowezekana kukomesha rushwa kwenye mfumo wa sheria.

Jaji Wambali akifungua mkutano mkuu wa TLS jana, alisema rushwa inawanyima haki wananchi. Aliwataka wanasheria kujitathmini kama malengo ya kuanzishwa taasisi hiyo yanaakisi shughuli zao sasa kulinganisha na idadi kubwa iliyopo ya wanasheria.

Alisema katika kuharakisha huduma za kisheria, mfumo wa Mahakama umeboresha utendaji kazi kwa kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) ili kusaidia upatikanaji wa haki kwa haraka.

Lissu akiwa nchini Ubelgiji anakoendelea na matibabu, aliwaandikia wanachama wenzake barua ya kuwaaga akisema; “Jioni ya Machi 18 mwaka jana, nilisimama mbele yenu na kutoa hotuba yangu nikiwa rais mpya. Juni 30, 2017 nilizungumza nanyi tena Dar es Salaam katika mkutano wa dharura wa TLS, lakini leo nazungumza nikiwa katika kitanda cha Hospitali ya Ubelgiji nikiuguza majeraha kama mnavyojua.” Katika salamu hizo zenye kurasa 10, Lissu ameelezea tukio la Septemba 7 mwaka jana, aliposhambuliwa na watu wasiojulikana kwa risasi zaidi ya 38 akiwa nyumbani kwake mjini Dodoma kisha kusafirishwa kwenda Hospitali ya Nairobi kabla ya kwenda Ubelgiji.

“Mlinipa nafasi ya kuwahudumia kwa kipindi cha mwaka mmoja lakini kipindi hicho kilikatishwa miezi saba,” alisema Lissu huku akielezea kwa ufupi mafanikio aliyoyafanya kwa muda huo.

Lissu ambaye pia ni mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) amezungumzia masuala mbalimbali huku akiwataka wanasheria hao kupigania utawala wa sheria kwani bila kufanya hivyo hali itakuwa mbaya na hakuna atakayekuwa salama.

Wakati Lissu akieleza hayo, wanachama wa TLS wamedai kuwa mazingira yao ya kazi yamekua magumu tangu mwaka jana baada ya matukio mbalimbali likiwamo la kushambuliwa kwa Lissu na ofisi mbili za mawakili kuvamiwa na watu wasiojulikana. Wakizungumza katika mkutano wao wa mwaka ulioanza jijini Arusha jana wakijadili mazingira ya kufanyakazi ya uwakili walisema imekua sio nzuri kutokana na sababu mbalimbali lakini wakiwa mawakili, kazi yao ni kuzungumza na hakuna la kuwazuia kufanya hivyo. Wakili Fatma Karume alisema ofisi yao ya IMMMA Advocates ilishambuliwa kwa bomu na nyaraka mbalimbali kuchukuliwa hatua ambayo iliwatia hofu.

“...Kama waumini wa utawala wa sheria na kuwahudumia wateja wetu kupata haki zao, tumejifunza mambo ya msingi, uharibifu uliotokea wa nyumba huo unaweza kulipwa na bima lakini mafaili ambayo ni maarifa yetu inabidi yafichwe angani,” alisema Karume.

Makamu wa Rais wa TLS, Godwin Ngwilimi alisema miongoni mwa walioathirika na kadhia ya uharibifu wa ofisi ya uwakili ya IMMMA ni pamoja na mawakili wawili ambao ni wajumbe wa baraza la uongozi na kufanya kazi ya TLS wakati huo kuwa ngumu.

Pia alisema matukio ya kuvunjwa ofisi ya uwakili ya Prime Attorneys lilishutua jumuiya ya mawakili na kuona umuhimu wa kufanya kazi kwa tahadhari zaidi.

Ngwilimi na Karume walumbana

Katika hali ambayo haikutarajiwa wakati wakijadili mada ya mazingira ya mawakili kufanya kazi nchini ilivyo kwa sasa, Ngwilimi na Fatma ambao wanagombea nafasi ya urais walirushiana maneno ambayo yalionyesha joto la uchaguzi huo kuzidi kupanda.

“Nafahamu anachokisema Makamu wa Rais Ngwilimi kuwa nafasi ya Rais TLS inamhitaji mtu makini asiye na papara ya kuzungumza najua anayesemwa ni mimi lakini tunapaswa tufahamu kukaa kimya au kuzungumza sio wakati wote kunafanya kazi,’’ alisema Karume

Hata hivyo Ngwilimi alionyesha kushangazwa na hali hiyo akidai haikua na lengo ambalo mwenzake ametafsiri na kusema mchango wakati akijadili mazingira ya mawakili umetokana na uzoefu aliopitia katika kushughulikia changamoto zilizojitokeza katika kipindi cha mwaka mmoja.

Alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu uchaguzi huo, mwanasheria mkongwe nchini, Profesa Issa Shivji alisema anaamini wanachama watatumia vyema kura zao kwa kuwachagua viongozi wenye dira na mtazamo sahihi na wala si vinginevyo.
“Ingawa tangu nimestaafu nimeacha kwenda mahakamani, lakini wanachama wachague viongozi wenye utashi wa kukivusha chama,” alisema.