Maajabu ya watekaji wa Mohammed Dewji

Askari wa upelelezi wakifanya uchunguzi wa gari linalodhaniwa lilihusika kwenye utekaji wa mfanyabishara maarufu Mohamed Dewji eneo la Gymkana jijini Dar es Salaam jana. Picha  na Said Khamis

Muktasari:

  • Maswali yameendelea kugubika namna tajiri huyo alivyopatikana na jinsi alivyotelekezwa na watekaji katikati ya Jiji la Dar es Salaam eneo lililosheheni ofisi mbalimbali za Serikali na kidiplomasia

Dar es Salaam. Watu waliomteka mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji ‘Mo’ wamemwachia bilionea huyo katika mazingira yanayofanana na yale waliyomteka, tukio linaloonyesha ustadi na uzoefu wa wahalifu hao.

Walimteka alfajiri ya Oktoba 11 Hoteli ya Colesseum Oysterbay, eneo ambalo pamoja na majengo jirani kuwa na ulinzi unaotumia vifaa vya kisasa, pia wakamuachia eneo la viwanja vya Gymkhana, katikati ya jiji na eneo linalozungukwa na majengo yenye ulinzi mkali.

Na licha ya Kamanda wa Polisi (IGP), Simon Sirro kutangaza kuwa wamelitambua gari walilotumia kumteka Mo Dewji na kuonyesha picha kwa waandishi wa habari, watu hao wasiojulikana wanaonekana walitumia tena gari hilohilo kumrudisha mfanyabiashara huyo tajiri na kumtelekeza katika viwanja vya gofu vya Gymkhana.

Pia, baada ya kumaliza shughuli yao wametelekeza gari hilo aina ya Toyota Surf katika eneo hilo pamoja na silaha ambazo huenda walizitumia kumteka.

Na kwa kuwa Kamanda Sirro alisema katika kufuatilia kamera za usalama waligundua watu hao walielekea hadi mzunguko wa Kawe, nje kidogo ya jiji, hakuna shaka watekaji hao walipita tena barabara zilizo na vifaa vya ulinzi kumrudisha Mo Dewji katikati ya jiji.

Na kama haitoshi, baada ya kuishi na Mo Dewji kwa siku tisa, angalau hadi jana jioni watekaji hao walikuwa hawajatiwa mikononi mwa polisi.

Mo Dewji (43) , anayejihusisha na biashara za aina tofauti kuanzia viwanda hadi vyakula, alitekwa alfajiri ya saa 11:35 alfajiri ya Oktoba 11 katika Hoteli ya Colosseum, Oysterbay ambalo wakazi wake wengi ni vigogo na hivyo majengo wanayoishi kuwa na ulinzi.

Na usiku wa kuamkia jana, watekaji hao walimtupa bilionea huyo pembezoni mwa viwanja vya Gymkhana jijini humo, kwa mujibu wa maelezo ya kamanda wa Polisi wa Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa.

Eneo alilotupwa bilionea huyo kijana barani Afrika ni takriban kilomita moja kutoka yalipo makao makuu ya Jeshi la Polisi.

Jinsi watekaji hao walivyomchukua na kumrejesha Mo Dewji inaonyesha walivyo na uzoefu wa uhalifu wa aina hiyo.

Kuonekana kwa Mo Dewji ikiwa ni siku tisa tangu alipotekwa, kumeendeleza mijadala ya jinsi mazingira ya kupatikana kwake na hatma ya nani hasa atajinyakulia Sh1 bilioni iliyotangazwa na familia ya mfanyabiashara huyo.

Si IGP Sirro au familia ya Mo Dewji ambayo imezungumzia kama kuna mtu aliyetoa taarifa za kuonekana kwake au mfanyabiashara huyo alitumia mbinu anazozijua yeye kumpata baba yake mzazi, Gullam Hussein ambaye alimfuata Gymkhana kumchukua jana alfajiri.

Video iliyorekodiwa muda mfupi baada ya kuonekana kwake, inamuonyesha Kamanda Mambosasa akielezea jinsi walivyopata taarifa na kwenda nyumbani kwa familia hiyo kuthibitisha.

Mambosasa anaelezea kuwa Mo Dewji yuko katika hali nzuri na huku akimpa pole na kumuuliza hali yake, anamualika ili azungumze mbele ya kamera.

Lakini mwekezaji huyo kwenye klabu kubwa ya michezo ya Simba, anaonekana kutokuwa na mwonekano wake wa kawaida. Haonekani kujiamini na muda wote wakati anazungumza, anaonekana kutotaka kuiangalia kamera na badala yake kuangalia chini.

“Naomba kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu, Lakini pia nimshukuru Mheshimiwa Rais na Jeshi la Polisi, mimi ni mzima. Asanteni Watanzania wote kwa kuniombea,” anasema Mo Dewji, ambaye anaonekana amevalia fulana nyeupe yenye mistari ya rangi tofauti kifuani. Ametumia sekunde 67 kutoa salamu hizo.

Mfanyabiashara huyoanayekadiriwa kuwa na utajiri unaothaminishwa kufikia dola 1.5 bilioni za Kimarekani kwa mujibu wa jarida la Forbes, anaonekana mwenye nywele ambazo hazijachanwa, ndevu zake zimeujaza uso na hivyo kuwa na mwonekano tofauti na alivyozoeleka. Haonekani kama alivyozoeleka.

Kamanda Mambosasa anaonekana amevalia kaunda suti nyeusi katika video hiyo iliyorekodiwa nyumbani kwa familia ya Gullam Dewji ambaye ni baba mzazi wa Mo Dewji, na ina urefu wa dakika 3.46.

Atembea kutafuta simu

Gullam mzazi huyo, ambaye alianzisha biashara zilizoendelezwa na Mo Dewji, alisema alimfuata mwanae alfajiri baada ya kupigiwa simu akielezwa kuwa amepatikana.

Akizungumza kwa sauti yenye kuashiria furaha, Gullam alisema alipokea simu iliyopigwa na mwanae akimtaka amfuate kwenda kumchukua Hoteli ya Southen Sun iliyopo takriban mita 200 kutoka eneo aliloachwa.

Alisema baada ya mtendaji huyo mkuu wa kampuni za Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL Group) kushushwa katika eneo la Gymkhana, alitembea hadi katika hoteli ambako aliomba simu na kumpigia baba yake.

“Namshukuru Mungu nimemkuta Mo akiwa salama na haraka nilimpeleka nyumbani, lakini tumemkuta ana majeraha kidogo. Ila jambo la kushukuru ni kwamba yuko hai,” alisema Gullam.

“Tulipofika nyumbani tulianza kufanya mawasiliano na Jeshi la Polisi kwa kuwapa taarifa kuwa kijana wangu nimempata na wao (polisi) walifika nyumbani kwangu Oysterbay.”

Kama ilivyokuwa kwa mwanaye, Gullam alimshukuru Rais John Magufuli kwa kufanikisha kupatikana kwa Mo Dewji.

Waishukuru MCL

Juzi, Gullam alisema wangekutana na waandishi wa habari jana lakini baadaye alighairi na kusema angefurahi kama mwanaye akipewa muda wa kutulia na kuamua kipi cha kuzungumza. Alisema hata yeye pia hakuwa akipumzika kutokana na juhudi alizokuwa akifanya kumtafuta mwanae.

“Tungeomba mtupe nafasi kidogo. Nafikiri tutawajulisha kama ilivyokuwa awali. Unajua Mohammed ametoka katika matatizo ni vyema akapumzika. Na hata mimi sijalala unajua,” alisema Gullam.

“Hata hivyo nawashukuru sana jinsi mlivyokuwa karibu nasi wakati wote huu wa hili tatizo. Tukitaka kuongea tutawapa taarifa.”

Gullam aliishukuru kampuni ya Mwananchi Communication’s Ltd (MCL) inayochapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti kwa jinsi ilivyokuwa ikiripoti tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara huyo tangu alipotekwa hadi kupatikana kwake.

Afya ni nzuri kwa asilimia 100

Akizungumza na Mwananchi nyumbani kwa Mo Dewji jana saa 11: 57 asubuhi, msemaji wa familia hiyo, Azim Dewji alimshukuru Mungu kwa mfanyabiashara huyo kuonekana.

Alisema afya ya bilionea huyo “ni nzuri asilimia 100”, na kwamba kutokana na kutekwa kunaweza kukawa na tatizo la kisaikolojia.

“Amepatikana muda wa saa 8.30 usiku, walimuacha halafu yeye (Mo) akapiga simu kwa baba yake,” alisema

“Tunamshukuru sana Rais (John Magufuli) kwa kuagiza vyombo vyake vya usalama na vyombo vyake. Tumempata.”

Ulinzi waimarishwa

Mwananchi lilifika nyumbani kwa ‘Mo’ Dewji, Oysterbay jijini hapa 10:49 alfajiri na kukuta polisi waliovalia sare na wenye silaha, sambamba na walinzi wa kampuni binafsi wakizunguka kila eneo.

Haikuwa rahisi kuingia ndani au hata kusogelea geti kwa kile kilichoelezwa kulikuwa na maofisa wa vyombo vya dola wakichukua maelezo.

Ulinzi kama huo ulikuwa pia nyumbani kwa baba yake anayeishi karibu na mwanae, lakini wakitofautiana mageti ya kuingia na kutoka magari na wakati mwingine wakitumia geti moja kulingana na mahitaji yao.

“Kule (huku akinyoosha kidole) wapo maofisa usalama na polisi wanafanya mahojiano. Kwa sasa huwezi kuingia wala kuzungumza na familia,” alisema mmoja wa askari aliyekuwa langoni.

“Pengine msubiri wakitoka ndio mtaweza kupata fursa ya kuzungumza nao lakini kwa sasa sidhani.”

doka na Sh1bilioni

Moja ya maswali yanayoulizwa ni je, nani kafanikiwa kupatikana kwa mfanyabiashara huyo ili aweze kujinyakulia dau la Sh1 bilioni?

Hii inatokana na dau hilo kutangazwa Oktoba 15 na familia ya ‘Mo’ kuwa mtu yeyote atakayewezesha kupatikana kwa bilionea huyo kijana atazawadiwa Sh1 bilioni.

Msemaji wa familia Azim Dewji, akizungumza siku alisema, “Yeyote atakayewezesha kupatikana kwa mtoto wetu mpendwa Mohammed atazawadiwa Sh1 bilioni.”

Baba yake, Gullam jana akizungumza na Mwananchi alisema kijana wake huyo baada ya kutupwa Gymkhana alitembea hadi hoteli ya Southen Sun, iliyoko umbali wa takribani kilomita moja kutoka alipotelekezwa na watekaji hao ambapo alikoomba simu na kumpigia baba yake ambaye alifika kumchukua.

Kwa maelezo haya ya Gullam, huenda kitita hicho kimekosa wa kukichukua.