Mabadiliko ya tabianchi kuathiri hifadhi 14 nchini ifikapo 2050

Muktasari:

Hofu iliyopo ni kwamba huenda hifadhi zote  zikatoweka na kubaki za Ruaha na Selous.

Tanga. Iwapo hazitachukuliwa hatua za makusudi ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kuna hatari ya kubakiwa na hifadhi mbili tu kati ya 16 zilizopo nchini ifikapo mwaka 2050.

Tahadhari hiyo imetolewa leo Ijumaa Julai 28 na Mkurugenzi wa Kituo cha Sayansi ya Tembo, Dk Alfread Kikoti katika mkutano wa wahariri wa vyombo vya habari nchini uliofanyika jijini hapa.

Amezitaja hifadhi hizo ambazo utafiti unaonyesha zitabaki kuwa ni Ruaha na Selous ambazo amesema kudumu kwake kunatokana na hali ya kijiografia pamoja na ikolojia.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo ni kwamba mabadiliko ya tabianchi yataleta athari kwenye hifadhi hizo ikiwamo ukame utakaotokana na kukauka maji na malisho ya wanyamapori.

Amesema ili kunusuru kupotea kwa hifadhi hizo, inahitajika mikakati madhubuti itakayohusisha pande zote pamoja na wananchi kwa ujumla.

Mkutano huo wa wahariri wa vyombo vya habari ulifunguliwa na Waziri wa Maliasili na Waziri wa Maliasli na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe jana ambaye aliviomba vyombo vya habari kuweka mbele uzalendo wakati wa kuvitangaza vivutio vya utalii nchini.

Katika mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Tanapa, Allan Kijazi amesema vyombo vya habari vimechangia kwa kiasi kikubwa kuvitangaza vivutio na hivyo kuwavuta wageni kutoka nchi za nje.

Amesema Tanapa itaendelea kuvitumia vyombo vya habari kuielimisha jamii hata katika suala la mabadiliko ya tabianchi ambayo yanatishia mambo mbalimbali zikiwamo hifadhi za wanyamapori.

Wahariri waliohudhuria mkutano huo walionesha hofu juu ya taarifa ya hatari ya kutoweka kwa hifadhi hizo na kuahidi kutumia nafasi zao kuielimisha jamii iweze kukabiliana na mabadiliko hayo.