Madiwani wawili Chadema wahamia CCM

Muktasari:

Ni diwani wa kata ya Romu wilayani Hai, Shilyimaufoo Kimaro na diwani wa kata ya Vumari, Wilayani Same, John Msofe.

Kilimanjaro. Madiwani wawili wa Chadema, wamejivua uanachama na kujiunga na CCM, na kufanya idadi ya madiwani waliohama chama hicho mkoa wa Kilimanjaro kufikia 12.

Waliohama chama hicho leo Agosti 17 ni aliyekuwa diwani wa kata ya Romu wilayani Hai, Shilyimaufoo Kimaro na diwani wa kata ya Vumari, Wilayani Same, John Msofe.

Akizungumzia kuondoka kwa madiwani hao Katibu wa Chadema mkoa wa Kilimanajro,Basil Lema amesema ni kweli madiwani hao wameondoka kwa kile wanachodai wao ni kuunga mkono juhudi za Rais.

Lema amesema kuwa anajua madiwani hao wanahama chama hicho kutokana na baadhi yao kutishiwa uhai na usalama wa maisha yao na wengine wanaondoka kwa sababu ya madeni waliyonayo au maslahi yao binafsi.

“Madiwani wanaobaki wabaki na wale wanaoondoka waondoke lakini tunajua wanaondoka kwa sababu ya vitisho wanavyopata na wengine wanaondoka kutokana na madeni walionayo wakijifanya wanaunga mkono jitihada za Rais,”amesema.

Alihoji kwani ni lazima madiwani wahame kwasababu wanataka kumpa heshima na sifa Rais?

“Ni kweli Rais wetu ameishiwa vitu vya kumpa heshima na sifa ili kodi zetu zitumike  kununulia madiwani  ili yeye apate sifa? je,Rais wetu hawezi kupata sifa kwa kuongeza mishahara ya wananchi?”amehoji Lema.

 

Mkurugenzi Mtendaji  wa Halmashauri ya wilaya ya Same, Anna Shija amesema amepokea barua ya Diwani wa kata ya Vumari.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai,Yohana Sintoo amesema amepokea barua ya kujiuzulu kwa diwani wa kata ya Romu leo asubuhi  kwa kile alichodai kuwa katika chadema hakuna demokrasia pana.

DONDOO

*Katika wilaya ya Siha madiwani waliohama Chadema na kuhamia CCM ni wanne.

*Wilaya ya Hai jumla madiwani sita

* Wilaya ya Rombo diwani mmoja.

* Wilaya ya same madiwani wawili.