Mahanga: Niliongoza Ukonga kwa miaka 10 nikiwa CCM kwa kuiba kura

Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Ilala, Makongoro Mahanga.

Muktasari:

  • Mahanga amewahi kuwa mbunge wa Jimbo la Ukonga kwa miaka kumi kuanzia 2000 mpaka 2010 na baadaye jimbo hilo liligawanywa na kuzaliwa Segerea ambako naibu waziri huyo wa zamani aliliongoza kuanzia mwaka 2010 mpaka 2015.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Ilala, Makongoro Mahanga amesema wakati akiwa CCM alishinda ubunge kutokana na wizi wa kura.

Mahanga amewahi kuwa mbunge wa Jimbo la Ukonga kwa miaka kumi kuanzia 2000 mpaka 2010 na baadaye jimbo hilo liligawanywa na kuzaliwa Segerea ambako naibu waziri huyo wa zamani aliliongoza kuanzia mwaka 2010 mpaka 2015.

Akizungumza jana wakati wa uzinduzi wa kampeni za ubunge wa Jimbo la Ukonga, Mahanga ambaye alihamia Chadema siku chache kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 alisema aliongoza Jimbo la Ukonga kwa miaka 10 na sababu kubwa iliyomfanya ashinde ni kununua kura na hivyo akawataka wananchi wasikubali kununuliwa.

“CCM nawafahamu sana, wanawatumia mabalozi kununua kadi za kupigia kura hata mimi walikuwa wananifanyia hivyo na ninashinda,” alisema Mahanga bila kuwa na nyaraka za kuthibitisha kuhusu madai hayo.

“Kura zinazoibiwa sio za Chadema ni za wananchi, wananchi kataeni kuibiwa,”alisema.

Katibu wa NEC Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa CCM, Kanali Ngemela Lubinga ambaye alisema yupo safarini Mkoa wa Lindi hakusita kumjibu Mahanga jana.

Lubinga alisema Dk Mahanga ni mtu wa kupuuzwa kwani anadhalilisha elimu aliyonayo.

“Huwezi ku-deal na mtu kama huyo. Yaani anawaambia wananchi kuwa alikuwa anaiba kura? ili iweje? Anaidhalilisha hata PhD (shahada ya uzamivu) aliyonayo tu, kama huyo ni wa kuachana naye,” alisema Lubinga.

Uchaguzi huo mdogo utafanyika Septemba 16 baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Mwita Waitara kujiuzulu uanachama wa Chadema na kuhamia CCM.

CCM wamemteua Waitara kuwania jimbo hilo na Chadema wamemteua Asia Msangi.

Akizungumza katika mkutano huo wa kampeni jana, waziri mkuu mstaafu Frederick Sumaye alisema iwapo nchi haina demokrasia ya kweli ya vyama vingi basi taifa litakuwa na wanyonge na maskini.

“Waitara alikuwa mbunge, leo anazungumza habari za (Mwenyekiti wa Chadema-Freeman)Mbowe. Mbowe ndiyo alimchagua kuwa mbunge? Waitara amewadharau sana, amewadharau wana Ukonga kupita kiasi,” alisema Sumaye katika mkutano huo uliofanyika Shule ya Msingi Mzambarauni maeneo ya Mombasa, Ukonga.

“Kwanini mtu afanye madharau ya namna hii na sisi tutake kumfikiria? Haya machama yanayojidai yameleta uhuru yana kiburi hujawahi kuona,” aliongeza

Alisema nchi zote zenye maendeleo ni ambazo zimeondoa vyama vikongwe.

“Sisi wengine tumetoka CCM kule ndio kulikuwa na makulaji, kila kitu kipo safi, lakini nikasema raha yangu iko wapi kama Watanzania wanateseka. Lazima maslahi ya umma yawe mbele kuliko maslahi binafsi,” alisema.

Sumaye ambaye alikuwa waziri mkuu kwa vipindi vyote vya Awamu ya Tatu alisema, “Vyama vya upinzani vina nafasi kama Mwalimu (Julius) Nyerere alivyosema tuingie kwenye mfumo wa vyama vingi ili kupata maoni ya upande wa pili.”

Mbunge wa Tarime Vijijini, (Chadema), John Heche akizungumza katika kampeni hiyo, amesema anaijua hofu waliyonayo CCM kwa sasa.

“Najua hofu iliyopo upande wa pili kwa mimi kuja Ukonga. Niseme wazi nitakuwa kwenye kampeni hizi kuanzia leo hadi siku ya mwisho. Sababu ni kulinda heshima ya Wakurya na watu wa Mara,” alisema.

“Kwa miaka yote Wakurya wameshiriki katika ukombozi kwa kupigania haki. Lakini kwa mara ya kwanza tumeiaibisha nchi hii tumeaibisha Wakurya na watu wa Mara. Nipo hapa kumfundisha yule aliyetuaibisha,”alisema.

Heche alisema anayehama chama ni sawa na mama anayeikimbia nyumba na kuacha watoto wakitaabika kwa sababu ya matatizo ya ndoa.

“Miaka kumi tukiwa kwenye uchaguzi Tarime, alipokufa Chacha Wangwe, Waitara alihamia Chadema baada ya kushindwa kwenye kura za maoni za CCM,” alisema.

Heche alisema: “Eti anasema amejiuzulu kwa sababu ya ugomvi wake na Freeman Mbowe, ujinga kabisa.”

Naibu Katibu Mkuu Zanzibar (Chadema), Salum Mwalimu alisema inashangaza kuona jeshi la polisi linatumia nguvu kubwa kupambana na Chadema.

“Kama nyinyi ni wanaume wa uhakika vaeni nguzo za kijani, pandeni jukwaani muone tutakavyowashughulikia,” alisema. Mgombe ubunge wa jimbo hilo, Asia Msangi alisema amejiandaa kuwapigania vijana na miongoni mwa atakayofanya ni kuanzisha ligi za michezo.

Asia alisema amebaini kuwa wazee hawatendewi haki nchini kwani wamepewa msamaha wa kodi ya majengo, lakini bado hawaupati msamaha huo.

“Kinamama wanapitia changamoto nyingi za kibiashara.

Kuhusu uchaguzi huo, Asia alisema amejiandaa kushinda na kutangazwa mshindi. “Nasema hapa nikiwa serious (makini)sina mchezo kwenye masuala ya msingi. Wana Ukonga mmelizwa ila mmepata mtu wa kuwatuliza. Tupige kura, tulinde kura lakini kikubwa nimejiandaa kutangazwa,”alisema.