Majaliwa awataka wananchi kutomwangusha JPM 2020

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiweka jiwe la Msingi la ujenzi wa barabara za mitaa katika mji wa Chamwino zinazojengwa kwa kiwango cha
lami zenye urefu wa kilometa 3.5 Mkoani Dodoma jana.Kushoto ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Dodoma, Godwin Mkanwa na watatu kushoto ni Mbunge wa Chilonwa, Joel Mwaka. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

Muktasari:

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kwamba Rais John Magufuli atatimiza asilimia 90 ya ahadi alizozitoa wakati wa uchaguzi mkuu 2015 na kuwataka wananchi wasimuangushe itakapofika 2020.

Dodoma. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametamba kwamba Rais John Magufuli atatimiza asilimia 90 ya ahadi zote alizozitoa katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kabla ya kufika mwaka 2020 na kuwataka Watanzania kutomuangusha muda utakapofika.

Majaliwa alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na watumishi na wananchi wa Jiji la Dodoma katika ziara ya kukagua shughuli za maendeleo ikiwa ni siku ya mwisho ya ziara yake.

“Rais atatimiza ahadi zote alizozitoa mwaka 2015 kwa asilimia 90, kabla ya 2020 atakuja kuwaambia alichotekeleza katika ahadi zake,” alisema Majaliwa.

“Lakini nawaombeni sana msimwangushe mara atakapopita tena kuwaombeni, eti mtamwangusha?”

Kauli hiyo ilipokewa kwa shangwe na makofi na watu waliokuwepo katika mkutano huo.

Majaliwa alisema Rais Magufuli anawapenda zaidi wananchi wa Dodoma kwa kuwa walimpa kura nyingi za kutosha katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na kuwataka kutobadilika hata kwa siku zijazo.

Alisema huu ni wakati wa kufanya kazi akisisitiza kwamba Watanzania hawana budi kufanya kazi kwa bidii na kujituma zaidi kwani ndicho ambacho Rais Magufuli anakipenda.

Kuhusu utendaji wa viongozi, Majaliwa alisema bado sekta ya ununuzi imekuwa kichaka cha kufuja mali ya Serikali kutokana na viongozi kuendelea kukiuka masharti na kuchakachua mali ambazo wengine wanahangaika kuzikusanya.

Akizungumzia kitendo cha Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) kufuta matokeo ya darasa la saba ya shule zote za Halmashauri ya Chemba mkoani Dodoma Majaliwa alisema, “Mmetia aibu kubwa kutokana na matokeo ya kufoji mitihani.”

“Hivi pale nia ilikuwa nini, mnatia aibu na fedheha si mnajua nami ni mwenzenu? Mtapoteza kazi bure badala ya kuwafundisha watoto waelewe.”

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amesimamisha ujenzi wa kituo cha madarasa na ofisini katika Mtaa wa Mwanga Baa kwa maelezo kuwa utaziba njia.

Alimweleza mkuu wa idara ya ardhi, Joseph Mafuru kuwa ramani imebadilishwa ili kupata kiwanja hicho na mhandisi huyo alipokataa, Waziri Mkuu alitoa ramani iliyoonyesha uhalisia wa alichosema kisha kuagiza mhusika apatiwe eneo mbadala na asiendeleze ujenzi huo.

Licha ya Mkurugenzi wa Jiji Godwin Kunambi kutolea ufafanuzi suala hilo kuwa lipo sahihi, ramani iliyoonyeshwa na Waziri Mkuu ilionyesha usahihi na kuamuru ifuatwe.

Waziri Mkuu pia aliuagiza uongozi wa Jiji la Dodoma kuanza utaratibu wa kujenga stendi tatu za mabasi ili kukidhi mahitaji ya jiji hilo.

Alisema jiji hilo halipaswi kuwa na stendi moja eneo la Nzuguni, “Nataka mjenge stendi upande wa barabara ya Iringa, Arusha na ya Singida, maeneo yote lazima yawe na stendi ili kupisha msongamano wa magari katikati ya Jiji.”

Alisema ujenzi katika jiji la Dodoma lazima uwe na mpangilio na kuepuka yanayotokea katika jiji kongwe la Dar es Salaam ambako ujenzi umefanyika bila mpangilio licha ya kuwapo kwa ardhi ya kutosha.