Mangula atoa neno wanaCCM kumkataa aliyeitosa Chadema

Makamu Mwenyekiti wa CCM - Bara, Phillip Mangula.

Muktasari:

  • Akizungumza na gazeti hili jana, Mangula alisema Kamati Kuu ya chama hicho itakaa mwezi ujao kuamua nani asimamishwe kwenye uchaguzi wa Monduli na majimbo mengine ikiwa ni baada ya kupata maoni ya chama kuanzia ngazi ya jimbo, mkoa na halmashauri kuu.

Dar es Salaam. Siku moja baada ya kundi la wanachama wa CCM kujitokeza hadharani kupinga aliyekuwa mbunge wa Monduli, Julius Kalanga kurejeshwa kugombea ubunge kupitia chama hicho, Makamu Mwenyekiti wa CCM - Bara, Phillip Mangula amesema hiyo ni hofu tu lakini hakuna mpango huo.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mangula alisema Kamati Kuu ya chama hicho itakaa mwezi ujao kuamua nani asimamishwe kwenye uchaguzi wa Monduli na majimbo mengine ikiwa ni baada ya kupata maoni ya chama kuanzia ngazi ya jimbo, mkoa na halmashauri kuu.

Kuhusu waliohama vyama vyao na kusimamishwa tena kugombea kwenye majimbo yaleyale, Mangula alisema wao wenyewe (jimboni) walitaka iwe hivyo ndiyo maana wagombea hao wakapewa nafasi.

“Wahusika walitaka iwe hivyo ndiyo maana wakapewa nafasi. Kwa mfano jimbo la Kinondoni, aliyepitishwa na chama alipata kura zaidi ya yule aliyegombea kwenye uchaguzi mkuu uliopita,” alisema kiongozi huyo wa chama.

Juzi, baadhi ya wanachama wa CCM kutoka kata za Isilalei, Monduli Juu na Sepeko waliandamana hadi ofisi za chama wakimtuhumu Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Monduli, Wilson Lengima kwamba kwa kushirikiana na viongozi wengine wa chama hicho, wanapanga njama ili Kalanga apitishwe kuwa mgombea ubunge pasipo kufanyika kwa kura za maoni.

Hata hivyo, Lengima alikanusha madai hayo akisema CCM ina utaratibu wake wa kuwapata wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi, hivyo kuwataka wanachama wa CCM kuwa watulivu.

Katibu wa Uenezi wa CCM Kata ya Sepeko, Nooy Naimisye alisema jana kuwa wanataka kuona demokrasia ikitendeka katika kumchagua mgombea ubunge jimboni Monduli.

“Mwenyekiti atupe ukweli kuhusu madai kwamba yupo upande wa mbunge wa zamani aliyejiuzulu Chadema na kutangaza kujiunga na CCM. Tunataka demokrasia hatuna nia kuona mgombea huyu anagombea tena kwenye chama chetu, hili ni kinyume cha kanuni na utaratibu ndani ya chama,” alisema.

Wakati hayo yakiendelea, mbunge wa Mtama, Nape Nnauye ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter:

“Chama hiki kina katiba, sheria, kanuni na utaratibu/utamaduni, ni vizuri wahamiaji wakasaidiwa kuvifuata ili kulinda umoja na mshikamano wetu.”

Alipotafutwa kufafanua maana ya maneno hayo, Nape hakupokea simu wala kujibu ujumbe wa maneno aliotumiwa.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi wameandika kwenye ukurasa wa mbunge huyo. Elibariki Magesa amesema: “Haya maneno Waitara na Kalanga hawataki kuyasikia kabisa wanatamani kurudi walikotoka lakini haiwezekani. Bila huruma za mwenyekiti hawa ndugu zetu wazalendo watapata vichaaa, ‘assume’ kura za maoni wapingwe na pensheni wakose si wazalendo ‘let it be’ (na iwe hivyo).”

Sylvester Muyigwe ameandika: “Kama kuna mahali Katiba ya nchi imekanyagwa na wewe na wenzako mkashangilia mkiona kuwa wamekomolewa Chadema au yoyote asiye wahusu basi eleweni hata hiyo ya chama itakanyagwa zaidi ya hii ya nchi na hamtakua na lakufanya.”

Meyasi Mollel ameandika: “Tuna tatizo kubwa sana katika siasa za nchi yetu na wanasiasa wanatupeleka pabaya sana. Siasa safi ina katiba, sheria, kanuni na utaratibu. Bro, double standard ni hatari sana...”