Tuesday, April 18, 2017

Mauaji yaathiri uchaguzi CCM

By Azory Gwanda, Mwananchi agwanda@mwananchi.co.tz

Kibiti/Rufiji. Mauaji yanayoendelea dhidi ya viongozi, yamesababisha wanachama wa CCM wa wilaya za Kibiti na Rufiji mkoani Pwani kuogopa kuchukua fomu za kugombea nafasi za uongozi ngazi za tawi na shina.

Tayari, zaidi ya askari 10 na viongozi 11 wa vijiji na watendaji wameuawa katika wilaya za Mkuranga, Rufiji na Kibiti, lakini hadi sasa wauaji hawajajulikana wala sababu za mauaji hayo.

Katika baadhi ya matukio, wauaji waliacha majina ya viongozi walio katika orodha ya watu wanaowasaka ili wawaue.

CCM, ambayo ilishinda viti vingi vya ubunge, udiwani na serikali za mitaa katika wilaya za mkoa wa Pwani, imeanza uchaguzi wa ndani kuanzia ngazi ya matawi hadi mkoa na baadaye itafanya uchaguzi wa kitaifa.

Akiongea kwa njia ya simu na gazeti hili jana, Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM anayesimamia wilaya hizo mbili, Mussa Nyeresa alisema wanachama wanasita kuchukua fomu.

Alisema sababu pekee ya wanachama hao kutojitokeza ni hofu ya maisha yao inayotokana na mauaji ya viongozi tofauti wa matawi ya chama hicho, wajumbe katika uongozi wa serikali za vitongoji na vijiji na wenyeviti wa vitongoji na vijiji katika wilaya hizo.

Mwenyekiti wa UVCCM Kata ya Ikwiriri, Saudi Mnengo alisema hali imekuwa tofauti mwaka huu kwa kuwa wanachama wamegoma kuchukua fomu na kushauri uchaguzi huo usogezwe mbele. 

 

-->