Mbunge Ukerewe aomba kivuko kingine

Muktasari:

  • Mkundi ametoa ombi hilo mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika shughuli ya mazishi ya kitaifa Ukara

Ukara. Mbunge wa Ukerewe (Chadema), Joseph Mkundi ameiomba Serikali kutafuta namna wakazi wa Kisiwa cha Ukara watakavyoendelea kupata huduma ya usafiri wa kuwaunganisha na wenzao wa Kisiwa Kikuu cha Ukerewe ambako ndipo mahitaji muhimu yanapatikana.

"Hii ndiyo namna pekee ya kutufariji kwa msiba huu mkubwa uliotukumba," amesema Mkundi.

Akitoa salaam kwa niaba ya wananchi leo Septemba 23,2018, Mkundi amesema licha ya ajali ambayo imesababisha vifo vya watu zaidi ya 200, maisha ya wakazi wa Ukara ikiwamo kuvuka kwenda Bugorola kufuata mahitaji lazima yaendelee.

Naye, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, George Nyamaha ameiomba Serikali kuimarisha utendaji wa Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) wilayani Ukerewe kwa kuipa vifaa, zana na nguvu kazi ili imudu kutekeleza na kusimamia usalama wa wasafiri.

"Sumatra ina mtumishi mmoja pekee wilayani Ukerewe, tena asiye hata na usafiri. Hawezi kutekeleza majukumu yake ipasavyo katika visiwa 38 vya wilaya hii," amesema Nyamaha.