Mbunge apaza sauti, njaa

Mbunge wa Tabora Mjini, Emmanuel Mwakasaka

Muktasari:

  •  Akizungumza kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri Mkoa (RCC) juzi, Mwakasaka alisema chakula ni changamoto kwani bei zimepanda na kwamba, hivi sasa debe la mahindi linauzwa Sh23,000 ilhali miezi mitatu iliyopita ilikuwa Sh12,000.

Tabora. Mbunge wa Tabora Mjini, Emmanuel Mwakasaka amemtaka Mkuu wa mkoa huo, Aggrey Mwanri kuhakikisha chakula kinatolewa kwenye maghala ili kudhibiti mfumko wa bei.

 Akizungumza kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri Mkoa (RCC) juzi, Mwakasaka alisema chakula ni changamoto kwani bei zimepanda na kwamba, hivi sasa debe la mahindi linauzwa Sh23,000 ilhali miezi mitatu iliyopita ilikuwa Sh12,000.

“Suala la chakula ni gumu, tukiwa wawakilishi wao wananchi hawatuelewi, hivyo kilichopo ghalani kitolewe kushusha bei,” alisema.

Akizungumzia hali hiyo, Mwanri aliwataka wananchi kuacha malumbano kuhusu chakula, badala yake watunze walichonacho.

Mwanri alisema wanatumia muda mwingi kubishana badala ya kuchukua hatua za kukabiliana na tatizo hilo.