‘Mchwa’ wavamia Tasaf, watafuna mamilioni ya shilingi

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene

Muktasari:

Hayo aliyasema jana mjini hapa wakati akifungua kikao kazi cha wakuu wa mikoa, wilaya, makatibu tawala na wakurugenzi wa mamlaka za Serikali za Mitaa kutoka mikoa ya Kanda ya Mashariki na Kati kilichoandaliwa na Tasaf kwa lengo la kupitia utekelezaji wa mpango huo.

Morogoro. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene amesema mpango wa kunusuru kaya maskini unaosimamiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), umebainika kuwa na changamoto nyingi ikiwamo  uingizwaji wa watu wasio na sifa.

Hayo aliyasema jana mjini hapa wakati akifungua kikao kazi cha wakuu wa mikoa, wilaya, makatibu tawala na wakurugenzi wa mamlaka za Serikali za Mitaa kutoka mikoa ya Kanda ya Mashariki na Kati kilichoandaliwa na Tasaf kwa lengo la kupitia utekelezaji wa mpango huo.

Waziri Simbachawene alizitaja baadhi ya changamoto nyingine kuwa ni kutofikisha ruzuku stahiki kwa walengwa, baadhi ya viongozi wa kamati za mpango huo kuwa ni miongoni mwa walengwa na wengine kuchukua malipo ya walengwa ambao wamefariki au kuhama maeneo yao.

Pia, alisema Februari Serikali ilitoa agizo la kufanya uhakiki ili kuondoa kaya zisizostahili na kwamba, kaya 32,456 zimeondolewa kati ya hizo 7,819 tayari wamekufa; 2,999 ni viongozi; 3,948 walihama; 9,342 hawafahamiki na 8,348 hawakuwa na sifa.

Akizungumza kwa niaba ya viongozi waliohudhuria kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo alisema kikao hicho kitaongeza uelewa wa masuala mbalimbali hususan utatuzi wa  changamoto zilizojitokeza.