Mhandisi Mv Nyerere asimulia alivyoishi zaidi ya saa 48 ndani ya maji

Muktasari:

  • Alphonse Augustine Charahani, fundi mkuu wa kivuko cha MV Nyerere Asema hatalisahau tukio hilo milele, baada ya kuokoka katika mazingira ambayo hakuna aliyetarajia angetoka akiwa hai.

Kumbukumbu yake ipo pale pale. Anakumbuka kama vile imetokea dakika mbili zilizopita.

Alphonse Augustine Charahani, fundi mkuu wa kivuko cha MV Nyerere kilichopata ajali Septemba 20, mwaka huu katika kisiwa cha Ukara, wilayani Ukerewe Mkoa wa Mwanza.

Ni mmoja kati ya abiria 41 walionusurika kwenye ajali hiyo iliyogharimu maisha ya watu 230.

Baada ya kunusurika kwenye ajali hiyo katika mazingira ambayo kila mmoja hakutarajia, na baadae kulazwa hospitalini, Mwananchi ilimtafuta Mhandisi Charahani na kufanikiwa kuzungumza nae mambo mbalimbali kuhusiana na ajali hiyo na jinsi alivyoweza kuokolewa.

Makazi ya Mhandisi Charahani yapo katika mji mdogo wa Kigongo Feri wilayani Misungwi, pembezoni mwa Ziwa Victoria.

Baada ya wawakilishi wa Mwananchi kufika nyumbani hapo, walikaribishwa na watoto wa fundi huyo kwa nyuso za furaha.

Muda mfupi baada ya makaribisho, Mhandisi Charahani aliungana na wageni sebuleni walikokaribishwa wakiwa pamoja na watoto wake wawili, Alicia na Meremo.

Safari iliyozamisha kivuko

Mhandisi Charahani anaanza kusimulia kwamba, Alhamisi ya Septemba 20, mwaka huu milele itabaki kuwa siku ya historia maishani mwake.

“Asubuhi hiyo tukiwa pale Ukara katika Kijiji na Kata ya Bwisya, tulipakia vizuri abiria na mizigo, nami kama kawaida nilikagua kila eneo langu ninalopaswa kulisimamia na kuhakikisha usalama wake na kujiridhisha kuwa kila kitu kilikuwa kwenye mstari na hatimaye tukaondoka,” anasema Mhandisi Charahani.

Anasema baada ya kutia nanga katika gati ya Bugorola, saa nne asubuhi abiria wote na mizigo ilishushwa naye alibaki akifanya tathimini na maborehso kulingana na nafasi kile alichotakiwa kufanya akiwa fundi mkuu wa kivuko hicho.

Mhandisi Charahani anasema ilipofika saa tano walianza kupanga mizigo na abiria kwa ajili ya kuanza safari ya kuelekea Ukara kama ilivyo ada kwa chombo hicho.

Safari ilianza saa sita kama na nusu hivi za mchana. Kivuko hakikuwa na dalili yoyote ya upungufu wala hitilifau kwenye mfumo wake wa injini na kwingineko.

Anasema, anakumbuka ndani ya safari hiyo ya Bugorola-Ukara alipanda juu kwa nahodha kama mara mbili hivi, kutoka ofisini kwake kwa ajili ya kujaza baadhi ya nyaraka kama iliyo kawaida.

“Niliweza kupanda kule juu kwa nahodha Constatine Mahatane (marehemu) na nikiwa nimebeba fomu fulani zinazojazwa wakati safari imeanza na kabla ya kutia nanga,” anakumbuka Charahani.

Anasema akiwa anaendelea kujaza fomu hizo kwa kuamini kwamba wamekaribia kutia nanga Ukara, ghafla alijikuta amelala na fomu hizo zimetapakaa kwenye chumba chake kidogo cha ofisi alimokuwamo.

Kwa mujibu wa Mhandisi Charahani, awali hakudhani kama kuna shida yoyote imetokea maana dakika chache zilizopita, alitupia jicho dirishani na kuiona gati ya Bwisya, hivyo alijua muda sio mrefu nahodha ataanza kushusha ngazi ili magari yaanze kuruhusiwa.

Ajali

Saa nane mchana wa siku ile, Mhandisi Charahani anasema kamwe hawezi kuisahau. Akiwa bado hajainuka kutoka chini alikolala baada ya kudondoka ghafla na kumfanya aziachie hata zile karatasi alizokuwa akizijaza, kivuko kilizimika na injini zote za upande ule wa karibu na ofisi yake zilikuwa kichwani mwake.

Anasema oili ilikuwa iikimwagika kwa fujo kama maji, na yote ilikuwa inamdondokea pale ofizini kwake alikokuwa. Hakuwa na uwezo wa kutoka maana mlangoni maji yalikuwa yameanza kujaa, hivyo kwa muda ule hakujua cha kufanya.

“Kikuweli baada ya kusikia kelele za watu nikiwa mule ndani huku oili ikiendelea kumwagika, ndipo akili ilikuja kwamba tayari tumezama na hakuna jinsi ya kujiokoa. Siwezi kushuka chini na kutafuta mlango ili nipenye kwenda nje,” anasimulia.

Anasema baada ya kivuko kupinduka na kugeuka chini juu, yeye kwa kuwa ofisi yake ilikuwa chini ina maana kwamba sasa alikuwa juu. Hilo lilimpa shida hata namna ya kufanya mawasiliano.

Alikaa humo huku kelele za kuomba msaada zikisikika, sio watoto, kinamama au wazee, sauti zilikuwa sawa na zile za kanisani wakati wa kuimba nyimbo za kuabudu.

“Niligaagaa ndani humo bila mafanikio yoyote. Baada ya muda hata zile kelele nilizokuwa nikizisikia zilitoweka, nguvu za kuwaza pia zikapungua nisijue cha kufanya,” anaeleza.

Anasema kilichoendelea kumpa wasiwasi ni ile oili iliyozidi kumwagika huku maji nayo yakiongezeka kwa kasi. Muda sio mwingi chumba chake kilijaa maji na hivyo akaanza kuelemewa.

Charahani anasema Alhamisi hiyo alikesha akiwa amesimama huku maji yakiwa yamekaribia kumfikia shingoni.

Namna alivyotumia oili, funguo, kalamu ili aokolewe

Ilipofika Ijumaa alfajiri, anasema alisikia sauti na watu wakitembeatembea juu ya kivuko kile ingawa hakujua kwamba kimekaa kwa namna gani.

“Akili iliniijia na nikambuka kwamba mfukoni nilikuwa na simu, funguo na kalamu. Kwa kuwa nimesomea fani inayohusiana na mambo ya majini, niliweza kutumia moja ya mbinu kubahatisha kama walioko nje wangeweza kunisikia, lakini ilishindikana,” anaeleza.

Hadi jioni ya siku hiyo, anasema alikuwa hajui cha kufanya ingawa alikuwa na matumaini kwamba uwezekano wa kuokolewa upo. Hakuhisi njaa, alichokifanya ni kuendelea kuumiza kichwa namna gani angeweza kutoka majini huku akiwa na muda mrefu hajafanya mazoezi ya kuogelea.

Anasema baadae alivua saa na kuitupa majini huku akiendelea kujipaka oili mwili mwake, lengo likiwa asiloe wala kusukumwa na maji. Pia, ilimsaidia mwili kuchemka na kukabiliana na ubaridi.

“Nilijipaka oili hadi kichwani. Kwa kuwa hakukuwepo na mbinu nyingine zaidi ya hiyo, wakati mwingine niliona oili ile ni rafiki wa karibu kwangu,” anasema Charahani.

Ilipofika Jumamosi asubuhi, sauti za watu na vishindo vya miguu viliendelea kusikisika juu ya kivuko. Kwa kuwa alikuwa na funguo zilizofungwa pamoja, alikumbuka mbinu walizokuwa wakizitumia wakati akiwa chuoni.

Alizishika kwa pamoja na kugongagonga akiwa ndani. Aligonga kwa karibu saa nne, lakini hakuna aliyefanikiwa kumsikia.

Ilipofika saa mbili asubuhi, alianza kuona maji yakichezacheza, ishara kwamba kuna kiumba hai kilikuwa kinajaribu kumsogelea.

“Niliingiwa na wasiwasi mkubwa kwamba huenda ni wale samaki wala watu au hata mamba. Nilijaribu kuvumilia na kumuomba Mungu huku nikikumbuka familia yangu changa kwamba ingebaki namna gani kama kingenitokea chochote cha kunitoa duniani,” anasema Chaharani.

Anasema ilipofika saa tatu hivi, kivuli alichokiona mwanzoni kikaendelea kuwepo. Hakuwa na hakika kilikuwa cha kiumbe gani lakini kilikuwa kikisogea.

Anasema muda huo huo, aliskia mkono wa binadamu unamgusa mguu wake wa kushoto. Alishtuka na yule mtu alimsogelea na hatimaye akazama ndani alikokuwa mhandisi.

Kwa kuwa alikuwa amevalia ‘mask’ hakuweza kuzungumza naye bali alimuashiria kinachotakiwa kufanyika naye akawa mwepesi wa kuelewa.

“Baada ya mazungumzo ya ishara, muokoaji huyo aliondoka na kuniacha ndani. Alikaa sana kabla ya kurudi hadi nikaanza kujiuliza maswali mengi kwamba, inawezekana ameenda hapo nje akawaambia hakuna mtu,” anasema.

Mhandisi huyo anasema muokoaji huyo alirudi akiwa amebeba mitungi miwili mgongoni, mmoja wa kwake na mwingine wa mhandisi. Kwa kutumia lugha ile ile ya ishara, alimwelekeza namna ya kuvaa na jinsi ya kupumua kisha wote wakaelewana.

“Aliniuliza kama nina nguvu au anibebe, nikamwambie nipo sawa. Je, unaweza kuogelea? Nikamwambia naweza ingawa nina siku nyingi sijafanya mazoezi,” anasema.

Anasema alimuomba mkono wake wa kushoto kama vile wanaonyeshana ishara ya kuagana, kisha akamsukuma chini ya maji baada ya kuelea kwa dakika kama tatu, mhandisi alijikuta yupo nchi kavu akiwa amebebwa na kikosi cha uzamiaji.

Baada ya kuokolewa

Baada ya kufikishwa nchi kavu, Charahani anasema anakumbuka kusikia sauti ya mtu mmoja aliyeamuru kwamba asiulizwe swali lolote na apelekwe hospitali moja kwa moja.

Alifanyiwa vipimo, ikiwemo kufinywa tumbo, kudadisiwa mwili kama kuna majeraha, muda mfupi kabla ya kusafirishwa kwa helkopta na kupelekwa Hospitali ya Rufaa, Bugando jijini Mwanza.

Akiwa hospitalini, alipewa huduma na afya yake iliendelea kuimarika hatua kwa hatua. “Nilikuwa natamani sana nirudi Ukara nikawaone wenzangu waliozama. Akili ilihangaika sana lakini basi,” anasema.

Anaongeza kwamba baada ya mke wake, Cecilia Kichaga, kufika hospitalini hapo na kumwambia kwamba waombolezaji wanakesha nyumbani kwake, Kigongo Feri wakisubiri mwili kwa ajili ya maziko, ilimuumiza sana.

Mhandisi Charahani anasema mke wake alimwambia kwamba hadi picha ya kutundika kwenye jeneza ilikuwa tayari imeshatangenezwa, jambo lililomsababishia huzuni kubwa fundi mkuu huyo.

Hali yake kwa sasa

Anasema sasa anaendelea vizuri na kila baada ya siku nne anarejea hosipitali kwa ajili ya kuangalia hali yake.

Anasema mbali na afya yake kuimarika hatua kwa hatua, bado kumbukumbu ya ajali hiyo inaendelea kumtesa jambo ambalo linaitia familia yake wasiwasi mkubwa.

“Kama unavyoniona, afya yangu iko sawa lakini ile ajali bado inanisumbua sana nikikumbuka abiria, marafiki na watoto wote walioangamia mle, najisikia huzuni kubwa,” anasema.

Hata hivyo, licha ya yaliyotokea anasema ajali hiyo ni sawa na ajali nyingine, bali tofauti yake ni idadi ya maisha ya watu yaliokatishwa ghafla.

Anatoa mfano wa ajali za barabarani amabpo madereva wakinusurika, wanarudi kazini na kuendelea na maisha yao ya kazi.

“Siwezi kusema kwamba nimestaafu, hii ndiyo fani yangu, siwezi kusema kwamba nitaendelea kukaa tu nyumbani wakati utaalamu ninao,” mhandisi.

Anasema kwa sasa hana la kusema, lakini anaweka wazi kwamba kama angekuwa na uwezo angewapa watu wote wanaoishi karibu na ziwa mafunzo ya kuogelea ili kujisaidia wakati wa ajali ya majini.