Msigwa amshukia Dk Kigwangalla bungeni

Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa akizungumza bungeni alipokuwa akichangia mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2018/2019, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Ni katika bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya mwaka 2018/19

Dodoma. Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa amemtaka Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla kujifunza namna wizara hiyo inavyoendeshwa na kuiendesha kwa manufaa ya Taifa.

Pia, Mchungaji Msigwa amemtaka Dk Kigwangalla kulieleza Bunge, tuhuma za ufisadi alizozitoa dhidi yake na Waziri wa zamani wa wizara hiyo, Lazaro Nyalandu zimeishia wapi na yeye amepokea kiasi gani kutoka kwa wawekezaji.

Hayo ameyasema leo bungeni Mei 21, 2018 wakati akichangia bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya mwaka 2018/19 ya Sh115.8 bilioni.

“Ulisema utautatua mgogoro wa Loliondo na ukasema kuwa mimi (Msigwa na Nyalandu) tulipokea rushwa, sasa na wewe utueleze ulipokea kiasi gani na magari umekwenda kuyapokea,” amehoji Msigwa.

Amesema wizara hiyo ina sifa ya mawaziri wake kutodumu muda mrefu isipokuwa Zakia Meghiji.

“Kaa ujifunze wizara vizuri, wizara ina mambo mengi,” amesema.