Thursday, September 14, 2017

Mtoto ‘atekwa’ na kuuawa kisha mwili wake kutupwa mtaroni Kibaha

By Hamida Shariff, Mwananchi

Morogoro. Mtoto Rehema Juma(5) mkazi wa Mtaa wa Kingolwira Manispaa ya Morogoro ameuawa na mwili wake kutupwa kwenye mtaro Kibaha mkoani Pwani baada ya ‘kutekwa’ na mtu anayedaiwa kuvaa baibui.

Mtoto huyo inadaiwa ‘alitekwa’ wakati akiwa anacheza jirani ya nyumbani kwao.

Taarifa za tukio hilo limeibua taharuki kwa wakazi wa Manispaa ya Morogoro hususani wenye watoto wadogo hasa ukizingatia siku za hivi karibuni kulitokea matukio ya utekaji na mauaji ya watoto jijini Arusha ambapo tukio hili la Morogoro bado halijafahamika kama visasi ama ushirikina.
Bibi aliyekuwa akimlea toto huyo, Maua Muhongole (74) amesema mtoto huyo alitekwa Septemba 12 jioni alipokuwa akicheza na wenzake na kwamba jitihada za kumtafuta zilifanyika hadi kufikia leo ndipo alipokea taarifa za kupatikana kwa mwili wa mtoto huyo maeneo ya Kibaha mkoani Pwani.

"Majira ya saa mbili kasoro usiku wakati chakula kikiandaliwa nilimtuma mjukuu wangu mwingine akamuite mwenzake ambapo alirudi na kunimbia kuwa wenzake wamemwambia hayupo kaondoka na mwanamke aliyevaa baibui kwenda kuchukua pipi dukani muda mrefu uliopita," amesema Maua .

Mtoto Ndichai Idrisa (6) ambaye alimuona Rehema akiondoka alisema aliondoka na mama huyo wakati yeye akiwa kwenye baiskeli akirudi nyumbani na baba yake na alimuita ili arudi nyumbani lakini Rehema hakuongea lolote.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonce Rwegasira amesema jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi zaidi ili kumtafuta mtuhumiwa aliyehusika na wizi wa mtoto huyo kabla ya kuuawa.

Kamanda Rwegasira alikiri kupokea taarifa za kupotea kwa mtoto huyo hata hivyo alisema kuwa tayari ameshatuma askari wake kwenda eneo la tukio kunakohisiwa kuwa mwili wa mtoto ulikutwa kwenye mtaro ili wajiridhishe na kuweza kutoa taarifa.
Amesema tukio la wizi wa mtoto lilitokea Septemba 12 saa mbili usiku na kwamba inadaiwa mwizi wa mtoto huyo alimdanganya  amfuate ili akampatie pesa na kutokomea naye.
Amesema pia mwizi wa mtoto huyo alitumia gari ndogo aina ya taxi yenye rangi nyeupe iliyokuwa imeegeshwa mita 60 kutoka eneo la tukio ambalo lilionekana tangu majira ya mchana na baada ya tukio hilo gari hilo lilitoweka.

-->