Mtoto azungumza na Dk Magufuli, mama aongea na Mwalimu Nyerere

Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Ingwe iliyopo Tarime, Monica Bernard akionesha kiasi cha Sh5 milioni alizokabidhiwa na Rais John Magufuli, Sepemba 7 mwaka huu kwa ajili ya maendeleo ya shule yao, mkoani Mara. Pia Rais Magufuli aliendesha harambee ya papo kwa hapo ambapo zilipatikana jumla ya Sh26 milioni kwa ajili ya maendeleo ya shule hiyo. Picha na Ikulu

Muktasari:

  • Hoja ya mtoto yamsukuma JPM kuendesha harambee na kukusanya zaidi ya Sh25 milioni papo hapo

Tarime. Unaweza kusema mtoto wa nyoka ni nyoka au papai haliwezi kutoa matunda ya maembe. Ndivyo ilivyo kwa Monica Bernard (20), mtoto wa Rhobi Francis (48) aliyethubutu kunyoosha mkono na hatimaye kutoa kilio cha matatizo yanayoikabili shule yake.

Septemba 7, Monica anayesoma kidato cha tano katika Sekondari ya Ingwe wilayani Tarime alimuorodheshea Rais John Magufuli matatizo yanayoikabili shule hiyo alipokuwa eneo la Nyamongo katika ziara ya kikazi mkoani Mara.

Hata hivyo, wakati wananchi wengi waliushangaa uthubutu wa mwanafunzi huyo kuzungumzia matatizo ya shule yao kwa ujasiri mbele ya mkuu wa nchi, mama yake, Rhobi wala hakushangaa.

“Hata sikushtuka nilipomsikia Monica kupitia redioni akizungumza mbele ya Rais Magufuli, naujua uwezo na ujasiri wake kwa kile anachokiamini,” anasema Rhobi.

Akizungumza nyumbani kwake kijiji cha Gamasara, mama huyo anafichua kuwa hata yeye aliwahi kuzungumza mbele ya mwasisi wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alipotembelea shuleni kwao mwaka 1986.

Wakati huo, mama huyo alikuwa akisoma darasa la tano katika Shule ya Msingi Kemamge wilayani humo. “Kama ambavyo inafanyika hivi sasa kwa Monica, watu wengi walistaajabishwa na uwezo na ujasiri wangu wa kusoma risala mbele ya Nyerere.”

Anasema ujasiri wake ndio ulimwezesha kuwalea watoto wake kwa kuwapa mahitaji yote muhimu tangu mume wake alipofariki dunia mwaka 2005.

“Wakati mume wangu anafariki dunia watoto wangu akiwemo Monica walikuwa wadogo na wengi hawakutegemea kama nitamudu kuisimamia na kuilea familia mwenyewe, lakini nimemudu kuwapa watoto wangu mahitaji yote muhimu ikiwemo elimu,” anasema Rhobi akimshukuru Mungu.

Mtoto alivyoshangaza wengi

Kwa upande wa mwanaye, Monica, Septemba 7 ilikuwa ni siku ya kipee yenye kumbukumbu isiyofutika maishani baada ya kupata fursa ya kuzungumza mbele ya Rais na kusababisha harambee ya dharura iliyofanikisha kupatikana zaidi ya Sh25 milioni za kutatua baadhi ya changamoto shuleni.

Rais Magufuli mwenyewe alichangia Sh5 milioni baada ya mwanafunzi huyo kumtajia changamoto hizo ikiwamo ya ukosefu wa bweni, maabara ya Jiografia, maktaba, vitabu vya ziada na kiada pamoja na upungufu wa walimu.

Ujasiri mbele ya Rais

“Sikupanga wala kujiandaa kuzungumza mbele ya Rais Magufuli kama wananchi wengine, nilifika kumwona na kumsikiliza kiongozi huyo,” anasema Monica.

“Lakini baada ya kuona viongozi wote kuanzia ngazi ya kata, wilaya na mkoa hawajazungumzia elimu ndipo nikajiwa na wazo la kuomba nafasi ya kuzungumza.”

Katika mahojiano maalumu na Mwananchi nyumbani kwao Gamasara, binti huyo anasema licha ya Serikali kutoa elimu bure kuanzia ya awali hadi sekondari, sekta hiyo bado inakabiliwa na changamoto ikiwamo kutoboreshwa kwa miundombinu ya kufundishia na kujifunzia.

Monica ambaye ni mtoto wa nne kuzaliwa katika familia ya Bwana na Bibi Bernard Dungu, anasema baada ya kufuta ada na michango mbalimbali kwa shule za msingi na sekondari, Serikali sasa inapaswa kuelekeza nguvu katika kuboresha taaluma kwa kupeleka vitabu, kuajiri walimu kulingana na mahitaji na kuboresha miundombinu.

Anasema, “maendeleo kupitia uchumi wa viwanda ifikapo 2025 inayosisitizwa na Serikali itakuwa ni ndoto kufikiwa bila suala la elimu kupewa kipaumbele.”

“Serikali lazima iboreshe shule za umma kimiundombinu, ufundishaji na huduma.”

Mwanafunzi huyo anayechukua mchepuo wa masomo ya sanaa akisomea Historia, Lugha na Jiografia akiwa na ndoto ya kuwa mwanasheria bora siku zijazo, anasema elimu bora itaiwezesha jamii kupambana na kumudu mabadiliko na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Monica ambaye ni kati ya wanafunzi sita waliofaulu mitihani ya kidato cha nne katika Sekondari ya Nyadoto na kupangiwa kuendelea na masomo ya kidato cha tano na sita katika Sekondari ya Ingwe, anasema upungufu wa walimu na kukosekana kwa baadhi ya miundombinu muhimu kama maabara na mabweni vinakwamisha matumaini yake na wenzake kielimu.

“Kwa uchache tunaochukua masomo ya michepuo ya HGK na HGL tungekuwa hata na walimu saba, lakini hivi sasa wapo wanne pekee wanaofundisha wanafunzi 60,” anasema mwanafunzi huyo.

“Hii inatulazimisha kufanya kazi ya ziada sisi pamoja na walimu wetu. Shule yetu inakabiliwa na upungufu wa vitabu, vitanda na huduma ya maji.”

Anasema, “ukosefu wa vitabu na upatikanaji wa majisafi na salama ni miongoni mwa mambo tutakayoyapa kipaumbele ili kunufaisha wanafunzi wote 748.”

Monica anafananisha kukosekana kwa vitabu kwa ajili ya wanafunzi sawa na kupeleka askari asiye na silaha vitani.

“Kama ambavyo askari anayekwenda vitani, anaweza kuuawa kirahisi na maadui zake ndivyo pia wanafunzi wasio na vifaa vya kujifunzia wanavyoweza kufeli katika masomo yao.

“Wanafunzi kukaa shuleni bila vitabu na miundombinu ya kufundishia na kujifunzia ni sawa na kazi bure kwa sababu si tu hawatafaulu, bali pia hawataelimika,” anafafanua.

Anasema kuboresha mazingira ya elimu katika shule za umma kutawezesha wanafunzi wengi, hasa kutoka familia maskini kufikia ndoto zao za elimu na kimaisha.

Kwa nini ni jasiri sana

Anasema ujasiri wake wa kusimama na kutoa hoja mbele ya Rais bila hofu ulitokana na tabia yake ya kujiamini na usahihi wa kila anachokifanya. “Kuna watu wanahoji ilikuwaje mtoto wa kike nilisimama na kuzungumza kwa ufasaha mbele ya Rais, nadhani hili siyo sawa kudhani wanawake hawawezi. Wanawake wanaweza sana wanapopewa nafasi. Tuache kusubiri kuwezeshwa, tuanze kujitafutia fursa na kujiwezesha wenyewe kwanza.”

Anasema kutojiamini, hofu na kutoshirikiana miongoni mwa wanawake ni sababu za kundi hilo kubwa kutofanikiwa katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa.

“Namshukuru bibi yangu kwa kunipa malezi ya kujiamini katika kila lililo la haki na sawa,” anasema Monica ambaye aliishi na kulelewa na bibi yake baada ya baba yake kufariki dunia akiwa na umri mdogo.

Anasema kutokana na majukumu ya kutunza familia, mama yake alilazimika kujihusisha na shughuli za kibiashara, hivyo jukumu la malezi yake na ndugu zake kusalia mikononi mwa bibi yao.

Fedha za harambee ya Rais

Akizungumzia fedha za haramnbee aliyoifanya Rais Magufuli baada ya kusikia kilio chake, anasema: “Kutokana na agizo la Rais kuwa fedha zilizopatikana kupitia harambee ile maalumu na ya dharura aliyoiendesha zitumike kwa kuzingatia mapendekezo na kipaumbele cha wanafunzi, tunatarajia kukutana na kulijadili hili baada ya shule kufunguliwa.”

Monica ambaye yuko nyumbani kwa likizo fupi, anasema kikao cha kujadili na kupanga matumizi ya fedha hizo kitahusisha wanafunzi pamoja na walimu wao ili kuangalia changamoto za kipaumbele.

Kongole kutoka kwa Diwani

Miongoni mwa waliokunwa na kustaajabishwa na uwezo wa Monica ni diwani wa Kata ya Kemambo, Rashid Bogomba anayesema ujasiri wa mwanafunzi huyo umetoa mwanga wa utatuzi wa changamoto zinazoikabili shule hiyo anayosema ameziwasilisha kwenye vikao vya baraza la madiwani mara kadhaa bila kupatiwa ufumbuzi.

“Nitatumia nafasi yangu kuendelea kufuatilia utatuzi wa changamoto zinazoikabili shule hii na taasisi nyingine za umma kwenye kata yangu. Pamoja na halmashauri kuanza mikakati ya kushughulikia suala hili, agizo la Rais Magufuli itakuwa chachu ya ufumbuzi kupatikana,” anasema Bogomba.