Namna ya kusikiliza kwa makini na kupata manufaa

Muktasari:

Au inatokea kuwa uko katika gari lako ukiliendesha kuelekea mahali usipopajua bali ulielekezwa tu na hatimaye ukagundua kuwa umepotea. Kisha unaomba msaada njiani na kukuelekeza tena wakati ukiwa umekaribia unakokwenda.

Je, unapokuwa kwenye maongezi, wewe ni msikilizaji mzuri? Je, huwa inatokea unakutana na rafiki yako mchana na mnaongea lakini jioni unapokuwa peke yako unagundua kuwa hukumbuki hata alichosema.

Au inatokea kuwa uko katika gari lako ukiliendesha kuelekea mahali usipopajua bali ulielekezwa tu na hatimaye ukagundua kuwa umepotea. Kisha unaomba msaada njiani na kukuelekeza tena wakati ukiwa umekaribia unakokwenda.

Unaelekezwa na unaendelea hadi unafika njiapanda. Ajabu kabisa unasahau tena ulivyoelezwa kama upinde kulia au kushoto.

Ukweli ni kwamba wengi wetu huwa tunajiamini kama ni wasikilizaji wazuri lakini utafiti umethibitisha kuwa hii sio kweli. Tunahitaji kutambua mbinu zitakazoimarisha uwezo wetu wa kusikiliza na kuyazingatia kwa uthabiti yale tunayoelezwa.

Pamoja na mambo mengi yanayoweza kutujengea uwezo wetu wa kusikiliza tutajadili mambo manne yafuatayo. Mosi, ili uweze kusikiliza kwa makini wengine wanapoongea waachie nafasi ya kueleza hadi neno la mwisho. Epuka tabia iliyozoeleka kwa watu wengi ya kumkatikiza anayeongea.

Tena unapokuwa ukisikiliza usijishughulishe sana na kufikiria utakachomjibu hadi ukashindwa kuzingatia anachosema. Kuwa na uwezo wa kuweka uwiano mzuri kati ya kusikiliza anachosema mtu mwingine na kufikiria kile atakachomjibu au kusema atakapomaliza ni ustadi muhimu sana katika mazungumzo.

Hapana shaka kwa juhudi kila mtu anaweza kuijenga tabia hiyo hadi akaizoea. Pili, zingatia kuwa kila mtu huwa na mtindo wake wa kuongea, kuna wale wanaongea haraka na wale wanaoongea polepole.

Kadri utakavyomudu kupunguza kasi ya mazungumzo ndivyo kadri utakavyoweza kumuelewa vyema zaidi mtu unayeogea naye na aliyeko mbele yako.

Tumia ishara sahihi zinazostawisha maongezi kwani katika mazungumzo watu huvutiwa zaidi na ishara za mwili za muongeaji au msikilizaji kuliko hata maneno anayosema.

Hivyo, hata kama utajitahidi kusikiliza kwa dhati hutaonekana kama uko makini ikiwa utaonekana unatazama vitu vingine kama vile ukuta, dari au hata saa yako.

Kuna watu wenye tabia ya kupandisha na kushusha kichwa chini wanapokuwa wakisikiliza kuonyesha wanaafiki au wanaelewa kinachosema.

Kama ishara za mwili wako zitaonyesha kama hauko makini, mtu yeyote unayeongea naye hatajisika vizuri na pengine utamfanya hata asikueleze mawazo halisi yaliyo katika akili yake. Kila mara kumbuka unapokuwa katika mazungumzo kuna mtu anayefuatilia mwenendo wako na kuchunguza kila unachotenda.

Onyesha unafuatilia kile unachoelezwa katika maongezi huwa na maana maalumu iliyokusuduwa. Msikilizaji aliye makini ataonyesha jinsi anavyoathiriwa na kinachosema kwa kushangaa, kusikitika, kuhamasika na pengine hata kughadhibika.

Mtu anayesikiliza anapoonyesha anafuatilia ujumbe wa kuuliza maswali au kuongezea kwa kile kilichosemwa na mwenzake anaelewa vyema zaidi na kumhamasisha anayesimulia.

Kwa mfano mtu akisema “Sipendi kabisa kazi yangu” Msikilizaji aliye makini hatatosheka na usemi huo kwani atapenda kuelewa zaidi. Ataweza kuuliza maswali kama vile “Kitu gani kinakufanya usiipende?” “Kwani kumetokea nini kazini kwako?” Maswali ya udadisi kama haya humfanya unayeongea naye apate imani kuwa unamsikiliza kwa makini na afurahie zaidi kuongea na wewe. Tena yatakusaidia kuelewa vyema zaidi unachosimuliwa.

Sikiliza kwa shauku ya kujifunza kutoka kwa wengine

Kulikuwa na mtu fulani ambaye alikuwa amekabiliwa na tatizo fulani kwa muda mrefu. Siku mmoja akiwa kwenye kituo cha basi akawasikia watu wakiongea kuhusu lile suala lililokuwa limemtatanisha kwa muda mrefu. Akapata ufumbuzi kutokana na maongezi ya watu wengine. Kwa kawaida tunajifunza mambo mengi kutokana na maongezi. Ukisikiliza kwa shauku ya kutaka kuona utajifunza nini kutokana na maongezi, utagundua kuwa unasikiliza kwa makini zaidi kuliko kawaida.