‘Ndege zinazochelewesha abiria sasa zitozwe faini’

Muktasari:

  • Akizungumza jana katika baraza la wafanyakazi wa mamlaka hiyo, Profesa Mbarawa alisema kuna mambo matatu ambayo wanatakiwa kuangalia ambayo ni kampuni, wananchi na Serikali.

Dodoma. Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ameiagiza Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) kuchukua hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kuzitoza faini kampuni za ndege zinazochelewesha abiria viwanjani.

Akizungumza jana katika baraza la wafanyakazi wa mamlaka hiyo, Profesa Mbarawa alisema kuna mambo matatu ambayo wanatakiwa kuangalia ambayo ni kampuni, wananchi na Serikali.

“Kazi yenu ni kuhakikisha hawa watu wote wanapata haki zao sawasawa. Hatutaki kuona mnawakandamiza wananchi kwa masilahi ya watu wakubwa au wenye kampuni na hatutaki kuona mnawagandamiza watu wenye kampuni kwa sababu sekta haitakua,” alisema.

Alisema usimamizi mzuri utawezesha watu wengi kutumia na kuwekeza katika sekta ya usafiri wa anga.

“Nasikia kuna watu wanalalamika sana huko Mbeya kuna kampuni imewaacha watu (uwanja wa ndege). Namuuliza mdhibiti (TCAA) unasimamiaje sasa? Kwa nini usimtoze faini huyu akajifunza?” alihoji.

Alisema kwa kuwasimamia vizuri na kuwatoza faini kwa mujibu wa sheria hawatarudia kufanya makosa hayo akisema uzoefu umejionyesha katika usimamizi wa kampuni za simu.

Mwenyekiti wa baraza hilo na Mkurugenzi Mtendaji wa TCAA, Hamza Johari alisema wamefanikiwa kununua rada mbili kwa kubana matumizi.

“Nilipongeze baraza hili kwa azimio moja. Tuliamua tujifunge mkanda tununue rada hizi lakini hili waziri limekuwa ni agizo lako kuwa tutumie mapato ya ndani katika kufanya miradi,” alisema.