Njia za panya tishio mafuta ya kula

Muktasari:

Mahitaji ya mafuta ya kula kwa Tanzania ni tani 570,000 kwa mwaka, wakati uzal-ishaji ni tani 210,000 tu. Mafuta mengine tani 360,000 huagizwa kutoka nje ya nchi.

Dar es Salaam. Hatua ya Serikali kupandisha kodi ya kuingiza mafuta ghafi ya kula kutoka nje ya nchi hadi asilimia 35 umesababisha baadhi ya waagiza wa malighafi hiyo nje ya nchi kutumia njia za panya hivyo kuendelea kuathiri soko la ndani.

Hatua ya kuongezwa kwa kodi hiyo kulitokana na agizo la Rais John Magufuli baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika Bandari ya Dar es Salaam Mei 15 na kuziagiza kampuni tatu kulipa asilimia 25 ya kodi baada ya kubaini matanki saba kati ya yaliyokaguliwa yana mafuta safi yanayofaa kwa ajili ya matumizi.

Awali, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilizizuia meli mbili zenye tani 62,000 za mafuta ya kula katika Bandari ya Dar es Salaam ikidai zilikuwa na mafuta yaliyosafishwa (refined) huku wenye mafuta hayo wakidai yalikuwa ghafi.

Baadhi ya wamiliki wa viwanda vya kusafisha mafuta hayo wameliambia Mwananchi kuwa ongezeko la kodi hiyo limesababisha baadhi ya wafanyabiashara kupitishia Bandari ya Zanzibar ambako hulipia Dola 650 kwa tani wakikwepa tozo ya Dola 750 ya Bandari ya Dar es Salaam.

Wamesema baada ya kuyapitishia Zanzibar, wafanyabiashara hao huyaingiza Bara kwa njia za magendo na kusababisha mafuta hayo yasiyolipiwa kodi kufurika sokoni, huku mafuta yao yakikosa soko.

Akizungumza kwa simu, mwenyekiti wa wamiliki wa viwanda vya mafuta ya kula, Hussein Kamote alisema endapo hali hiyo itaendelea, watalazimika kufunga viwanda vyao hali itakayowakosesha ajira mamia ya wafanyakazi na kutokea kwa uhaba wa mafuta hayo nchini.

“Tumejaribu kuzungumza na wenzetu wa Serikali lakini hakuna dalili ya kukubaliwa. Mpaka sasa hatujafunga viwanda lakini tayari kuna athari ya kupungua kwa ‘profit margin’ (faida) na hali ikiendelea hivi tutashindwa ku-operate, tutafunga viwanda,” alisema Kamote.

Akifafanua zaidi, Kamote alisema wakati Tanzania ikipandisha kodi ya kuingiza mafuta ghafi hadi asilimia 35 ya kodi, Kenya yanaingizwa kwa asilimia 0, Uganda wanaingiza kwa asilimia 10 na Rwanda asilimia 0.

Wakati huohuo, alisema kuna mafuta yanayoingizwa kutoka nchi za Afrika Mashariki hasa Kenya kwa kodi ya asilimia 25 na hivyo kuongeza wingi wa mafuta sokoni kwa bei ya chini.

“Kwa hali hiyo sisi hatuwezi kupandisha bei ili kukidhi gharama zetu, kwa sababu tukifanya hivyo mafuta yetu yatadoda sokoni,” alisema.

Alisema tofauti na wafanyabiashara wanaoagiza mafuta safi kutoka Kenya kwa asilimia 25, wao wanaagiza kwa asilimia 35 na wakishasafisha wanapata asilimia 75 ya mafuta safi huku asilimia 25 inabaki kwa matumizi mengine yakiwamo ya kutengeneza sabuni.

“Sasa mwenzako anaingiza mafuta safi kwa asilimia 100 analipa asilimia 25 halafu wewe uliyeingiza kwa asilimia 35 ukisafisha unapata asilimia 75. Hata mkiuza bei sawa tayari wewe una upungufu na ndiyo hasara,” alisema.

Aliongeza: “Lengo lilikuwa ni kulinda viwanda vya ndani, lakini haitasaidia kwa sababu kuna mafuta mengi yanayoingia kwa magendo yapo sokoni. Labda kama wana lengo la kuua viwanda,” alisema.

Tanzania huagiza tani 360,000 za mafuta ya kula nje ya nchi huku pia ikizalisha tani 210,000 wakati mahitaji yakiwa ni tani 570,000 kwa mwaka.

Mmoja wa wamiliki aliyezungumza na Mwananchi kwa simu kwa sharti la kutotajwa jina lake alisema kodi hiyo imesababisha baadhi yao kupitishia mafuta ghafi Bandari ya Zanzibar ambako kuna gharama nafuu.

“Itakuwaje ulipe kodi zote hizo wakati mtu akienda Zanzibar hazipo? Ndiyo maana watu wanaamua kwenda Zanzibar. Bei ya mafuta iko chini na ukishatoa kodi zote hupati chochote,” alisema mfanyabiashara huyo.

Alisema licha ya dhamira njema ya Rais ya kulinda viwanda vya ndani, lakini haitasaidia kwa sababu mafuta hayo yanapitia Zanzibar na kuingizwa nchini kwa njia zisizo rasmi tena bila kulipa kodi.

“Rais aliweka bei ya chini kwa lengo la kulinda viwanda vya ndani na zao la sunflower (alizeti) lakini haitasaidia. Mtu unatoa mzigo Malaysia na Indonesia inabidi upitie Zanzibar kisha unaingia Bara.”

Mfanyabiashara huyo alisema wameshakwenda Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji na TRA kulalamikia kodi hiyo lakini hawasikilizwi.

Mkurugenzi wa Elimu ya Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo alithibitisha tozo ya asilimia hiyo ya kodi akisema iliwekwa kwa lengo la kuzuia udanganyifu wa wafanyabiashara.

“Hiyo kodi iliwekwa kwa sababu kuna wafanyabiashara walikuwa wakisema wanaleta mafuta ghafi, kumbe wanaleta yaliyosafishwa halafu wanapaki upya. Tumezuia hiyo ili walipe kodi,” alisema Kayombo.

Kuhusu asilimia 25 ya kodi inayotozwa kwa mafuta yanayotoka nchini Kenya, Kayombo alisema kodi hiyo inazingatia mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa hiyo hawawezi kuingilia.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Profesa Joseph Buchweshaija alisema wizara hiyo haina taarifa ya kuingia kwa mafuta ya magendo, bali inafuatilia yanayoingia kwa njia rasmi.

Alisema kodi hiyo ya mafuta imewekwa kwa mwaka mmoja ili kuangalia kama italeta mafanikio.

“Hizo tariffs (tozo) zimewekwa kwa ajili ya kulinda viwanda vya ndani. Ni ‘exercise’ (zoezi) ya mwaka mmoja ili tuone kama wafanyabiashara walikuwa waaminifu au vipi,” alisema Profesa Buchweshaija.

Aliwataka wenye viwanda kununua mafuta ghafi kutoka kwa wazalishaji wa ndani badala ya kununua nje ya nchi.

Mwenyekiti wa Chama cha Wazalishaji wa Mafuta wa Ndani, Ringo Iringo aliliambia Mwananchi kwa kuwa uzalishaji wa mafuta unaendelea vizuri na wapo tayari kuuza mafuta kwenye viwanda vinavyoagiza mafuta hayo kutoka nje.

“Uzalishaji unaendelea vizuri ndiyo maana hakuna upungufu wa mafuta. Tatizo tulilonalo ni mbegu bora. Kuna wazalishaji wanaokamua mbegu na kuuza moja kwa moja na wengine wanakamua na kuuza mbegu kwa wenye viwanda,” alisema Iringo.

Alipoulizwa kuhusu mafuta ya magendo yanavyoathiri biashara yao, Iringo alisema wameshindwa kuthibitisha licha ya kuwa na taarifa ya mafuta yanayoingia kutoka Kenya na Uganda.

“Tulifuatilia katika mipaka ya Namanga na Taveta, kote tumeambiwa mafuta yanapita kwenye njia sahihi. Tumeshindwa ku establish (thibitisha) hizo taarifa. Hilo ni suala la Polisi wanaweza kujua,” alisema.

Kamanda wa Kikosi cha Wanamaji cha Jeshi la Polisi, Evans Mwijage alithibitisha kuwapo kwa magendo ya mafuta ya kupikia katika Bahari ya Hindi na kusema kwa Septemba pekee wamekamata zaidi ya madumu 100 yakitokea Zanzibar.

“Hayo ni matukio ya mara kwa mara ila wafanyabiashara hao wameweka watu wa kuwapa taarifa pale Ferry. Boti ya Polisi ikitoka wanawajulisha wasilete, kwa hiyo sisi huwa tunajificha mahali siku mbili tatu ili kuwapoteza na ndipo tunapowavizia. Wanapenda kushushia mafuta hayo maeneo ya Mlingotini wilayani Bagamoyo na Ununio (Dar es Salaam),” alisema Kamanda Mwijage.