Polisi yashikilia 20 kutekwa kwa MO Dewji

Mohamed Dewji ‘MO’

Muktasari:

  • Mohamed Dewji ‘MO’ alitekwa juzi saa 11 alfajiri wakati akienda kufanya mazoezi kwenye gym iliyoko katika Hoteli ya Colosseum. Polisi imeanza msako mkali kwa ajili ya kufahamu aliko mfanyabiashara huyo maarufu Tanzania na Afrika.

Dar es Salaam. Polisi inawashikilia Watu 20 wakihusishwa na tukio la utekaji wa mfanyabiashara maarufu na mfadhili wa klabu ya Simba, Mohammed Dewji’MO’.

Mo alitekwa JumatanO alfajiri wakati akienda katika mazoezi(gym) katika Hoteli ya Colosseum jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola alisema jana kuwa Jeshi la Polisi wanaendelea kumtafuta Mo Dewji na kuwasaka wote walimteka.

“Niwahakikishie Watanzania, Jeshi la Polisi linaendelea kumtafuta Mo Dewji na pia wanaendelea kuwasaka waliomteka mpaka kuhakikisha wanapatikana.

“Wamejipanga vizuri na mpaka sasa ninapozungumza takribani watu 20 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi na wanaendelea kuhojiwa na wengine wanaendelea kusaidia kutoa angalau wanajua nini kinachoweza kusaidia jeshi la polisi

“Nimemuelekeza Inspekta wa Polisi (IGP), Simon Siro kuwa licha ya kwamba watawakamata hawa watu wengi juu ya kupata ushahidi wa kupelekea kumpata Mo Dewji waendelee kuchambua haraka iwezekanavyo na wasiendelee kumshikilia mtu zaidi ya masaa 24.

“Ambaye wamechambua na wakaona hakuna muelekeo waweze kumuachia mara moja,”alisema Lugola.

Pia Lugola amewakumbusha Watanzania kuendelea kutoa taarifa za uhalifu,kuwepo mipango ya uhalifu wa aina yoyote ikiwemo uhalifu wa utekaji wa watu,kwenye vyombo vya usalama,vituo vya polisi vilivyoko karibu huku akiwaonya kutumia vizuri mitandao ya kijamii.

“Nawaomba Watanzania waendelee kutumia mitandao ya kijamii kwa uangalifu kwa sababu wasipotumia mitandao ya kijamii kwa uangalifu wataweza kuitumia mitandao hii kwa uchochezi, upotoshaji wataendelea kutumia mitandao hii kwa kujenga hofu kwa watanzania hivyo kuleta sintofahamu miongozi mwa watanzania.

“Taarifa ambazo ni rasmi kuhusiana na matukio ya kiuhalifu ama matukio ya utekaji wa watu zitaendelea kutolewa na jeshi la polisi hapa nchi na si vinginevyo” alisema.

Juzi msemaji wa Simba,Haji Manara alikamatwa na Polisi kwa madai ya kutumia vibaya mitandao ya kijamii.