Rais Magufuli ampa pole Kamishna Jenerali mpya wa Magereza

Raisi Magufuli akimvisha cheo Kamishna Jenerali mpya wa Magereza, Phaustine Kasike.

Muktasari:

  • Kiongozi mkuu huyo wa nchi alitoa kauli hiyo Ikulu jijini Dar es Salaam katika hafla fupi ya kumuapisha Kamisha Jenerali Kasike na Balozi Joseph Sokoine ambaye ameteuliwa kuwa naibu katibu mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).

Dar es Salaam. Rais John Magufuli jana alitumia dakika 20 kueleza mambo asiyopendezwa nayo ndani ya Jeshi la Magereza na kumtaka Kamishna Jenerali mpya wa jeshi hilo, Phaustine Kasike kuyafanyia kazi huku akirudia kumpa pole mara nne.

“Nakupongeza kidogo, lakini pole ndio nyingi,” alisema.

Kiongozi mkuu huyo wa nchi alitoa kauli hiyo Ikulu jijini Dar es Salaam katika hafla fupi ya kumuapisha Kamisha Jenerali Kasike na Balozi Joseph Sokoine ambaye ameteuliwa kuwa naibu katibu mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).

Katika maelekezo yake, Rais Magufuli alimtaka Kasike kuhakikisha wafungwa wanafanya kazi ipasavyo, wazuie matumizi ya simu gerezani, washiriki katika shughuli za kilimo na ujenzi, wazuie kufanya biashara na kushiriki katika matukio ya wizi wakiwa gerezani.

“Ni aibu nchi kuendelea kulisha wafungwa, maeneo ya magereza ni mengi mno ukienda kule Mbeya mashamba yanalimwa robo tu, kila mahali kuna magereza na maeneo ya mashamba, lakini kila mwaka kunakuwa na maombi ya bajeti kulisha wafungwa,” alisema Rais Magufuli.

“Maana ya kufungwa ni ukafanye kazi, maaskari magereza kazi yao ni kuwafanya wafungwa wafanye kazi, ndio maana wengine wanahukumiwa na kuchapwa fimbo ziwachangamshe wakafanye kazi.”

Alisema kutokana na wafungwa kutofanyishwa kazi ipasavyo, anashangaa wakati mwingine kamishna jenerali anaomba msaada wa fedha za kununua matofali, jambo alilosema kuwa ni la aibu kwani wafungwa wana uwezo wa kufyatua matofali.

“Unakuta hata maaskari na watumishi hawana nyumba za kukaa na wafungwa wapo tena wa bure kabisa ambao unaweza kuwaambia wafyatue matofali na teke ukawapiga. Askari huna pa kulala na wafungwa wapo, lakini unawatafutia Bajeti ya Serikali,” alisema.

Huku akimtaka Kasike kusimamia hilo, Rais Magufuli alisema hataki kusikia mfungwa aliyehukumiwa kwa ujambazi anashikwa akishiriki kuua tembo.

“Sitaki kusikia mfungwa aliyeacha familia yake nyumbani anakuja mke wake gerezani na tena anakaribishwa na askari wa magereza ili wafanye mambo ambayo mfungwa hatakiwi kuyafanya gerezani,” alisema.

“Sitaki kusikia kwenye gereza wafungwa wanawasiliana na jamaa zao kwa kutumia simu, simu zimejaa kwenye magereza tena magereza za Dar es Salaam wanazungumza na simu mpaka nje ya nchi.”

Alisema hataki kuona wafungwa wanapata nguvu ya kuvuta bangi na kujamiiana na kubainisha kuwa hali hiyo inatokea kwa sababu hawafanyi kazi za kutosha.

“Sitaki kusikia mfungwa anafuga mbuzi na ng’ombe akiwa gerezani na kupeleka kwenye mnada na anakuwa tajiri kuliko hata askari. Nina mifano ya kila gereza,” alisisitiza.

Huku akimtaka kuhakikisha mambo hayo yanadhibitiwa Rais Magufuli alisema, “Ndio maana nakueleza Kamishna Jenerali nakupongeza, lakini pongezi zangu ni kidogo pole ndio nyingi. Najua kuna askari watakuchukia kwa hatua utakazozichukua lakini usipochukua hatua mimi utanichukia. Nataka maaskari wangu wakafaidike.”

Pia, aligusia kitendo cha Jeshi la Magereza kutokuwa na matrekta wakati Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), limekopesha matrekta hadi wananchi.

“Hawakukopa, lakini wanalalamika hakuna vitendea kazi. Sioni sababu ya Magereza kukosa pesa. Mkijipanga vizuri… litakuwa jeshi la mfano kwa maendeleo ya nchi hii. Kamishna nenda ukazikabili hizi changamoto,” alisema.