Saccos ziwanufaishe wanachama kwa njia hii

Muktasari:

  • Kwenye kila changamoto, watu hutafuta mbadala kufanya maisha yaendelee. Licha ya kuwapo kwa benki nyingi za biashara nchini, watu wanaohudumiwa ni chini ya asilimia 20 kutokana na masharti magumu yanayowakimbiza wengi. Vyama vya kuweka na kukopa vinapaswa kuongeza ubunifu ili wanachama wake wanufaike zaidi.

Dhima kuu ya vyama vya ushirika wa akiba na mikopo (saccos) ni kukusanya fedha chache kutoka kwa wanachama na kuzigawanya kwa utaratibu mzuri ili zitumike kwenye mambo yatakayosaidia ukuaji na kustawisha uchumi wa wanachama na mambo mengine ya kijamii.

Kumekuwapo na changamoto kubwa hasa kwenye masuala ya fedha za vyama hivi yaliyochangia kuviingiza kwenye migogoro na kuleta kutoelewana kati ya bodi ya chama, watendaji na wanachama wenyewe.

Uwekezaji kwenye rasilimali za muda mrefu kama vile ujenzi wa majengo, ununuzi wa viwanja na minada ya rasilimali zisizohamishika imekuwa haina tija sana kwa ukuaji wa taasisi hizi kwa sababu hakuna uhusiano wa moja kwa moja na uboreshaji wa huduma na bidhaa za chama ambacho ndicho kitovu cha biashara na zinategemewa kuwanufaisha wengi.

Kumekuwa na harufu ya rushwa na ubadhilifu wa fedha na mali za chama hata kusababisha kuingia kwenye migogoro.

Ili tuondoke kwenye changamoto hii ni vyema viongozi wa bodi na wanachama wakafahamu kufanya uwekezaji mkubwa na kuboresha huduma zao ziwe bora na zinazoenda na wakati.

Chama kinahitaji kukazania biashara ya msingi ili kuwa na huduma nzuri zenye ubora kwa wanachama, lakini uwekezaji mzuri zaidi ni kuboresha huduma za taasisi kila wakati badala ya kuhamisha faida na mtaji kutengeneza majengo au kufanya uwekezaji mwingine.

Ikumbukwe kuwa kazi kubwa ya chama ni kukusanya fedha na kuzitawanya kwa wahitaji wake ili wabadilishe maisha yao kwani hii ndiyo biashara kubwa na kukimbiza rasilimali kwenye mambo mengine kunaharibu msingi wa chama.

Mfano mzuri ni benki za biashara ambazo hazina uwekezaji kwenye majengo au viwanja, bali zinahakikisha mteja anapata huduma wakati wote anapohitaji na huduma na bidhaa zao ni za kisasa kukidhi mahitaji ya soko la sekta ya fedha.

Unapowekeza kwenye ununuzi wa viwanja 500 wakati chama kina wanachama 5,000 maana yake utatoa huduma hii kwa wanachama wachache na kuwaacha wengine nje.

Hata uwekezaji wa muda mrefu kama ujenzi wa majengo vinawaacha baadhi ya watu nje ya manufaa kwa kuwa faida yake hupatikana baadaye sana.

Biashara nyingine zinaua lengo mama ya Saccos. Inapaswa kukumbuka kuwa kuwekeza zaidi nje ya biashara ya msingi kunaifanya biashara kuu kupunguza mwitikio na mvuto.

Vilevile, uwekezaji kwenye ardhi kunaweza kuiingiza saccos kwenye migogoro ya kisheria kwa kuwa hiyo ni miongoni mwa maeneo yenye migogoro mikubwa kutokana na changamoto za umiliki, sheria za mipango miji na matumizi bora ya ardhi. Chama kikishindwa kufuata utaratibu huo basi kinaweza kuingia kwenye migongano ya kisheria kati yake na Serikali, watu binafsi au taasisi.

Siyo dhambi kwa chama cha kuweka na kukopa kuwekeza katika maeneo mengine kwa kuzingatia mazingira bila kuathiri utoaji wa huduma za msingi kwa wanachama ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Saccos nyingi hivi sasa zimeamua kutafuta fedha kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo kuuza hisa mpya kwa wanachama ili kununua ardhi na kujenga majengo ambayo ni vitega uchumi vya pembeni vinavyovuna faida na matumizi yake hayaathiri utoaji huduma za msingi kwa wanachama.

Hassani ni mdau wa sekta ndogo ya fedha. Anapatikana kwa simu namba 0657-157122 au [email protected]