Samia Suluhu mgeni rasmi kongamano la 30 la Sayansi

Makamu wa Rais,  Samia Suluhu .

Muktasari:

  • Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR),  Dk Mwele Malecela alisema Kongamano hilo limeandaliwa na taasisi  hiyo kwa  ajili ya kujadili Mikakati ya afya ya uzazi ya mama, watoto wachanga, na vijana.

Dar es Salaam. Makamu wa Rais,  Samia Suluhu anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Kongamano la 30 la Sayansi litakalofanyika Jumanne ijayo jijini hapa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR),  Dk Mwele Malecela alisema Kongamano hilo limeandaliwa na taasisi  hiyo kwa  ajili ya kujadili Mikakati ya afya ya uzazi ya mama, watoto wachanga, na vijana.

Kadhalika kongamano hilo litajadili kuhusu magonjwa sugu yasiyoambukiza, Magonjwa ya kitropiki yasiyopewa kipaumbele,  usalama wa maji,  usafi wa mazingira pamoja na kuendeleza Mafanikio yaliyopatikana katika mapambano dhidi ya Ukimwi, kifua Kikuu na Malaria.

"Lengo la Kongamano hili ni kuwakutanisha watafiti,  watoa huduma za afya, watunga sera,  wakufunzi na wadau wengine wa afya katika kubadili matokeo ya tafiti mbalimbali za afya zinazofanyika nchini"alisema Dk Malecela.

Alisema jumla ya mada 220 zitawasilishwa katika Kongamano hilo huku mada kuu ikiwa ni 'Uwekezaji katika tafiti zenye ubunifu ili kufikia malengo endelevu ya Dunia'

Washiriki 300 kutoka nchi 18 duniani watashiriki Kongamano hilo