Saratani sasa kuanza kugundulika siku tatu

Katibu mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Mpoki Ulisubisya

Muktasari:

  • Hivi sasa, mgonjwa akipimwa maradhi hayo majibu huyapata baada ya wiki mbili, lakini kwa mashine hiyo majibu yatapatikana ndani ya siku tatu.

Dar es Salaam. Chama cha Wataalamu wa Patholojia kutoka Marekani kimetoa mashine ya kupima saratani itakayosaidia kupunguza muda wa kutoa majibu baada ya vipimo.

Hivi sasa, mgonjwa akipimwa maradhi hayo majibu huyapata baada ya wiki mbili, lakini kwa mashine hiyo majibu yatapatikana ndani ya siku tatu.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa kifaa hicho, katibu mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Mpoki Ulisubisya alisema inagharimu zaidi ya Sh308 milioni.

“Mashine hii itasaidia kupunguza muda ambapo utaratibu wa kusema baada ya mwezi mmoja mgonjwa afuate majibu hiyo itakuwa historia,” alisema Dk Ulisubisya na mashine hiyo itafungwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Alisema tatizo kubwa lililopo nchini ni kuongezeka kwa kasi kwa saratani kwani takwimu za 2005 zinaonyesha watu 2,500 waliugua maradhi hayo, lakini hadi kufikia 2017 wagonjwa walifikia 43,600.

Daktari bingwa wa uchunguzi wa saratani kutoka kitengo cha Patholojia Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Leah Mnanga alisema mashine hiyo itawasaidia kusoma kidigitali majibu ya vipimo vyote. “Hii mashine itakuwa na uwezo wa kuhifadhi taarifa zote za sampuli za vinyama (vinavyochukuliwa kwa ajili ya vipimo) tofauti na njia nyingine iliyokuwa inatumika,” alisema Dk Mnanga.